Loading...

Wanaotoza kodi ya pango zaidi ya Shilingi laki 5 kwa mwaka kulipa kodi.

Watu wenye majengo yanayopangishwa na kupata zaidi ya Sh500,000 kwa mwaka wametakiwa kujipanga kulipa kodi ili kuepuka kufikishwa mahakamani kwa kukwepa kodi.

Ofisa wa Elimu kwa Walipa kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Nyanda za Juu Kusini, Kissa Kyejo alisema hayo jana kwa wananchi waliotembelea banda lao kwenye Maonyesho ya Wakulima (Nanenane) yanayofanyika Uwanja wa John Mwakangale jijini Mbeya.

Alisema utaratibu kwa wamiliki wa majengo ya kupangisha mwaka huu unaelekeza wazi kwamba wanaopata zaidi ya Sh500,000 kwa mwaka kutokana na kupangisha lazima walipe asilimia 10 ya mapato hayo.

Kwa utaratibu huo, watu wanaotakiwa kulipa kodi ni wale wanaopangisha kuanzia Sh50,000 kwenda juu kila mwezi kwenye vyumba ama majengo yao.

Kwa mujibu wa waraka wa mhutasari wa mapato ya mwaka huu, Mtanzania anayemiliki nyumba ya kupanga atatakiwa kulipa asilimia 10 ya mapato hayo, lakini kwa wageni wanaomiliki nyumba za biashara watakiwa kulipia asilimia 15 ya mapato.

Alisema wanaendelea kuzitambua nyumba zinazopangishwa ili wamiliki waanze kulipa kodi kutoka kwenye mapato ya pango.

Mkazi wa Majengo, Mzee Juma Choga alisema kitendo cha kuwabana wapangishaji walipe kodi kinaweza kupandisha gharama za maisha kwani wenye nyumba wataongeza kodi kwa wateja wao.

Choga alisema nyumba nyingi za kupanga kodi yake ni kati ya Sh100,000 hadi 400,000 kwa mwezi jijini hapa jambo linaloonekana wazi kwamba wamiliki wake watalazimika kulipa kodi kwani vipato vyao kwa mwaka ni zaidi ya Sh500,000.



Credits: Mwananchi
ZeroDegree.
Wanaotoza kodi ya pango zaidi ya Shilingi laki 5 kwa mwaka kulipa kodi. Wanaotoza kodi ya pango zaidi ya Shilingi laki 5 kwa mwaka kulipa kodi. Reviewed by Zero Degree on 8/08/2016 07:21:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.