Loading...

Umoja wa vijana wa Chama Cha Wananchi [ CUF ], wamjia juu Matatiro na wenzake.


JUMUIYA za Vijana wa Chama cha Wananchi ( CUF) katika mkoa wa Dar es Salaam, wameibuka na kulaani tabia inayojiita Kamati ya Uongozi ya chama hicho inayoongozwa na Julius Mtatiro, kutoa lugha za kubeza dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi.

Vijana hao wamedai hatua hiyo ya Mtatiro na wenzake, kutumia vyombo vya habari hasa redio na televisheni, kumkashifu Msajili wa vyama kwa maamuzi yake ya kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba kama mwenyekiti halali wa chama hicho kwa mujibu wa katiba, haikubaliki.


Viongozi wa vijana wa chama hicho katika wilaya za Temeke, Ilala na Kinondoni, wakizungumza na waandishi wa habari jana, walimtaka Mtatiro kuacha kuwakashifu viongozi hao vinginevyo wataomba uongozi kuwachukulia hatua kulingana na Katiba ya chama ikiwemo kuondolewa uanachama.

Akisoma taarifa ya upotoshaji unaofanywa na wanaojiita Kamati ya Uongozi wa chama hicho, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana wa chama hicho wilaya ya Ilala, Canal Shughuly, alisema Katiba ya chama hicho inaamini kwamba kila mtu ana wajibu wa kuheshimu utu, uhuru na haki za wengine pamoja na kutii sheria halali za nchi.


Shughuly aliongozana na Katibu wa Vijana wa chama hicho Ilala, Abdul Komesha na Katibu wa Kinondoni, Yusuph Kitogota alisema kitendo cha kubezwa kwa msajili pamoja na maamuzi yake wakati anatambulika kikatiba ni kuonesha jinsi alivyo mbumbumbu wa kuielewa katiba ya chama anachokiamini.


Alisema Mtatiro ni miongoni mwa vijana waliopata bahati ya kushika nafasi ya juu ya uongozi wa ndani ya CUF ya Naibu Katibu Mkuu bara ambayo aliteuliwa na Lipumba, lakini uteuzi huo ulitenguliwa baada ya kukumbwa na kashfa ya ubadhirifu wa Sh milioni 86 kwa ajili ya ununuzi wa bendera na vifaa vingine vya chama.


ZeroDegree.
Umoja wa vijana wa Chama Cha Wananchi [ CUF ], wamjia juu Matatiro na wenzake. Umoja wa vijana wa Chama Cha Wananchi [ CUF ], wamjia juu Matatiro na wenzake. Reviewed by Zero Degree on 10/06/2016 08:18:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.