Loading...

Majambazi waliohusika na mauaji ya polisi wanne wauawa

WATU wanne wanaotuhumiwa kuhusika kwenye mauaji ya askari Polisi wanne katika tukio lililotokea benki ya CRDB Mbande, wameuawa wakati walipokuwa wakipambana na Polisi.

Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro aliyasema hayo jana, na kueleza kuwa tukio hilo lilitokea Oktoba 10, mwaka huu saa 2:45 maeneo ya pori la Dondwe katika mpaka wa Chanika na mkoa wa Pwani.

Kamanda Sirro alisema Kikosi Maalumu cha Kupambana na Ujambazi wa kutumia silaha mkoani humo, kilifanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja baada ya kupata taarifa kwa raia wema kuwa ni jambazi na ndiye aliyehusika na mauaji ya askari hao.

Aliongeza kuwa baada ya kumkamata mmoja wa watuhumiwa, alikiri kuhusika na tukio hilo akiwa na wenzake saba, hivyo aliwaambia askari kuwa anawapeleka sehemu walipo wenzake kwenye pori la Dondwe, ambapo wanafanya mazoezi ya kivita.

“Walipofika eneo la mipakani huko Chanika kwenye pori hilo, ghafla majambazi walianza kufyatua risasi uelekeo wa askari, askari walilala chini na mtuhumiwa aliyeongozana na askari alikimbia. Ndipo askari walijibu mashambulizi na mapambano yalikuwa kwa dakika kadhaa,” alisema Kamanda Sirro.

Alisema walifanikiwa kupata bunduki ya kijeshi aina ya SMG iliyofutwa namba za usajili ikiwa na risasi 22 ndani ya magazini.

Aliongeza kuwa askari walifanikiwa kuwajeruhi majambazi hao wanne, ambao baadaye walikimbizwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar es Salaam kupatiwa matibabu na kufariki dunia kutokana na majeraha ya risasi.

Pia alisema uchunguzi wa awali, umebaini kuwa bunduki hiyo ndiyo aliyoporwa wakati askari wakiwa wanabadilishana lindo katika benki ya CRDB na kwamba upelelezi zaidid unaendelea.

ZeroDegree.
Majambazi waliohusika na mauaji ya polisi wanne wauawa Majambazi waliohusika na mauaji ya polisi wanne wauawa Reviewed by Zero Degree on 10/14/2016 09:04:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.