Loading...

Daftari la wapiga kura kuanza kufanyiwa maboresho mwakani.


Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inatarajia kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura ifikapo mwaka wa fedha wa 2017/2018 kwa mara ya kwanza baada ya uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2015.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC Bw. Kailima Ramadhani wakati akitoa elimu ya mpiga kura kupitia kipindi cha Alasiri Yetu kinachorushwa na televisheni ya Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC).

Alisema kuwa baada ya uboreshaji huo wa mwaka 2017/2018, Tume hiyo inategemea kuboresha kwa mara ya pili daftari hilo ifikapo mwaka wa fedha 2019/2020.

Bw. Kailima alifafanua kuwa uboreshaji huo unafanyika kwa mujibu wa kifungu namba 5 cha Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kinachoielekeza NEC kuboresha daftari hilo mara mbili.

“Kwa mujibu wa kifungu namba 5 cha Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kinasema Tume ya Taifa ya Uchaguzi itapaswa kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura mara mbili, baada ya uchaguzi mara moja na kabla ya uchaguzi ujao mara moja” alisema Bw. Kailima na kuongeza.

“Kwa hiyo tumemaliza uchaguzi mwaka jana na kabla ya uchaguzi wa mwaka 2020, Mungu akituweka hai tunategemea mwaka 2017/2018 tuboreshe daftari na mwaka 2019/2020 tufanye hivyo”

Mbali na kuzungumzia uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, Bw. Kailima aleleza jinsi tume hiyo inavyotekeleza mikakati ya kutoa elimu ya mpiga kura na kwamba NEC itajipanga ili kwenda kutoa elimu hiyo visiwani Zanzibar.

Alisema NEC inapanga kwenda kutoa elimu hiyo kwenye Chuo Kikuu Zanzibar (State University) mjini Unguja na baadaye kwenda kisiwani Pemba na pia inategemea kushiriki Jitimai ili kutoa elimu ya mpiga kura kwa washiriki wa mjumuiko huo.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa lengo la kuandikisha kila raia mwenye sifa za kupiga kura na kutunza taarifa zake katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Inaelezwa kuwa kuwepo kwa Daftari sahihi la Wapiga Kura linaloaminiwa na wadau ni kigezo muhimu cha kufanikisha chaguzi huru, wazi, zenye kukubalika na za haki zaidi.

ZeroDegree.
Daftari la wapiga kura kuanza kufanyiwa maboresho mwakani. Daftari la wapiga kura kuanza kufanyiwa maboresho mwakani. Reviewed by Zero Degree on 10/09/2016 02:47:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.