Loading...

Mchezaji anayekipiga Italia aitwa Taifa Stars.

Said Mhando.
KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars, Charles Mkwasa ameita kikosi cha wachezaji 22 kambini akiwemo mchezaji Said Mhando anayecheza Brescia Calcio ya ligi daraja la pili ‘Serie B’ Italia.
Kikosi hicho kinatarajiwa kuingia kambini Jumapili ya wiki hii kujiandaa na mechi ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa Afrika dhidi ya Nigeria Septemba 3 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkwasa alisema wamemuona mchezaji huyo Mtanzania anayecheza ligi ya Serie B hivyo wamemwita na wanaamini atawasaidia kwa vile ana umri wa miaka 19.

Akimzungumzia zaidi mchezaji huyo, Mkwasa alisema walipata taarifa zake kutoka kwa wadau wa soka na kuamua kumfuatilia ambapo waligundua baba wa mtoto huyo ni Mtanzania na mama yake ana asili ya Kisomali. Timu ya Brescia Calcio ilianzishwa mwaka 1911 na kwa sasa inafundishwa na kocha Cristian Brocchi raia wa Italia mwenye umri wa miaka 40.

Baadhi ya wachezaji nyota waliowahi kuchezea timu hiyo ni kocha wa sasa wa Manchester City, Pep Guardiola, Roberto Baggio, Gheorghe Hagi, Luca Toni na Andrea Pirlo. Kwa mujibu wa tovuti ya klabu hiyo, mchezaji huyo ametambulishwa kwa jina la Mhando Carte Said akicheza nafasi ya kiungo mshambuliaji na amezaliwa Aprili 15, 1997.

Aidha katika kikosi hicho cha Mkwasa mshambuliaji wa TP Mazembe ya Congo DR, Thomas Ulimwengu hatokuwepo kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya nyama ya paja. Mechi hiyo ya kukamilisha ratiba kwa Stars imepanga kuchezwa mjini Lagos, Nigeria.

Tayari Kocha Mkwasa alisema mchezo huo wa kukamilisha ratiba ni muhimu kushinda ili kuiweka Tanzania kwenye nafasi nzuri katika ubora wa viwango vya Fifa.

“Timu itaingia kambini Agosti 28, itakaa kambini kwa siku tano kabla ya kusafiri kucheza mchezo huo wa kukamilisha ratiba ambao Misri tayari wameshafuzu fainali za Afrika,” alisema Mkwasa.

Wachezaji walioitwa kwenye kikosi hicho ni makipa Deogratius Munishi, Aishi Manula, mabeki ni Kelvin Yondani, Vincent Andrew, Mwinyi Haji, Mohamed Hussein, Shomari Kapombe na David Mwantika.

Viungo ni Himid Mao, Shiza Kichuya, Ibrahim Jeba, Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Juma Mahadhi, washambuliaji ni Simon Msuva, Jamal Mnyate Ibrahim Ajib na John Bocco.

Pia amewaita wachezaji wanaosakata soka la kulipwa nje ya nchi, Mbwana Samatta anayecheza CK Genk na Farid Mussa anayetarajiwa kujiunga na Tenerif ya Hispania.

Mkwasa alisema Farid Mussa ameshapata ITC ya kwenda kucheza Hispania na muda wowote ataondoka baada ya timu yake kukamilisha taratibu za uhamiaji na kibali cha kwenda kufanya kazi hivyo ameona siyo busara kumwacha kwenye mchezo huu.

“Farid hajacheza mchezo wowote na Azam FC ila kwa kutambua kuwa ameshapata ITC nimeona siyo busara kumwacha kwani timu yake inaweza kusema kiwango chake kimeshuka ndio maana hata timu ya taifa ya kwao ameachwa,”alisema Mkwasa.

ZeroDegree.
Mchezaji anayekipiga Italia aitwa Taifa Stars. Mchezaji anayekipiga Italia aitwa Taifa Stars. Reviewed by Zero Degree on 8/25/2016 10:38:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.