Loading...

Serikali na kiwanda cha nguo mkoani Morogoro kutoa ajira kwa vijana 1,000.

Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Eric Shitindi.
JITIHADA za serikali ya Awamu ya Tano ya kuongeza ajira kwa vijana zimeanza kuzaa matunda baada ya kusainiwa mkataba wa pamoja na kiwanda cha kutengeneza nguo za michezo cha Mazava Fabric & Production East Africa Ltd cha Morogoro ili kuwapatia mafunzo ya ufundi katika teknolojia ya kisasa vijana wapatao 1,000.

Mkataba huo umesainiwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, kupitia Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Eric Shitindi kwa niaba ya serikali na Meneja Mipango wa kiwanda hicho, Nelson Mchukya alisaini kwa niaba ya Mazava.

Shitindi alisema chini ya utaratibu huo, tayari vijana 360 wamekamilisha mafunzo ya aina hiyo katika kiwanda cha Tanzania Tooku Garment kilichopo mkoani Dar es Salaam na lengo la serikali ni kuwapatia vijana 27,000 mafunzo mbalimbali kwa ajili ya kuwawezesha kupata ajira katika maeneo mbalimbali nchini.

Katika hafla hiyo pia ulishuhudiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk Adelhelm Meru na Mkurugenzi wa Kanda Maalumu ya Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA), Joseph Simbakalia na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dk John Ndunguru.

“Tukio la kusainiwa kwa mkataba huo ni muhimu katika nchi yetu ambapo nia ya serikali kuona taifa linapiga hatua kubwa katika uchumi wa viwanda na ili kufikia lengo hilo hawana budi kuwa na wafanyakazi wenye kupata ujuzi wa kutumikia sekta ya viwanda… vivutio vya biashara si kodi pekee ni hata kuwa na wafanyakazi wenye ujuzi walioandaliwa kufanya kazi katika viwanda mbalimbali,” alisema.

Aliongeza kuwa, fursa hiyo imetolewa na serikali kwa vijana kutoka sehemu mbalimbali za nchi na kwamba ili kuwapata matangazo yanatolewa kwenye magazeti na vyombo vingine na hakutakuwa na mipaka ya sifa ya elimu.

Alisema Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo itakayogharamia mafunzo hayo, huku Kiwanda cha Mazava kitatoa eneo lake na wataalamu kwa ajili ya kuwafundisha vijana watakaochaguliwa kujiunga na mafunzo hayo katika awamu mbalimbali.

Dk Meru alisema hayo ni mageuzi makubwa katika suala la uwekezaji nchini, ambapo serikali imeamua kuwafundisha vijana wake ili wawe tayari kuajiriwa na viwanda vitakavyojengwa na pia kujiajiri wao wenyewe.

Alisema Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na wizara yake imeanzisha mpango huo maalumu kuwafundisha vijana ufundi stadi kwa kuandika na ushonaji wa nguo kwa gharama ya serikali.

Dk Meru alisema vijana hao 1,000 watapata mafunzo ya ushonaji ya muda wa miezi mitatu kila awamu, jambo litakalowawezesha wawekezaji katika sekta ya viwanda vya nguo kuajiri vijana wenye ujuzi.

Meneja Mipango wa kiwanda cha kutengeneza nguo za michezo cha Mazava Fabric & Production East Africa Ltd, Nelson Mchukya, alisema baada ya kusaini mkataba huo wapo tayari kuwapokea vijana 100 kuanzia Novemba 15, mwaka huu.

Meneja huyo alisema serikali itagharamia vijana hao posho, nauli, chakula, wakati kiwanda kitakuwa na jukumu la kutoa utaalamu wa mafunzo ya ufundi ushonaji nguo kwa kutumia mashine za kisasa kupitia wakufunzi waliopo.

Kiwanda cha Mazava Fabric & Production East Africa Ltd kinamilikiwa na Winds Enterprises (Hangzou) Ltd, ambapo kinajishughulisha na utengenezaji wa nguo za michezo na soko lake kubwa ni nchi za nje, hasa Marekani.

ZeroDegree.
Serikali na kiwanda cha nguo mkoani Morogoro kutoa ajira kwa vijana 1,000. Serikali na kiwanda cha nguo mkoani Morogoro kutoa ajira kwa vijana 1,000. Reviewed by Zero Degree on 10/29/2016 12:34:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.