Loading...

Ng’ombe, punda watumika kuingiza magendo Jijini Dar.

POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imebaini mbinu mpya inayotumiwa na wahalifu kuingiza bidhaa za magendo kwa kutumia wanyama wakiwemo ng’ombe na punda.


Wahalifu hao wamekuwa wakiingiza bidhaa mbalimbali za magendo kwa njia za panya, wakiwatumia wanyama hao kwa lengo la kukwepa kulipa kodi.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Kamanda wa Kanda hiyo, Naibu Kamishna Hezron Gyimbi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya usalama ya wiki katika jiji hilo.


Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Naibu Kamishna, Hezron Gyimbi.
Kamanda Gyimbi alisema wamebaini wahalifu wamekuwa wakibadili mbinu tofauti tofauti za wizi ikiwemo za kutumia punda na ng’ombe waliofundishwa kwa ajili ya kusafirisha bidhaa za magendo za wakwepa kodi.

“Wanyama hao huswagwa hadi kwenye ufukwe wa bahari na moja kwa moja kuelekea kwenye boti ambayo imeegeshwa katikati ya maji na mizigo kupakiwa kwenye trela ya ng’ombe na ng’ombe hupigwa fimbo ambapo hukimbia hadi alipoelekezwa na wahalifu,” alisema Kamanda Gyimbi.

Alisema Agosti 17, mwaka huu saa 2:00 usiku katika eneo la Mbweni kwenye ufukwe wa Bahari ya Hindi, alikamatwa ng’ombe akiwa amebeba vitu mbalimbali zikiwemo runinga, sukari, sabuni ambavyo vyote vilikuwa havijalipiwa ushuru.

Aliongeza kuwa wameshabaini mbinu hizo na wanaendelea kufanya uchunguzi na kuwasaka wamiliki wa wanyama hao, huku akiwataka raia wema kuendelea kutoa taarifa.

Katika hatua nyingine, Kamanda Gyimbi alisema wamewakamata watu wanne kwa tuhuma za ujambazi wa kutumia silaha katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Morogoro, Lindi na Mtwara.

Alisema watuhumiwa hao walikamatwa na kikosi maalumu cha kupambana na ujambazi wa kutumia silaha cha kanda hiyo, ambapo walikamatwa juzi saa 1:00 asubuhi katika eneo la Chamazi, Wilaya ya Temeke.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Uswege Selemani (23) mkazi wa Mgandaga Kilwa Chamazi, Hassan Abdallah (73) mkazi wa Hoteli Tatu mkoani Lindi, Said Kiwambu (39) mkazi wa Mnyagala na Hamad Badrilu (28) mkazi wa Chamazi.

Alisema watuhumiwa hao walikamatwa muda mfupi baada ya kuingia nyumbani kwa Uwesu Selemani kwa ajili ya kukutana kufanya mipango ya uhalifu wa kutumia silaha.

“Baada ya nyumba hiyo kupekuliwa na askari, walifanikiwa kupata silaha aina ya Mark IV yenye namba LA-227725 ikiwa imeviringishwa kwenye shuka,” alisema. Alisema baada ya kuhojiwa watuhumiwa hao walikiri kufanya matukio mbalimbali ya ujambazi wa kutumia silaha katika mikoa mbalimbali.


Credits: Habari Leo
ZeroDegree.
Ng’ombe, punda watumika kuingiza magendo Jijini Dar. Ng’ombe, punda watumika kuingiza magendo Jijini Dar. Reviewed by Zero Degree on 8/20/2016 10:27:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.