Loading...

Simanzi tetemeko la ardhi.

Wananchi waliojeruhiwa baada ya kutokea tetemeko.
Simanzi na taharuki vimetawala katika miji ya Mwanza na Bukoba baada ya tetemeko la ardhi lililotokea jana kuharibu mali na kusababisha vifo vya watu huku wengine wakijeruhiwa.

Taarifa za awali kutoka Bukoba zilisema watu 11 wamefariki dunia na wengine zaidi ya 200 kujeruhiwa.

Tukio hilo ambalo lilitokea jana saa 9:20 alasiri, lilisababisha watu kadhaa, hususan waliokuwa katika nyumba za ghorofa kushikwa na taharuki baada ya tetemeko hilo lililodumu kwa takribani dakika tatu, kutikisa nyumba hizo na kuwafanya kukimbia ovyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustino Ollomi, alisema maafa hayo yalitokea katika Masnispaa ya Bukoba na Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba.

Baadhi ya wakazi wa jiji la Mwanza, wakizungumza baada ya kutokea tetemeko hilo, walisema hali ilikuwa mbaya kwao kutokana na kutofahamu kilichokuwa kikiendelea.

“Hili tetemeko limetuacha na mshangao kwani tukiwa ndani ya nyumba zetu, ghafla tukashangaa kuona tunatikiswa huku na huko na watu wengine wakishuka kwa kasi toka maghorofani,” alisema Majura John.

John ambaye alikuwa akiangalia mpira katika jengo moja lililoko mtaa wa Posta jijini Mwanza, alisema awali aliamini gari kubwa lililobeba mzigo likitetemesha jengo walililokuwa wakiangalia mpira, lakini baada ya kuchungulia nje alishangaa kuona watu wanakimbia ovyo.

Naye Estaria Phabian alisema hajawahi kushuhudia tetemeko la ardhi likipita zaidi ya kushuhudia kwenye luninga katika nchi zingine na kusababisha madhara.

Hata hivyo, watu mbalimbali waliokuwamo katika hoteli maarufu ya Gold Crest jijini hapa hasa ghorofa ya tisa, walionekana kushikwa na butwaa na kushindwa kuteremka chini zaidi ya kubaki juu na kuangalia watu waliokuwa wakikimbia bila mpangilio.

Mwandishi wa habari mkoani Kagera, Lilian Lugakingira(wa gazeti la Nipashe), alisema nyumba yake ilikumbwa na zahama hiyo, kwa kuwa ilipata ufa mkubwa.

“Nyumba yangu iliyopo mtaa wa Kyakailabwa manispaa ya Bukoba, imeathirika kwa kupata mipasuko katika kuta mbili…watoto waliokuwamo ndani walipatwa na taharuki na kukimbia ovyo,” alisema Lugakingira.

Lugakingira alisema alipata taarifa hizo akiwa safari kutokea jijini Dar es Salaam kwenda Bukoba. Alisema wakati tukio hilo linatojkea nyumbani hapo walikuwapo watoto wake wawili, Ruth na Gloria Peter na dada wa kazi, Anitha George, ambao hata hivyo hawajaathirika kutokana na tukio hilo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, alikiri kutokea kwa tetemeko hilo, lakini mpaka gazeti hili linaenda mitamboni alisema alikuwa hatajapata taarifa za madhara yoyote.

Source: Nipashe
ZeroDegree.
Simanzi tetemeko la ardhi. Simanzi tetemeko la ardhi. Reviewed by Zero Degree on 9/11/2016 08:56:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.