Loading...

Mtikisiko Polisi.

Ni mtikisiko! Hivyo ndivyo yeyote anavyoweza kueleza kuhusiana na uamuzi mzito uliochukuliwa na Jeshi la Polisi wakuwaengua watumishi wake zaidi ya 600 wasio kuwa askari.

Uamuzi huo ni utekelezaji wa agizo walilopewa Julai 18 mwaka huu na Rais John Magufuli, la kuhakikisha kuwa wanabaki na watumishi askari katika kila eneo, lengo likiwa ni kuepuka kuchafuliwa kwa taarifa za kuwapo kwa vitendo vya rushwa na ufisadi vinavyodaiwa kufanywa zaidi na watumishi walio raia wakawaida ndani ya jeshi hilo.

Magufuli alitoa agizo hilo wakati akizungumza na Naibu Makamishna wa Polisi 25 na Makamishna Wasaidizi wa Polisi 35, Ikulu Jijini Dar es salaam mara baada ya askari hao kula kiapo cha uadilifu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira, alisema tayari mchakato wa kutekeleza ushauri wa Rais Magufuli kwa kubainisha majina ya watumishi hao (zaidi ya 600) na kuyawasilisha Wizara ya Utumishi kwa hatua ya kuwaondoa katika orodha ya watumishiwa Jeshi la Polisi.

Meja Jenerali Rwegasira aliongeza kuwa majina hayo ya watumishi wasio kuwa polisi ya meshawasilishwa kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi, Angela Kairuki.

“Tayari mchakato umefanyika na zaidi ya watumishi raia wakawaida 600 tumeshapeleka majina yao Utumishi kwa ajili ya kuwaondoa kama Mheshimiwa Rais alivyoagiza,” alisema Meja Jenerali Rwegasira.

Akifafanua zaidi, Rwegasira alisema watumishi raia watakaoonekana kuwa wanapaswa kubaki ndani ya jeshi hilo kutokana na weledi wao mbalimbali, watawabakiza kwa sharti kwamba nilazima waende kuhudhuria mafunzo na kufuzu ili wawe na sifa za kuwa askari.

“Wale ambao wanafaa na kukubaliwa watapewa nafasi ya kwenda kuchukua mafunzo ya Jeshi… siyo kwamba sasa kuna watu wamepelekwa kuchukua mafunzo.

Nasema ikitokea nafasi wanaweza kupelekwa na yeyote atakayetoka kwenye mafunzo hayo atalazimika kufanyakazi kwa kufuata vyeo vya Jeshi la Polisi,” alisema.

Hivi karibuni, Jeshi la Polisi limekuwalikikumbana na taarifa mbaya za kuwapo kwa vitendo kadhaa vya rushwa na ufisadi, baadhii vikiwa ni kulipwa mamilioni ya fedha za posho maalumu wanazopata askari kwa watumishi wasio kuwa askari na pia madai ya jeshi hilo kuingizwa katika mikataba mbalimbali isiyo kuwa na maslahi kwao (polisi) nataifa.

Aidha, ni wazi kuwa uamuzi huo wa kuwaondoa watumishi wote raia ndani ya jeshi hilo utawaacha baadhi yao wakipata mshituko, wakiwamo wale waliotumikia jeshi hilo kwa muda mrefu katika fani mbalimbali zikiwamo za uhasibu, ufundi mbalimbali, udaktari wa binadamu, ufundi na wale wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

“Hili ni pigo kubwa kwa baadhi ya watumishi hao raia kwa sababu sasa hatima yao itategemea maamuzi ya Wizara ya Utumishi. Sijui itakuwaje… lakini ukweli ni kwamba Rais yuko sahihi. Kuna watu wasio kuwa askari walikuwa wakijisahau na kuchafua mwenendo wa jeshi kutokana na kutanguliza zaidi maslahi yao binafsi,” chanzo kilisema hayo jana.

WAZIRI UTUMISHI ANENA


Alipoulizwa jana kuhusu suala hilo, Waziri Kairuki alisema ni kweli amepokea majina ya wahusika wote na hatua zaidi zinaendelea kuchukuliwa.

Aliongeza kuwa, hatua kama hiyo inachukuliwa pia katika majeshi mengine baada ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa kuwasilisha orodha ya watumishi raia 100 ambao wanatakiwa kuondolewa.

AGIZO LA MAGUFULI

Wakati akitoa agizo la kutaka Jeshi hilo lijiweke mbali na ufisadi kwa kuondoa watumishi wasio kuwa askari pindi wakiona kunaumuhimu wa kufanya hivyo, Magufuli aliagiza pia Jeshi hilo lichukue hatua dhidi ya wote wanaokabiliwa na tuhuma za wizi wa fedha wakiwamo wanaodaiwa kuiba fedha zilizotolewa kwa ajili ya ununuzi wa sare za askari mwaka 2015.

"Kama mnafikiri kuwa na raia katika Jeshi la Polisi kuna waharibia kazi zenu waondoeni na muwapeleke utumishi…kwani hakuna Mhasibu ambaye ni askari polisi? Hakuna Mhandisi ambaye ni askari polisi? Hakuna Afisa Tawala ambaye ni askari polisi? Mimi nafikiri kama matatizo ya wizi na wafanyakazi hewa yanaletwa na raia waliomo ndani ya Jeshi la Polisi …IGP kaorodheshe raia wote wanaofanya kazi Jeshi la Polisi iliwaondolewe," alisema Rais Magufuli.

Mbali na agizo hilo, Rais Magufuli alimtaka Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Mangu kufuatilia mtu aliyelipwa kati ya Sh.bilioni 40 hadi Sh.bilioni 60 kwa ajili ya kutengeneza sare za polisi.

Alisema inashangaza kuona licha ya fedha hizo kutolewa lakini hadi leo hakuna hata sare moja iliyonunuliwa tangu mwaka jana, wakati Jeshi hilo likikosa Sh.bilioni 4 za kukomboa magari yake yanayoshikiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

“Nataka tuhakikishe tunapata hizo fedha zenu ilimkakomboe magari yenu kule TRA. Natarajia siku moja waliohusikana hilo la kununua sare watapelekwa mbele ya haki,” alisema Rais Magufuli akimaanisha kuwa anatarajia watafikishwa mahakamani.

Aidha, wakati Rais Magufuli akitoa agizo hilo, Julai 9 mwaka huu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Rwegasira alimsimamisha kazi Mhasibu Mkuu wa Jeshi hilo ambaye ni raia, Frank Msaki kwa makosa ya kufanya malipo hewa ya posho ya chakula kwa watu wasio kuwa askari.

Mhasibu huyo anatuhumiwa kufanya malipo ya Sh. 305,820,000 kama posho ya chakula kwa watu ambao sio askari kwa kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha 2013/2014 hadi 2015/2016.

Mhasibu Mkuu huyo alisimamishwa kazi tangu Julai9, 2016 ili kupisha uchunguzi juu ya tuhuma zinazo mkabili.

Source: IPPMedia/Nipashe
ZeroDegree.
Mtikisiko Polisi. Mtikisiko Polisi. Reviewed by Zero Degree on 8/21/2016 03:58:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.