Loading...

Yanga yafuata pointi 6 Shinyanga kwa ndege.

YANGA imejipanga vya kutosha kuhakikisha inaibuka na pointi zote sita Kanda ya Ziwa, baada ya kufanya maandalizi yao ya mwisho katika Uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini jijini Dar es Salaam, kabla ya leo kukwea pipa kuelekea Shinyanga.

Yanga inatarajiwa kusafiri na ndege ili kuhakikisha haiwachoshi wachezaji wake kutokana na kudhamiria kufanya kweli na kuzoa pointi zote sita katika michezo yake hiyo miwili ya mkoani humo.

Katika mazoezi yao ya mwisho yaliyofanyika jana jioni Kocha wa Hans van der Pluijm, alionekana kuwapa mbinu wachezaji wake namna ya kufanya mashambulizi kutumia mipira mirefu na kushtukiza langoni mwa timu pinzani.

Kwa kutambua kuwa wakicheza ugenini huwa wanakamiwa benchi la ufundi la timu hiyo likiongozwa na Pluijm, Juma Mwambusi na Juma Pondamali, muda wote katika mazoezi ya jana jioni lilionekana kuzifanyia kazi mbinu mbalimbali chafu wanazofanyiwa wapinzani wao wakiwa katika viwanja vya ugenini.

Kocha Mkuu wa Yanga, Pluijm ameahidi kuendeleza ubabe na kuisambaratisha Mwadui kwenye ardhi yake ya nyumbani.

Yanga wanashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom msimu huu wakiwa na pointi saba baada ya kucheza michezo mitatu wakiwa nyuma ya Simba na Azam kwa tofauti ya pointi tatu, lakini timu hizo mbili zina mchezo mmoja zaidi.

Katika hatua nyingine, Yanga imetoa pole kwa wahanga wa tetemeko la ardhi lililosababisha athari kubwa mkoani Kagera.

Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mkuu Yanga, Baraka Deusdedith, alisema timu hiyo ina mpango wa kuchangia waathirika wa tetemeko hilo la ardhi.

“Kwanza tunawapa pole watu wote waliopoteza ndugu zao katika tetemeko hili la ardhi, sisi kama Yanga iwapo mambo yatakwenda vizuri tutachangia na sisi kiasi chochote cha fedha kuwafariji waathirika wa janga hili,” alisema Baraka.

Credits: Bingwa
ZeroDegree.
Yanga yafuata pointi 6 Shinyanga kwa ndege. Yanga yafuata pointi 6 Shinyanga kwa ndege. Reviewed by Zero Degree on 9/15/2016 11:15:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.