Loading...

Mashirika manne kikaangoni kwa upotevu wa mabilioni.

Makamu Mwenyekiti wa PAC, Aeshi Hilary.
WAKATI Rais John Magufuli akitumia mbinu mbalimbali kubana matumizi ya serikali, vikao vya kamati za bunge vinavyoendelea mjini Dodoma, vimeonyesha namna serikali inavyopoteza mabilioni ya fedha kupitia bodi za mashirika mbalimbali na matumizi mengine yasiyo na tija.

Taarifa za taasisi mbalimbali zilizowasilishwa mbele ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), zimeonyesha kuwa fedha zinazotumika kugharamia vikao vya bodi zimekuwa zikiongezeka maradufu huku kukiwa hakuna majibu ya kujitosheleza.

Madudu hayo yamebainishwa katika taarifa za fedha za mashirika hayo zilizowasilishwa mbele ya PAC tangu ilivyoanza vikao vyake Agosti 15 mjini hapa.

Kutokana na ripoti hizo, Makamu Mwenyekiti wa PAC, Aeshi Hilary, mwishoni mwa wiki 
alisema kuwa kamati yake haitafumbia macho matumizi yoyote mabaya ya fedha na watapeleka ripoti bungeni ili chombo hicho kiamue cha kufanya juu ya taasisi zinazotafuna fedha za umma. 

"Lengo letu ni kila senti itumike kwa maslahi ya umma, hayo mambo unayosema, yapo ambayo tumetaka taarifa za kina na mengine tutayaweka kwenye ripoti yetu tutakayowasilisha bungeni ili uamuzi uchukuliwe," alisema Aeshi ambaye pia ni Mbunge wa Sumbawanga Mjini (CCM).

Baadhi ya taasisi ambazo matumizi yake ya bodi yameonekana kupanda huku kukiwa hakuna maelezo ya kujitosheleza ni Mamlaka ya Ustawishaji Mji wa Dodoma (CDA) ambayo mwaka 2014 ilitumia Sh. milioni 48 na mwaka 2015 ikatumia Sh. milioni 124 kwa kufanya vikao sita pekee.

Bodi nyingine ni ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ambayo mwaka 2014 ilitumia Sh. milioni 150 na mwaka 2015 ikatumia Sh. milioni 250.

Katika vikao vya kamati hiyo, baadhi ya wajumbe walihoji kuongezeka huko kwa fedha huku wahusika wakiwa hawana majibu.

Mbali na bodi hizo, baadhi ya mashirika yameonekana kuingizia serikali hasara ya mabilioni ya shilingi kwa kuwekeza kwenye miradi ambayo mpaka sasa haijaanza kufanya kazi na mingine imekufa.

Moja ya taasisi hizo ni Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) ambalo limetumia mabilioni ya shilingi kuwekeza kwenye miradi ambayo licha ya kukaa kwa muda mrefu, mpaka sasa haijaanza kufanya kazi.

Shirika hilo ambalo PAC ilikataa kujadili hesabu zake kutokana na upungufu uliojitokeza, limewekeza Sh. bilioni tatu katika kiwanda cha matairi cha General Tyre cha mkoani Arusha, lakini shirika hilo halijui zilivyotumika.

Shirika hilo pia limewekeza Sh. milioni 469 kwenye mradi wa umeme wa upepo Singida na sasa mradi huo umefutwa.

Shirika hilo pia limetumia Sh. bilioni 2.3 kwenye mradi wa magadi soda uliopo Engaruka, Arusha na mpaka sasa haujaanza.

Taarifa hizo pia zinaonyesha shirika hilo limetumia takriban Sh. bilioni 60 kwenye kiwanda cha kutengeneza viwatilifu vya kuua mbu cha Kibaha na mpaka sasa hakijaanza kufanya kazi.

Kwa mwaka wa fedha uliopita pekee, shirika hilo lilitumia Sh. bilioni 20 kwenye kiwanda hicho.

PAC haikuweza kujadili hesabu za shirika hilo na badala yake watendaji wake walirudishwa ili waandae hesabu zao na zionyeshe ni kwa namna gani fedha hizo za umma zimetumika.

Kwa upande wa TBC, taarifa za hesabu zake zinaonyesha shirika limefanya uwekezaji wa Dola za Marekani 350,000 kwenye kampuni ya Star Media waliyoingia nayo ubia, lakini mpaka sasa shirika hilo halipati gawio.

Pia hesabu hizo zinaonyesha TBC imeilipia Star Media ada ya Sh. milioni 689 kwenye Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), jambo ambalo halikutakiwa.

Kutoka na hali hiyo, PAC iliagiza TBC kuandaa ripoti itakayoonyesha namna shirika hilo litakavyofaidika na ubia huo.

Mkurugenzi wa TBC, Dk. Ayubu Rioba, aliiambia kamati kuwa mwanzo ilitarajiwa Star Media ingepata faida kwa watu kulipia ving'amuzi, jambo ambalo ni tofauti na sasa ambao wengi hawalipii. Kwa upande wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), hesabu zake zinaonyesha kimewekeza Sh. bilioni 4.7 kwenye akaunti maalum yenye riba wakati ikishindwa kutembelea taasisi kinazozipa msamaha wa kodi kuona kama zinatumika kama ilivyokusudiwa.

Source: Nipashe
ZeroDegree.
Mashirika manne kikaangoni kwa upotevu wa mabilioni. Mashirika manne kikaangoni kwa upotevu wa mabilioni. Reviewed by Zero Degree on 8/29/2016 10:07:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.