Loading...

Lowasa aitikisa CUF.

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Imebainika kwamba mgogoro unaoendelea kufukuta ndani ya CUF unabebwa zaidi na hoja dhidi ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa baada ya aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba kuendelea kutumia jina hilo kama sababu za mvurugano unaokikabili kwa sasa.

Katika mahojiano na kituo cha redio cha Clouds FM, Profesa Lipumba amesema mkutano wa chama hicho uliomridhia Lowassa kuingia Ukawa ulifanyika Zanzibar bila yeye kuambiwa, kitendo kinachoonyesha kuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad alikuwa akimzunguka. 

Mbali na tuhuma hiyo, kiongozi huyo alieleza kuwa hatakuwa tayari kuona CUF ikinunuliwa kwa bei chee na Lowassa au Chadema hata kama atakuwa nje ya chama hicho.

Hata hivyo, madai hayo yamepingwa vikali na Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui aliyedai kuwa Profesa Lipumba ni “kigeugeu” huku Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akisema “hakutegemea maneno hayo yangetoka kwa mtu kama Profesa Lipumba.”

Katika mahojiano hayo, Profesa Lipumba alisema alijua uwepo wa mkutano huo baada ya Mbowe kumuuliza iwapo alikuwa anafahamu juu ya wito wake visiwani Zanzibar baada ya kuitwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar wakati huo, Maalim Seif.

“Hoja ya kwamba Lowassa anaweza kujiunga na Ukawa ilitokea katika kikao hicho wakati huo viongozi wa Chadema walikuwa na msimamo kwamba hakuna kumruhusu mtu mwingine kutoka nje kuja kugombea na tungechaguana sisi wenyewe,” alisema Profesa Lipumba na kuongeza: “Pamoja na kwamba Lowassa alianza kuwa na mazungumzo na Chadema, lakini suala la kuingia Ukawa endapo ataachwa na CCM lilianzia CUF.”

Profesa Lipumba alisema baada ya kukutana na Lowassa, waziri mkuu huyo wa zamani alimwambia kuwa tayari ameshafanya mazungumzo na viongozi wengine wa Ukawa... “Aliniuliza kama nilikuwa nikifahamu jambo hilo.”

Baada ya kumjibu kwamba hajui chochote katika mazungumzo ya awali, Profesa Lipumba alimtaka Lowassa kukutana na viongozi wote wa vyama vinavyounda Ukawa ili kujadili suala lake.

“Nilikuwa nakubali Lowassa aingie ndani ya Ukawa lakini sio kuwa mgombea wa urais. Kiongozi wa Taifa anahitaji kuwa na msimamo, hawezi kuwa anaongozwa na upepo tu kwamba ukitaka urais unaangalia chama gani kinaweza kukusimamisha kama mgombea,” alisema.

Sababu hizo za Profesa Lipumba dhidi ya Lowassa ni mwendelezo wa kutetea uamuzi wake wa kujiuzulu uenyekiti mapema Agosti mwaka jana licha ya kushiriki kumpokea kiongozi huyo katika umoja huo unaoundwa na vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.

Lowassa, aliyegombea urais kupitia Ukawa katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana, alihamia Chadema mwishoni mwa Julai baada ya jina lake kukatwa na CCM katika mchakato uliofanikisha kupatikana kwa Rais John Magufuli kugombea kupitia chama hicho tawala.

Mwanasiasa huyo, ambaye amesimamishwa uanachama wa CUF alisema hana mpango wa kuhamia chama chochote wala kuanzisha kipya na endapo Lowassa atakuwa mgombea wa urais katika umoja watakaokuwa nao mwaka 2020 hatakuwa tayari kumuunga mkono.

Licha ya chama hicho kupata wabunge wengi katika uchaguzi huo, Profesa Lipumba alisema Lowassa hakuwasaidia kuongeza idadi ya wawakilishi hao kwa kuwa yalikuwa ni matokeo ya ujenzi wa chama walioufanya katika maeneo ya Kusini.

“Huwezi kupata ubunge ndani ya mwezi mmoja kama hakuna mtandao na chama hakiaminiki,” alisema Profesa Lipumba baada ya kuulizwa iwapo Lowassa alichangia kuongeza wabunge.

“Kama tungeweka wana-Ukawa wenyewe pekee na tukawa na umoja thabiti huenda tungefanya vizuri zaidi kuliko hata tulivyofanya, lakini jambo la msingi katika kipindi hiki ni kila mtu kuweza kujenga chama chake”.

Alisema Lowassa alikuwa miongoni mwa wajumbe wa Bunge la Katiba ambao hawakuunga mkono rasimu ya Jaji Joseph Warioba hivyo alikuwa kinyume kabisa na misingi iliyounda Ukawa.

Bado ni mwenyekiti

Profesa Lipumba alidai kuwa yeye bado ni mwenyekiti wa chama hicho kwa kuwa mamlaka iliyomchagua haijatengua nafasi yake kwa kuthibitisha barua yake ya kujiuzulu.

Baada ya kujiuzulu mwaka jana, alisema watu wengi walimfuata wakiwamo wazee na vijana kumuomba arejee katika nafasi yake na walikwenda kwa Maalim Seif ambaye aliwauliza, je? Profesa atakubali.

“Nilipoona kuwa tuna matatizo mengi na wanachama kunitaka nirejee kwenye nafasi yangu ndipo nilipoandika barua ya kutengua barua ya awali ya kujiuzulu na kukijulisha chama kuwa naturudi katika ofisi yangu Juni 10 kwa ajili ya kuendelea na majukumu yangu ikiwa ni pamoja na kufanya uchambuzi wa bajeti ya Serikali na kutoa msimamo wa chama katika bajeti hiyo,” aliongeza: “Barua unaweza ukaitengua kabla ya maamuzi lakini baada ya maamuzi huwezi kutengua”.

Pamoja na wakosoaji kumwelezea kiongozi huyo kuwa anang’ang’ania madaraka, Profesa Lipumba alipinga tuhuma hizo akieleza kuwa anaangalia mustakabali wa mtu ambaye ataweza kuifanya CUF kuwa chama cha kitaifa.

Hata hivyo katika mkutano mkuu wa CUF uliofanyika katika Ukumbi wa Ubungo Plaza mwezi uliopita, wanachama waliliridhia kujiuzulu kwa Lipumba, lakini walipokuwa wakijiandaa kupiga kura kujaza nafasi hiyo zilizuka vurugu zinazodaiwa kusababishwa na vijana wanaomuunga msomi huyo wa uchumi.

CUF wamjibu

Akizungumza kwa simu jana, Mazrui alimtaka Profesa Lipumba asitafute mchawi kwa yanayoendelea kwa kuwa yeye ndiye wa kwanza kumtambulisha Lowassa na Ukawa CUF.

Alisema Profesa Lipumba alikuwa akiwaambia viongozi wa CUF kwamba utafiti uliokuwa umefanywa wakati huo, Lowassa alikuwa na uwezo wa kupata kura nyingi hivyo isingekuwa vibaya kama angekaribishwa ndani ya Ukawa.

“Makubaliano yalikuwa Dk (Willibrod Slaa) awe mgombea wa Ukawa lakini yeye (Profesa Lipumba) alianza kuvunja makubaliano kwa kutangaza kugombea urais akiwa Tabora.

“Baada ya kupata fedha anakokujua alifanya sherehe Ubungo Plaza ya kuchukua fomu ya kugombea urais na baadaye ndiye aliyemleta Lowassa na kumsafisha kuwa ufisadi ni mfumo siyo mtu, sasa hapo nani kigeugeu?” alihoji.

Source: Mwananchi
ZeroDegree.
Lowasa aitikisa CUF. Lowasa aitikisa CUF. Reviewed by Zero Degree on 9/09/2016 08:20:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.