Loading...

Sitavumilia chokochoko – Magufuli.

RAIS John Magufuli amesema hatavumilia aina yoyote ya vitendo vya uvunjifu wa amani kwa sababu amekula kiapo cha kulinda amani na utulivu kwa maslahi ya wananchi wa Tanzania, hivyo katika kipindi cha uongozi wake wa miaka mitano atahakikisha kipaumbele cha kulinda amani na kuimarisha Muungano ndiyo dira na mwongozo.

Rais Magufuli alisema hayo jana kwenye Viwanja vya Demokrasia Kibanda Maiti mjini Unguja, Zanzibar wakati akizungumza na wananchi wa mikoa mitatu ya Unguja akitoa shukrani baada ya kuchaguliwa kwa kura nyingi kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Awamu ya Tano, Oktoba mwaka jana.

Alisema hatovumilia aina yoyote ya vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani kwa sababu amekula kiapo kulinda amani na utulivu kwa maslahi ya wananchi wa Tanzania.

“Narudia tena sitawavumilia wanaoleta chokochoko na kuhatarisha amani ya nchi kwa sababu nimekula kiapo kulinda amani ya Watanzania wote,” alisema Dk Magufuli na kuongeza kuwa hana mjadala na suala la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa na viongozi wakuu walioleta ukombozi wa wananchi hivyo ataulinda kwa nguvu zote.

“Hivyo ndiyo vipaumbele vyangu kulinda amani kwa nguvu zote pamoja na kulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao ndiyo kielelezo cha taifa letu,” alisema huku akishangiliwa na mamia ya wananchi waliofurika kwenye uwanja huo.

Aidha, alimpongeza Dk Shein kwa uvumilivu wake ikiwemo kuwajumuisha wapinzani katika serikali, lakini alionesha kukerwa na kitendo cha Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad kukataa mkono aliopewa na Rais Shein katika msiba wa Rais wa Awamu ya Pili Zanzibar, Alhaji Aboud Jumbe mwezi uliopita.

“Wewe Rais Shein ni mvumilivu sana bwana.....mtu anakataa kupokea mkono wako, lakini baadaye unakwenda kutengeneza maslahi yake wakati anapotaka kwenda matibabuni nje......hii kama mimi namkatalia bwana,” alisema Rais Magufuli anayefahamika kwa misimamo yake iliyo wazi na isiyoyumba.

Alimtaka Rais Shein kufanya kazi zake vizuri na yeye akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atahakikisha Zanzibar inapiga hatua kubwa ya maendeleo. Kwa mfano, alisema tayari upo mradi mkubwa wa maji katika mji wa Unguja ambao ni mkopo kutoka Serikali ya India utekelezaji wake utasaidia kulimaliza tatizo la maji.

“Mimi nikiwa Rais wa Muungano nitafanya kazi bega kwa bega na Rais Shein......huyu namfahamu, kwanza alikuwa bosi wangu akiwa Makamu wa Rais uwezo wake ni mkubwa,” alieleza Rais Magufuli ambaye amekuwa Zanzibar kwa ziara iliyoanza juzi kisiwani Pemba.

Mapema jana, Rais Magufuli alipata nafasi ya kuzuru kaburi la mwasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar, hayati Abeid Amaan Karume, Kisiwandui mjini Unguja pamoja na kuweka shada la maua na kusomwa kisomo cha dua.

Aidha, alifika katika makazi ya Rais wa Awamu ya Pili Zanzibar hayati Aboud Jumbe Mwinyi aliyefariki mwezi uliopita kwa kuzuru kaburi lake na kusalimiana na wanafamilia wa marehemu na kuandika katika kitabu cha wageni maalumu.

Rais Magufuli amemaliza ziara ya siku mbili ya kisiwa cha Unguja na Pemba ambavyo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano katika ziara ambayo ilikuwa na lengo la kutoa shukrani kwa wapiga kura ambao walimpa ushindi mkubwa katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka jana. Kwa upande wake, Dk Shein amewataka wapinzani wasahau kushika dola na kuongoza nchi kwani Chama Cha Mapinduzi (CCM) kipo imara.

Muda mfupi kabla ya kumkaribisha Rais Magufuli kuhutubia, Dk Shein alisema, “Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushika dola na wapinzani wasahau kushika madaraka......tutashinda kwa njia ya demokrasia ya kufanya uchaguzi.”

Aidha, aliwataka wapinzani kusahau Serikali ya Mpito kama inavyodaiwa na baadhi ya viongozi huku akisisitiza hakuna sababu ya kuwa na aina ya serikali hiyo kwa sababu uchaguzi umefanyika kwa njia ya huru na haki.

Dk Shein alisema kazi kubwa inayofanywa kwa sasa ni kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015, huku Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwa katika hatua ya mwisho ya kuanza kazi za kuchimba mafuta na gesi.

Alisema muswada wa mafuta na gesi tayari umewasilishwa katika Baraza la Wawakilishi na kusomwa kwa mara ya kwanza ambapo katika kikao kijacho cha Baraza la Wawakilishi kitakachofanyika Septemba 26 utasomwa kwa mara ya pili na kusubiri saini yake.

“Namshukuru sana Rais Kikwete kwa kusaidia na kufanikisha taratibu zote ambazo sasa zimetoa nafasi kwa Zanzibar kutayarisha muswada wa mafuta na gesi ambao tayari umesomwa katika Baraza la Wawakilishi,” alisema na kuwatoa wasiwasi wananchi wa Zanzibar akisema nchi imeanza kupata mafanikio makubwa ikiwemo makusanyo ya kodi.

Source: Habari Leo
Zerodegree.
Sitavumilia chokochoko – Magufuli. Sitavumilia chokochoko – Magufuli. Reviewed by Zero Degree on 9/04/2016 08:45:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.