Loading...

Mkakati wa kuzuia bidhaa feki za China nchini uko jikoni.

SERIKALI inaandaa mkakati wa kuhakikisha bidhaa feki kutoka China haziuzwi tena nchini.

Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji iko kwenye mazungumzo na serikali ya China ili kupata njia bora ya kuzuia bidhaa bandia na hafifu kutoka huko kuingizwa soko la Tanzania.

Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Adelhelm Meru, aliyasema hayo wiki hii katika mahojiano maalum na waandishi wa habari, kuhusu utekelezaji wa sera, mipango na usimamizi wa sheria unaofanywa na Serikali ya Tanzania kuelekea kuwa nchi ya viwanda.

“Tanzania tunafanya mazungumzo na China ili kufanikisha makubaliano kati ya TBS (Shirika la Viwango Tanzania) na Shirika la Ukaguzi la China ili wasaidie kwenye ukaguzi wa bidhaa za China kabla hazijapakiwa kwenye meli kusafirishwa kuja Tanzania.

Kwa sasa tunashirikiana na kampuni mbili za ukaguzi za SGS na Bureau Veritas ambazo zipo duniani kote,” alisema Dk. Meru.

Dk. Meru alisema mazungumzo yamefikia hatua nzuri na kwa sasa mkataba wa makubaliano (MoU) unafanyiwa kazi, ukikamilika utasainiwa na lengo ni utekelezaji wake kuanza kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Alisema kuwa katika makubaliano hayo Tanzania itatoa viwango vya ubora (specification) inayotaka kwa kila bidhaa, na kuhakikisha bidhaa zinazoingia ni ambazo ubora wake umeshakubalika, utaratibu ambao unatumiwa pia na nchi za Ulaya na Marekani.

“Kwa kuwa bidhaa nyingi zinazoingia nchini mwetu kwa sasa zinatoka China, chini ya makubaliano hayo ni lazima zikaguliwe kulekule kabla ya kupakiwa kwenye meli kuja nchini,” alisema.

Dk. Meru aliendelea kueleza kuwa kampuni hizo ni kubwa, lakini kuna baadhi ya nchi ukaguzi unachukua muda mrefu kwa kushindwa kuwafikia wadau wote kwa haraka kutokana na kampuni kuwa kwenye mji mmoja.

“Tunalenga kupanua zaidi ili TBS waweze kushirikiana na taasisi nyingine za udhibiti wa ubora, bidhaa zote zikaguliwe kabla hazijaingia nchini,” alisema Dk. Meru.

Aliongeza kuwa kinachofanywa kwa sasa ni ukaguzi kwenye masoko na kukamata bidhaa bandia na hafifu. Alisema TBS inaongezewa nguvu ili kuyafikia maeneo mengi nchini na kutumia vifaa vya kisasa.

Wakati wa Bunge la Bajeti, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa ifikapo Julai Mosi, mwaka huu (siku ya kwanza ya mwaka wa fedha 2016/17), atafanya ukaguzi Kariakoo na maeneo nchini kukamata bidhaa zisizo na ubora zilizosheheni.

Alisema anatambua uwapo wa bidhaa hizo katika soko la Tanzania na mipango inaandaliwa kukamata na kuchukua hatua madhubuti kwa waingizaji ikiwamo kuziba mianya ya uingizaji bidhaa hizo.

“Unapokuwa na uwezo wa kukagua bidhaa za nje kwa mfumo wa kompyuta, inarahisisha kazi kwa kuwa tangu mzigo unapakiwa inajulikana na unapofika inakuwa suala la ukaguzi wa kujiridhisha zaidi,” alisema.

Dk. Meru aliendelea kueleza kuwa ukaguzi unapofanyika kwa ushirikiano kuanzia mzigo unapotokea, unasaidia kupunguza uzito wa kazi na kuchelewesha mizigo bandarini.

TBS YAAJIRI WATUMISHI 200

Alisema katika kuimarisha uwezo wa utendaji wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), watumishi 200 waliongezwa katika mwaka wa fedha 2015/16.

Ili kuidhibiti vizuri mipaka ya Tanzania katika uingizwaji wa bidhaa feki na hafifu, Dk. Meru alisema wamepanga kufungua ofisi hivi karibuni katika maeneo ya mipaka ya Mtukula, Tunduma na Kasumulu.

Katibu Mkuu huyo alisema kwa sasa TBS ina ofisi kwenye Bandari ya Tanga, mpaka wa Holili (Kilimanjaro), Namanga (Arusha) na Sirari (Mara).

Kadhalika, alisema shirika hilo linajipanua zaidi na kwa sasa lina watumishi kwenye viwanja vya ndege vilivyopo nchini.

Alisema malengo ya muda mrefu ni kuhakikisha mipaka yote inakuwa na wafanyakazi wa TBS ili kudhibiti bidhaa bandia na zisizo na ubora ambazo nyingi zinapotishwa katika mipaka na njia za panya.

“Hata kama ni mtumishi mmoja kulingana na ukubwa wa mpaka ni lazima kuwe na mtu wa TBS," alisema.

Dk. Meru alisema wanashirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Tume ya Ushindani (FCC) na halmashauri katika kudhibiti na kukamata bidhaa ambazo si salama kwa afya za walaji kwa kuwa “haiwezekani kila kona ya nchi kuwa na mtumishi wa TBS.”

Katibu Mkuu huyo, alisema bidhaa zinazoingia nchini na kubainika ziko chini ya kiwango au bandia hurudishwa zilikotoka na zinapokamatwa sokoni huteketezwa.

BIDHAA ZILIZOKAMATWA HIVI KARIBUNI

Katika kipindi cha miezi sita iliyopita, meli moja iliyokuwa na mafuta yaliyokuwa chini ya kiwango yakitokea Uarabuni ilirudishwa ilikoyatoa (Dubai).

Dk. Meru alisema bidhaa bandia nyingi hupita njia za panya kwa kusafirishwa kwa majahazi kipindi cha usiku na kuhifadhiwa kwenye nyumba za watu.

Alisema serikali inapambana na kadhia hiyo kwa kutumia mbinu mbalimbali zinatumika kukamata bidhaa hizo.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk. Egid Mubofu, alisema katika kipindi cha kuanzia Januari hadi sasa, bidhaa bandia zilizokamatwa ni betri za umeme nuru 593, dawa ya mbu aina ya Heat katoni 2,474, mabati 28,000 na taulo za kike (pedi) katoni 13,211.

Nyingine ni mitumba ya nguo za ndani tani 6.9, 'ice cream' 1,260, mchele kilo 500, matairi yaliyotumika 1,250, mikate 593, vilainishi vya mitambo na magari lita 21,587 na mafuta ya petroli yenye ujazo wa metriki tani 38,521.018.

“TBS imefanikisha zoezi hili kutokana na kampeni maalum iliyoanza Januari mwaka huu ya kuondoa bidhaa hafifu sokoni. Kampeni hii bado inaendelea nchi nzima na pia inaenda sambamba na usitishwaji wa uzalishaji wa bidhaa zisizokidhi matakwa ya viwango vya bidhaa husika vya kitaifa mpaka hapo wazalishaji watakapofuata utaratibu wa kuzalisha kwa kuzingatia viwango,” alisema.

Credits: Nipashe
ZeroDegree.
Mkakati wa kuzuia bidhaa feki za China nchini uko jikoni. Mkakati wa kuzuia bidhaa feki za China nchini uko jikoni. Reviewed by Zero Degree on 8/26/2016 09:25:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.