Loading...

Siri nzito imebainika kinachoendelea kati ya Pluijm na Haruna Niyonzima.

WAKATI mashabiki wa Yanga wakitofautiana juu ya kitendo cha mchezaji wao kipenzi, Haruna Niyonzima, kutopangwa au kuingizwa dakika za mwisho katika mechi za hivi karibuni, imebainika kinachoendelea kati yake na kocha mkuu wa timu hiyo, Hans van der Pluijm.

Kiungo huyo wa kutumainiwa wa Yanga na timu ya Taifa ya Rwanda, mwishoni mwa mwaka jana aliingia kwenye mgogoro mzito na Yanga baada ya kutimuliwa na uongozi wa timu hiyo huku chanzo kikitajwa kuwa ni utovu wa nidhamu.

Baadaye staa huyo aliomba radhi wanachama, viongozi na wachezaji wenzake kwa kile ambacho kilitokea na hilo lilimfanya kusamehewa.

Itakumbukwa kuwa mgogoro huo ulisababisha kutimuliwa kwa aliyekuwa katibu mkuu wa timu hiyo, Dk. Jonas Tiboroha, baada ya mwenyekiti wa timu hiyo na Kamati ya Utendaji kufanya uchunguzi na kugundua kwamba kiongozi huyo alikuwa akificha mawasiliano yake na kiungo huyo ili afukuzwe klabuni.

Tangu kufunguliwa pazia la Ligi Kuu Tanzania Bara Agosti 20 mwaka huu, Niyonzima ameshindwa kupata nafasi ya kuanza ndani ya kikosi cha mabingwa hao watetezi kutokana na sababu mbalimbali huku matatizo ya kifamilia yakitajwa kuhusika.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo zimepatikana kutoka ndani ya Yanga, zinasema kiungo huyo ameshindwa kupata nafasi ya kucheza kwa kile kinachodaiwa kushindwa kwenda na mfumo wa Pluijm.

Inadaiwa Pluijm amemchimba mkwara mzito nyota huyo akimtaka kuhakikisha anapandisha kiwango chake la sivyo ataozea benchi.

“Mwalimu (Pluijm) amesisitiza kwamba Niyonzima apandishe kiwango na kufuata mfumo wake la sivyo atakuwa kwenye wakati mgumu kupata nafasi kikosini,” kilisema chanzo hicho.

Kwa upande wake, akizungumza na waandishi wa habari, Niyonzima alisema matatizo ya kifamilia aliyonayo yamemfanya kushindwa kufanya kazi yake kwa ufanisi mkubwa na kusababisha kushindwa kuonekana uwanjani.

“Kaka nilikuwa nina matatizo makubwa sana ya kifamilia ndio maana umeona nimeshindwa kufanya vizuri, akili ilikuwa haiko sawa kwa kweli. Ila nashukuru nimeyapunguza baadhi,” alisema Niyonzima.

Kiungo huyo aliongeza kuwa hakuna tatizo lingine linalomkabili zaidi ya matatizo ya kifamilia na kuwaahidi wapenzi wa Yanga kukaa mkao wa kula na kupata vitu vizuri kutoka kwake.

“Mambo yatakuwa mazuri wasiwe na wasiwasi, mimi nipo sana tu Yanga sina tatizo na mtu yeyote wasubiri waone kazi,” alisema Niyonzima.

Niyonzima aliingia dakika za mwisho kwenye mchezo kati ya Yanga na Stand United na ule dhidi ya Simba uliopigwa Oktoba mosi Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Source: Bingwa
ZeroDegree.
Siri nzito imebainika kinachoendelea kati ya Pluijm na Haruna Niyonzima.  Siri nzito imebainika kinachoendelea kati ya Pluijm na Haruna Niyonzima. Reviewed by Zero Degree on 10/18/2016 10:59:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.