Loading...

Watanzania milioni 23 kupewa vitambulisho vya uraia ifikapo Desemba 31.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa mamlaka hiyo, Rose Mdami.
MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), imeeleza kuwa ifikapo Desemba 31, mwaka huu, Watanzania milioni 23 watakuwa na namba za utambulisho wa Vitambulisho vya Uraia.




Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa mamlaka hiyo, Rose Mdami, amesema kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli la kuitaka Nida kuweka saini ya mwombaji na mtoaji wa vitambulisho hivyo.

"Tumeanza kutekeleza agizo la Rais tangu Juni, mwaka huu. Hii inamaanisha kwamba vitambulisho vyote tulivyochapisha kuanzia Juni mpaka leo, vina saini ya muombaji, saini ya mtoaji na tarehe ya kuzaliwa muombaji,” alifafanua Mdami.

Mdami alisistiza kuwa ifikapo Desemba 31, mwaka huu, Nida itakuwa imetoa namba za utambulisho wa vitambulisho hivyo kwa Watanzania milioni 23 kwa kutumia taarifa za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) zilizo katika vitambulisho vya kupigia kura na kuzihamishia katika kanzi data ya Nida.

Alisema ili mwananchi apate kitambulisho cha uraia, atalazimika kufika katika ofisi za Nida akiwa na vielelezo vinavyoonyesha mwaka wake wa kuzaliwa pamoja uthibitisho wa uraia wake kwa kuwa Nec haina viambatanisho hivyo.

Aliongeza kuwa mwananchi mwenye namba ya utambulisho, atapata huduma zote zinazohitaji namba ya kitambulisho cha uraia kutokana na namba hiyo kutobadilika na kuendelea kutumika hata baada ya kitambulisho kuchapishwa.

Alisema mpaka sasa Watanzania milioni 2.7 wamekwisha patiwa vitambulisho hivyo na milioni 6.5 wamesajiliwa kwa ajili ya kupata vitambulisho hivyo.

Aidha, amefafanua kuhusu malalamiko ya baadhi ya watu wanaodai kwamba kumekuwa na mlolongo mrefu wa kupata vitambulisho hivyo.

Alisema Nida haina namna ya kufupisha mlolongo huo kwani kufanya hivyo ni sawa na kuuza uraia wa Tanzania.

Alisisitiza kuwa ni lazima Nida ijiridhishe juu ya uhalali na sifa za muombaji kuwa ni Mtanzania kwa kuambatanisha vielelezo vinavyohitajika.


Credits: IPPMedia
ZeroDegree.
Watanzania milioni 23 kupewa vitambulisho vya uraia ifikapo Desemba 31. Watanzania milioni 23 kupewa vitambulisho vya uraia ifikapo Desemba 31. Reviewed by Zero Degree on 8/16/2016 09:39:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.