Loading...

Vita ya meno ya tembo ni tishio.

NI wazi kwamba vita dhidi ya biashara ya meno ya tembo ni tishio kutokana na uchunguzi uliofanyka, imebainika kuwa ni biashara inayohusisha mataifa makubwa, wafanyabiashara maarufu duniani na wanasiasa kutoka pande zote tawala na upinzani.

Uchunguzi huo uliofanyika kwa wiki kadhaa sasa kwa kulihusisha Pori la Akiba la Selous pamoja na mambo mengine umebaini hali ya ujangili kuendelea kuwa tishio pamoja na jitihada mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na serikali ili kukomesha hali hiyo.

Imeelezwa kuwa pori hilo lililopo kusini mwa Tanzania limepoteza asilimia 90 ya tembo waliopo katika hifadhi hiyo kutokana na ujangili uliokithiri.

Katika kuthibitisha hilo ripoti ya Mfuko wa Hifadhi ya Wanyamapori na Mazingira Duniani (WWF) ya hivi karibuni, imesema kufikia mwaka 2022 kama hakutakuwa na hatua zozote kali zitakazochukuliwa kuwalinda tembo kutokana na ujangili katika Pori la Selous basi watatoweka kabisa.

Ripoti hiyo imeendelea kusema kuwa kwa miaka ya nyuma Pori la Selous lilikuwa mojawapo ya mbuga kubwa kabisa katika Bara la Afrika lenye tembo wengi ambapo kulikuwa na tembo zaidi ya 110,000 lakini kutokana na ujangili uliokithiri katika miaka 40 iliyopita tembo hao wamepungua na kubaki 13,000.

Hatua hiyo inadaiwa kuwa inachangiwa na mahitaji makubwa ya pembe za ndovu katika nchi kubwa duniani hatua inayoelezwa kuwa kichocheo kikubwa cha ujangili na mauaji ya idadi kubwa ya tembo hao.

Aidha ripoti hiyo inaonesha athari kubwa kiuchumi itakayotokea kutokana na kwamba Tanzania kupitia Pori la Selous inaingiza dola milioni 6 kwa mwaka ikilinganishwa na sekta ya viwanda inayochangia dola milioni 5 katika Pato la Taifa.

Kupungua kwa tembo Pori la Akiba la Selous linafahamika kwa kuwa na tembo wengi, kwa bahati mbaya kutokana na mfululizo wa hali ya ujangili wa biashara ya meno ya tembo hesabu ya tembo ilipungua kutoka 110,000, ilivyokuwa mwaka 1976 na kufikia tembo 13,000 sasa.

Si mara nyingi tembo kuonekana wakiwa katika makundi makubwa bali huonekana wakitembea kwa vikundi vidogo vinavyoongozwa na kiongozi. Madume ya tembo hupendelea kukaa kwenye vichaka mara kwa mara lakini wakati fulani hujitokeza kujiunga na makundi ya tembo wa kike.

Inadaiwa kuwa kukithiri kwa ujangili umesababisha kuwepo kwa tembo wachache wenye meno makubwa, huku pia tembo wa umri wa miaka 30 wakiwa wachache. Tembo kiongozi anapochezesha masikio au kuinua mkonga na kusonga mbele ni dalili ya kuwepo kwa adui. Kiutaalamu inaelezwa kuwa ni hatari sana kukutana na tembo anayetishia adui, askari wa wanyamapori wenye uzoefu ndio wanaoweza kutambua kama tembo anatishia tu au amekasirika.

Juhudi za serikali Pamoja na hayo Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeweka mikakati madhubuti ikiwemo kuunda kitengo chake cha intelijensia na kuunda kanda nane za doria za ushirikiano katika mifumo ya ikolojia ya mbuga ya Selous ambayo imeanza kuwa na mafanikio.

Mwaka 2014 Shirika la Kimataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) liliweka Pori la Selous katika urithi wa asili ulio hatarini duniani.

Meneja wa Pori la Akiba la Selous, Hanock Msocha akitoa maoni yake kufuatia maswali yaliyojitokeza wakati wa uchunguzi wa gazeti hili kuhusu hali ya ujangili katika mbuga hiyo, pamoja na kukiri kuwa ni tishio anasisitiza kuwa kiama cha watu wanaojishughulisha na biashara hiyo kimefika kutokana na nia ya dhati ya Rais John Magufuli kukabiliana na masuala mbalimbali ya kitaifa kwa nguvu zake zote.

Msocha anasema pamoja na kwamba askari wa Wanyamapori wanaendelea na mapambano ya kukabiliana na majangili wanaovamia mara kwa mara katika Pori la Selous na kuua tembo, lakini vita hiyo ni ngumu kwa vile wanaojihusisha ni wafanyabiashara wakubwa na mataifa makubwa duniani, huku wakitumia teknolojia ya kisasa kila mara.

“Ni mapambano magumu, kwanza askari wetu wanapambana na watu na mataifa yenye fedha na teknolojia za hali ya juu. Zipo jitihada zinafanyika za kuwajengea uwezo askari wetu na kuwapatia vifaa mbalimbali lakini bado ni vita hatari na tishio.

“Kwangu mimi naona tatizo kubwa limekuwa ni utashi wa kisiasa. Wanasiasa hawapigani kwa dhati katika vita hii na wapo ambao wamegeuka mawakala na kazi yao ni kuhakikisha kuwa nchi haifanikiwi katika mapambano haya,” alisema Msocha.


Muelekeo wa mapambano.


Akizungumzia namna anavyoona muelekeo wa vita hiyo baada ya kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Tano, Meneja huyo wa Pori la Selous alisema;

“Rais Magufuli ameonesha utashi wa kisiasa, nimeingiwa na matumaini yeye kushinda vita hii.” Alisema ingawa haiwekwi wazi, lakini ni ukweli kwamba Operesheni Tokomeza Ujangili iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Nne ili kukabiliana na ujangili pamoja na kuwa na kasoro za hapa na pale ilikuwa ni sahihi katika kukabili vita hiyo.

“Ni kweli unapohusisha wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) haiwezi kuwa sawa na kuwatumia askari wa Wanyamapori, wao nguvu yao ni kubwa zaidi, na naamini wangekomesha kabisa.

“Kilichotokea ndiyo hicho ninachosema ni ukosefu wa utashi wa kisiasa maana wanasiasa ndio waliotumika kuipiga vita hadi ikasimamishwa kwa kuwalaghai wananchi kudhani kuwa haikuwa operesheni sahihi na badala yake ilitesa na kuwaumiza watu,” alisema.

Alisema askari wa Wanyamapori wanajitahidi pamoja na hatari iliyo mbele yao ya kuuawa ama na tembo wenyewe au majangili akitolea mfano wa askari mmoja (bila kupenda kumtaja jina) aliyesema aliuawa na tembo hao wiki mbili zilizopita akiwa katika eneo la ofisi Matambwe na kusafirishwa mkoani Mbeya kwa maziko.

Operesheni Tokomeza Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Maliasili na Mazingira chini ya aliyekuwa Mbunge wa Kahama, James Lembeli wakati huo akiwa CCM, iliyotolewa kuhusiana na kasoro za utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili ilipandisha hasira za wabunge na hatimaye kulazimisha mawaziri wanne kujiuzulu.

Operesheni hiyo ilianza Oktoba mwaka 2013, na kusitishwa na Bunge Novemba 4, mwaka 2014, kwa maelezo kuwa ilikiuka haki za binadamu.

Mawaziri waliojiuzulu ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dk Shamsio Vuai Nahodha na aliyekuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David.

Hata hivyo licha ya kuwepo kwa madhara yaliyojitokeza katika operesheni tokomeza Ujangili, Rais mstaafu wa Awamu ya Nne Jakaya Kikwete alisema kuwa operesheni hiyo ingeendelea, hatua ambayo Meneja wa Selous alisema ana imani kubwa na Rais Magufuli ataiendeleza na kutokomeza kabisa ujangili.

Kasoro katika operesheni hiyo zilitajwa na Tume ya Uchunguzi iliyoundwa na Kikwete ikiongozwa na Jaji mstaafu Balozi Hamisi Msumi ikiwa na makamishna Jaji mstaafu Stephen Ihema na Jaji mstaafu Vincent Lyimo, huku Wakili wa Serikali, Frederick Manyanda akiwa Katibu wa Tume, kueleza kubaini ukiukaji wa haki za binadamu katika utekelezaji wake.

Tume hiyo ilitumia siku 265 kwa kutembelea wilaya 38 na mikoa 20 ambapo walipokea malalamiko mbalimbali yakiwemo unyang’anyaji wa silaha wanazomiliki kihalali na kuhoji mashahidi 259 katika mikoa ya Ruvuma, Iringa, Morogoro, Pwani, Rukwa, Mbeya, Geita, Singida, Tanga, Arusha, Manyara, Shinyanga, Kigoma, Katavi, Kagera, Simiyu, Mara, Lindi na Tabora.

Mwigulu azungumza Katika hatua nyingine, alipotakiwa na HabariLeo Jumapili kuelezea hatma ya silaha za wanannchi zilizochukuliwa na serikali wakati wa Operesheni Tokomeza, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba alisema serikali ipo tayari kuzirejesha silaha hizo.

Waziri huyo alitumia mwanya huo kutoa mwito kwa wananchi wanaomiliki kihalali silaha ambazo zilichukuliwa wakati wa operesheni hiyo na hawajarudishiwa hadi leo, kufika kwenye vituo vya Polisi katika maeneo yao, wakiwa na nyaraka za umiliki silaha hizo.

Nchemba alisema wakati wa operesheni hiyo iliyoanza Oktoba mwaka 2013, silaha mbalimbali zilizokuwa zikitumika isivyo halali zilikamatwa na kwamba wale waliokuwa wanamiliki silaha hizo kihalali na wana nyaraka, wanapaswa kufika kwenye vituo vya Polisi vya maeneo yao kuulizia silaha zao.

“Ni kweli katika Operesheni Tokomeza ambayo ililenga kutokomeza ujangili dhidi ya tembo, silaha mbalimbali zilikamatwa na nyingine zilikuwa zikimilikiwa isivyo halali. “Sasa kwa yeyote anayemiliki silaha kihalali, alichukuliwa silaha yake na hakurudishiwa ni vyema akaenda kituo cha Polisi kwenye eneo lake akiwa na nyaraka halali za umiliki,” alisema Mwigulu. Kauli hiyo imekuja kutokana na malalamiko ya wananchi kwenye maeneo tofauti kuwa wengi hawajarejeshewa silaha zao

wanazozimiliki kihalali na kuzitumia kwa shughuli mbalimbali ikiwemo kujikinga na wanyama wakali.


Lijue Pori la Akiba la Selous


Pori la Akiba linatofautiana kwa kiwango kikubwa na Hifadhi za Taifa, tofauti kubwa ikiwa ni wakati Hifadhi za Taifa ni kwa ajili ya utalii, Pori la Akiba ni kwa ajili ya uhifadhi wa ikolojia unaokwenda sambamba na utalii mdogo na uwindaji katika vitalu.

Aidha wakati Hifadhi za Taifa zipo chini ya Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) na nyinginezo, Mapori ya Akiba yapo mbioni kuwa na Mamlaka yao kutokana na kuundwa kwa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) hivi karibuni.

Likiwa na eneo la kilometa za mraba kati ya 50,000, au asilimia tano ya sehemu ya nchi kavu ya Tanzania, Pori la Akiba la Selous ni moja ya maeneo makubwa yaliyohifadhiwa duniani.

Namna ya kufika Pori hilo linaweza kufikika kwa njia mbalimbali ikiwemo usafiri wa anga kutokana na kuwepo kwa kiwanja kidogo cha ndege eneo la Matambwe, usafiri wa Reli ya Tazara hadi Matambwe ambako ndiko liliko lango kuu la kuingilia. Unaweza kufika pia kwa barabara kilometa 300 kutoka Dar es Salaam kupitia Morogoro au kilometa 310 kutoka Dar es Salaam kupitia Kibiti mkoani Pwani. Njia nyingine ni usafiri wa maji katika ukanda wa mkoa wa Pwani.

Ni pori kubwa kuliko yote Afrika na lenye maji ya kutosha kiasi kwamba uwezekano wa kuwepo kwa binadamu kwa ajili ya makazi ungekuwepo, na hivyo ukweli huo unalifanya pori hilo kutofautiana na mapori mengine makubwa yaliyohifadhiwa Afrika.

Mapori kama hayo ni Pori la Namib-Naukluft la Namibia ambalo sehemu kubwa ni jangwa. Wageni wanaolitembelea Pori la Akiba la Selous hujikuta wakiwa katika nyika za asili mbali na maeneo yaliyozoea mapito ya kitalii. Wanyamapori waliopo katika pori hilo ni wa kushangaza, makundi ya wanyama wakiwemo nyati, tembo, viboko, mbwa mwitu na mamba ni wakubwa kuliko kote Afrika, lakini pia mfumo wa mito na maziwa ni wa kipekee katika Afrika Mashariki.

Pori hilo lina maeneo aina kwa aina yakiwemo maeneo wazi yenye nyasi fupi, misitu ya miombo, na misitu kando kando ya mito, lakini pia mabwawa ambayo ni tegemeo kubwa kwa wanyama na mimea. Sababu ya kuwa urithi wa dunia Ni kutokana na sifa hizo Umoja wa Mataifa ulilipa hadhi Pori la Selous kuwa eneo la Urithi wa Dunia kutokana na kuwa na ikolojia ya kipekee, ikidaiwa kuwa ndio pori pekee lililosalia Afrika likiwa na hali halisi ya kiuhalisia.

Kutokuwepo kwa shughuli nyingi za utalii, kunachangia kuwepo kwa hali ya nyika na ili kuhifadhi mazingira hayo na vile vile kuzuia utalii mkubwa ni utalii mdogo unaodhibitiwa ndio unaopewa kipaumbele zaidi. Sehemu kubwa ya Kanda ya Kaskazini ya Selous imetengwa kwa ajili ya utalii wa picha. Ni moja ya maeneo mazuri na yenye wanyama wengi.

Kanda hii imepakana na Reli ya Tazara kwa upande wa Kaskazini. Mashariki ni mpaka wa pori lenyewe na kwa upande wa Magharibi ni Stiegler’s Gorge pamoja na barabara iendayo Matambwe na kwa upande wa Kusini, mpaka ni Mto Rufiji. Mto mpana wa Rufiji na muelekeo wake wa kuzunguzunguka, hufanya maeneo mengi kuwa na ardhi oevu za maziwa na mabwawa na kufanya ikolojia ya kuvutia.

Source: Habari Leo
ZeroDegree.
Vita ya meno ya tembo ni tishio. Vita ya meno ya tembo ni tishio. Reviewed by Zero Degree on 10/09/2016 02:56:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.