Loading...

Polisi yaita ‘makomandoo’ kufyeka majambazi Dar.

SIKU moja baada ya mapambano baina ya polisi na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi kutokea eneo la Vikindu, Mkuranga mkoani Pwani, jeshi la polisi limechukua hatua kali ya kuwapa kazi maalum askari wake shupavu zaidi ya 80 kwa ajili ya kuendesha operesheni ya kukabiliana na wahalifu hao.

Aidha, kwa kuanzia, kikosi hicho cha askari walioiva kwa mafunzo na kusheheni silaha mbalimbali kitakwenda katika maeneo yote yanayodhaniwa kuwa maficho ya majambazi na kuwashughulikia ipasavyo ili hatimaye wafikishwe kwenye mkono wa sheria na kuchukuliwa hatua stahiki. 

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana ikiwa ni siku moja baada ya kujiri kwa tukio la mapigano makali baina ya polisi na watuhumiwa wa ujambazi kwenye eneo la Vikindu, Kamanda wa Polisi katika Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro, amesema kikosi hicho cha askari shupavu zaidi ya 80 kitapita kwenye maeneo yote yakiwamo ya mapori na vichaka vyote jijini Dar es Salaam na maeneo jirani ya Mkuranga na kwingineko ili kuwasaka watuhumiwa.

Kamanda Sirro alisema kuwa operesheni hiyo ni mwendelezo wa ile iliyoanza Alhamis baada ya askari wanne wa jeshi hilo kuuwawa eneo la Mbande, katika mkoa wa Kipolisi wa Temeke jijini Dar es Salaam.

“Operesheni hii tuliianza juzi na tumeendelea nayo jana (juzi) na leo (jana)… tunaamini hadi kufikia Jumanne, jeshi la polisi tutakuwa na la kuongelea kuhusu operesheni hizi. Kubwa zaidi ni kuona kuwa silaha zao zinarudi… lakini niseme unapoua unategemea nini?” alisema Kamanda Sirro na kuongeza:

“Baada ya mauaji ya askari wetu, kuna raia wema walitoa taarifa nyingi na tunazifanyia kazi. Na tumewakamata watu kadhaa na hadi sasa wengine kadhaa wameuawa… idadi kwa sasa siwezi kuisema kwa sababu bado tupo kwenye mapambano ya kuwasaka majambazi,” alisema.

Akizungumzia hali halisi ya kwenye maeneo ya mapambano, Kamanda Sirro alisema ni ya kawaida kwao katika kuhakikisha kuwa wananchi wanahakikishiwa ulinzi wao na mali zao.

“Mapambano ya silaha kwetu ni ya kawaida. Ndiyo maana polisi akipigwa risasi kwetu ni kawaida, kwa sababu askari silaha yao ni bunduki na atakayekufa kwa kupigwa na risasi siyo jambo la ajabu kwetu… tutaenda Vikindu, Pwani na Dar es Salaam yenyewe,” alisema.

Aidha, alisema lengo la jeshi lao ni kuhakikisha kwamba Dar es Salaam inakuwa shwari, sawa na maeneo mengine yote nchini.

“Hao walioingia Dar es Salaam na kudhani wanaweza kuitawala watambue kuwa hiyo nafasi haipo. Lazima tufagie ili turudishe heshima ya Dar es Salaam,” alisisitiza.

Juzi, paliibuka mapambano makali baina ya polisi na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi katika eneo la Vikindu, kwenye nyumba moja ya makazi na taarifa zilisambaa kuwa watuhumiwa 14 waliuawa na wengine saba kukamatwa.

Aidha, ilielezwa kuwa katika mapambano hayo, Mkaribu Mwandamizi wa Polisi (ASP), Thomas Njiku (40), ambaye alikuwa mkuu wa vikosi vya kupambana na ujambazi vilivyofika kwenye nyumba iliyodaiwa kuwa ndani yake kuna wahalifu, aliuawa kwa kupigwa risasi maeneo ya kichwani.

Ilidaiwa kuwa Njiku aliuawa muda mfupi baada ya kuwasili na vikosi hivyo kwenye eneo la tukio na wakati akitoa maelekezo ya namna ya kuanza mashambulizi, ndipo alipofyatuliwa risasi na mtuhumiwa mmojawapo anayedaiwa kuwa wakati huo alikuwa amesimama kwenye moja ya dirisha la nyumba hiyo. Hata hivyo, Kamanda Sirro hakueleza kiundani juu ya taarifa rasmi za tukio hilo.

Taarifa za kifo cha askari huyo (Njiku) zimeongeza idadi ya polisi waliouawa hivi karibuni kutokana na ‘unyama’ wa majambazi kufikia watano juzi baada ya wengine wanne waliouawa pia na majambazi katika eneo la Mbande, Temeke.

Taarifa zaidi kuhusiana na tukio la Vikindu zilidai kuwa katika tukio hilo, watuhumiwa ni pamoja na askari mstaafu wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), ambaye anadaiwa alikuwa ni mtaalam wa utunguaji (Sniper).

SEPTEMBA MOSI

Kamanda Sirro alisema kupitia taarifa zake za kiintelijensia, kuna taarifa kuwa baadhi ya watu wanataka kuandamana na hivyo wao wamejipanga kuhakikisha kwamba uvunjifu wa amani haupati nafasi kwa namna yoyote ile.

“Wale wazalendo wasiopenda kupambana na jeshi hili, wasiingie barabarani lakini wale wanaotaka kuonekana nawakaribisha waingie… hata wakiingia amani itakuwapo na sheria itachukua mkondo wake,” alisema.

Source: Nipashe
ZeroDegree.
Polisi yaita ‘makomandoo’ kufyeka majambazi Dar. Polisi yaita ‘makomandoo’ kufyeka majambazi Dar. Reviewed by Zero Degree on 8/28/2016 09:52:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.