Loading...

Wahusika utoroshaji wa makontena bandarini Dar wajisalimisha.

WAFANYABIASHARA wakubwa wanaodaiwa kutorosha makontena 100 bila kulipia kodi katika Bandari ya Dar es Salaam, wameanza kujisalimisha.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana.

Alisema wafanyabiashara waliohusika na suala hilo wameanza kujisalimisha tangu Jumamosi na kusistiza hakuna atakayesalimika.

“Mpaka sasa hakuna mfanyabiashara tuliyemkamata, kumbuka nilisisitiza kila aliyehusika ajisalimishe mwenyewe kabla hatujachukua hatua zaidi, tayari wameanza kujisalimisha tangu Jumamosi ya wiki iliyoisha,” alisema Waziri huyo.

Waziri Mwijage alisema hawezi kuiweka wazi hivi sasa kwa vile bado wasaidizi wake wanakusanya taarifa.

“Wengi wameanza kujisalimisha na kila siku wanakuja, hivyo siwezi kukupa takwimu ni wangapi wamekuja, sijapewa taarifa kamili bado wasaidizi wangu wanaendelea kuwapokea na kukusanya taarifa.

“Zile ‘bill’ zina namba inabidi tuende kwenye ‘ system’ ya TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) kule tunajua meli gani ilileta mzigo, nani alichukua na nani hakulipia, katika hatua huu tutajua mengi maana kuna chakula, madawa yalipita pale nataka kujua yapi hayakulipiwa ushuru,” alisema.

Awali akizindua Matokeo ya Sensa ya Viwanda ya mwaka 2013, waziri Mwijage alisema wapo watu wanaomshangaa na kumkosoa kwa hatua yake ya kwenda kukagua makontena bandarini,

Lakini alisisitiza kwamba kamwe hataacha kufuatilia ukaguzi wa makontena hayo kwa vile ndiyo kazi aliyoagizwa na Mkuu wake, Rais Dk. John Magufuli.

“Tuna viwanda vya nguo lakini haviwezi kuzalisha kwa asilimia 63 au 70 kwa sababu kuna nguo zinaingia nchini kama zile zinazozalishwa. Kimsingi siangalii bandarini, naangalia viwanda vyangu, nafanya kazi ya ukaguzi na kukusanya taarifa mtaani.

“Sijapewa tu uwaziri kuna mambo anaangalia (Rais Magufuli), najua jinsi nitakavyoyakagua nataka kuhakikisha walaji wanapata bidhaa bora lengo ni kulinda viwanda vyangu, asiyetaka nikague anyooshe mkono,” alisema.

Akizungumza matokeo ya utafiti wa Sensa ya Viwanda nchini, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dk. Albina Chuwa alisema matokeo ya utafiti huo yanaonyesha sekta ya viwanda imetoa ajira kwa watanzania 264,224 mwaka 2013.

“Kwa mwaka huo ilichangia uchumi kwa takriban Sh bilioni 8.0 na hadi kufikia mwaka huu kuna viwanda 50,656 vikiwamo viwanda vidogo 49,243,” alisema.

Alisema idadi ya viwanda kwa mkoa kwa vile vikubwa vyenye wafanyakazi 10 au zaidi, matokeo yanaonyesha kutoka a viwanda 1,322, Mkoa wa Dar es Salaam uliongoza kwa kuwa na viwanda 389 (asilimia 29.4).

“Ulifuatiwa na mkoa wa Manyara 167 (asilimia 12.6), Arusha 89 (asilimia 6.7), na Kilimanjaro 66 (asilimia 5.0). Mkoa wa Manyara, viwanda 149 sawa na asilimia 89.2 ya viwanda vinavyoshiriki katika shughuli za uchimbaji wa madini vilihusika zaidi na uchimbaji wa madini ya tanzanite,” alisema.

Source: Mtanzania
Zerodegree.
Wahusika utoroshaji wa makontena bandarini Dar wajisalimisha. Wahusika utoroshaji wa makontena bandarini Dar wajisalimisha. Reviewed by Zero Degree on 10/18/2016 10:53:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.