Loading...

Wanafunzi 12 wabeba ujauzito ndani ya mwezi mmoja.

JINAMIZI la wanafunzi wa Shule za Sekondari Wilaya ya Rombo, kubeba ujauzito linaendelea kuitesa wilaya hiyo, baada ya wasichana wengine 12 kugunduliwa katika kipindi kisichozidi siku 60.

Idadi hiyo sasa, inafanya wanafunzi waliopata mimba wilayani humo kufikia 36 tangu mwezi Januari, mwaka huu, Serikali ya mkoa wa Kilimanjaro, ilipoanzisha zoezi la upimaji wa mimba katika shule za sekondari na msingi.


Mkuu wa wilaya hiyo, Agess Hokororo, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa wanafunzi hao waligunduliwa, baada ya kufunguliwa shule na yeye kuagiza wanafunzi wote wa kike kupimwa ujauzito ili kubaini kiini cha tatizo kama hupata wakiwa likizo au shuleni.

“Katika uchunguzi wetu uliofanyika kati ya Agosti 15 hadi 19, mwaka huu, baada ya wanafunzi kutoka likizo, tumebaini kwamba kasi ya wanafunzi kupewa mimba inapanda.

Sababu za kupata ujauzito ni wanafunzi hao kujihusisha na vitendo vya ngono mapema na waendesha bodaboda na madereva wa magari madogo aina ya Noah,” alisema Hokororo.

Jumla ya wanafunzi 8,895 wa shule 39 za serikali ndio waliopimwa na kati yao wanafunzi 36 kugundulika kuwa ni wajawazito.

Hokororo alisema kabla ya wanafunzi hao 12 kuongeza idadi hiyo na kufikia 36, wanafunzi hao wakati wakijiandaa kwenda likizo ya muhula wa kwanza wa mwezi wa Juni mwaka huu, walipimwa na 24 waligundulika kuwa wajawazito na kushauriwa kubaki nyumbani.

Hivi karibuni, Ofisa elimu Mkoa wa Kilimanjaro (REO), Euphrasia Buchuma, alinukuliwa akisema hadi kufikia mwezi Agosti, kulikuwa na wanafunzi 80 wa shule za msingi na sekondari mkoani hapa waliosimamishwa kuendelea na masomo yao, baada ya kupata ujauzito kati ya Januari na Julai, mwaka huu.

Wilaya ya Rombo ndiyo kinara wa wanafunzi kupata ujauzito ikiwa na wanafunzi 36, ikifuatiwa na Siha 12, Hai wanafunzi 11, Moshi wanane, Mwanga sita Manispaa ya Moshi watatu, huku Wilaya ya Same, ikiwa haina mwanafunzi aliyebainika kuwa mjamzito.

Credits: Nipashe
ZeroDegree.
Wanafunzi 12 wabeba ujauzito ndani ya mwezi mmoja. Wanafunzi 12 wabeba ujauzito ndani ya mwezi mmoja. Reviewed by Zero Degree on 8/30/2016 02:32:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.