Loading...

VIDEO: CHADEMA wasitisha tena maandamano ya UKUTA.

Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe.
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimekubali yaishe baada ya kusitisha kwa mara ya pili, maandamano ya Ukuta ambayo yalitakiwa kufanyika leo nchi nzima kwa kile walichodai kuwa kila wanapopanga tarehe, upande wa serikali unaandaa mikakati kwa ajili ya kuvuruga siku hiyo.

Hata hivyo, chama hicho kimesema kuwa operesheni hiyo imesogezwa mbele hadi muda maalumu utakaopangwa na kwamba wamebadilisha mbinu, ambapo sasa mkakati utakuwa si kufanya Ukuta kupitia mikutano ya hadhara pekee, bali pia kupitia vikao vya chama katika majimbo, wilaya na mikoa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe alisema intelijensia ya chama hicho, imetambua mbinu zinazoandaliwa na taasisi za kiusalama za serikali za kudhuru watu ili baadaye waseme kuwa Ukuta umesababisha vifo.

Mbowe alisema wanabadilisha mbinu kwa kuangalia mazingira, usalama wa wananchi, viongozi wa chama na wanachama wao; na kusisitiza kuwa Ukuta utakaokuwepo si wa siku moja, isipokuwa ratiba rasmi ya vikao itatangazwa.

‘’Si sifa kupeleka watu kuumizwa, ila ni sifa kuwapeleka wananchi kwenye malengo mapana yanayojenga demokrasia na uchumi wa nchi kwa ujumla utakaosaidia maisha ya wananchi kuwa bora zaidi. Kwa kupitia intelijensia yetu, tunasema wenye makusudio batili na chama chetu hawatatupata,’’ alisema Mbowe.

Alifafanua kuwa walipotangaza kuwa maandamano ya Ukuta, yatafanyika Septemba mosi mwaka huu, viongozi wa dini waliwasihi kutoendelea na mpango huo na kuwaomba wawape wiki mbili hadi tatu, wakiamini watatafuta namna ya kumaliza mikinzano ya kikatiba ya kutofanyika mikutano ya kisiasa hadi 2010.

Kwa mujibu wa Mbowe, kwa kutii mamlaka ya viongozi wa dini katika kutetea na kulinda amani ya nchi, walitangaza kuwa operesheni hiyo haitakuwepo na badala yake waliisogeza mbele hadi Oktoba mosi (leo).

Pia alisema kuwa hadi juzi, Kamati Maalumu ya Kamati Kuu ya chama hicho walikutana kujua kama viongozi wa dini walipeleka taarifa yoyote kwa kile walichoahidi, lakini hawakupokea taarifa yoyote kama viongozi hao walionana na Rais John Magufuli au kiongozi yeyote wa Serikali au kama wana ushauri wowote wa kuwapa.

Aliongeza kuwa wao kama chama cha siasa, wanaheshimu mamlaka ya kidini na wataendelea kuwaheshimu viongozi hao, lakini wataendelea kupigania haki zao kama sheria za vyama vya siasa zinavyowaruhusu.

Alieleza kuwa mapambano ya kisiasa, si tukio la siku moja, bali ni endelevu na kwamba baada ya tathmini wameona kuwa kuna umuhimu wa kutoendelea na mikutano hiyo iliyokusudiwa kufanyika.

Alisema kuwa wameona majeshi yamekuwa yakiandaliwa kupanda miti kwa lengo la kukabiliana na wafuasi na wananchi wao badala ya kuwalinda; huku akisema kwamba majeshi hayo yalitakiwa kwenda Kagera kwa ajili ya kuwasaidia wananchi waliokumbwa na tetemeko la ardhi.

Mbowe alisema mbinu za watawala, kupambana na vyama vya upinzani nchini zinafanywa na mawakala wanaokuja kwa sampuli mbalimbali, ikiwemo aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba.



ZeroDegree.
VIDEO: CHADEMA wasitisha tena maandamano ya UKUTA. VIDEO: CHADEMA wasitisha tena maandamano ya UKUTA. Reviewed by Zero Degree on 10/01/2016 08:45:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.