Loading...

Wazee Yanga wazidi kumtilia ngumu Manji.

Katibu wa Kamati ya Muafaka ya Wazee wa Yanga, Ibrahim Akilimali.
ZIKIWA zimebaki siku nne kabla ya kufanyika mkutano wa dharura wa wanachama wa Yanga, Kamati ya Muafaka ya Wazee wa klabu hiyo imesema Yanga haiwezi kukodishwa kama masufuria ya kwenda shughulini.

Uongozi wa Yanga umeitisha mkutano wa dharura kwa wanachama utakaofanyika Jumapili ya wiki hii ambapo kutakuwa na agenda takriban 14 za kujadiliwa, mojawapo ikiwa kuikodisha timu hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana, Katibu wa Kamati hiyo Ibrahim Akilimali alisema mfumo ambao mwenyekiti wa Yanga, Yusuph Manji anataka autumie katika kuingia mkataba wa miaka 10 kuimiliki nembo ya klabu unawagawa wanachama na mashabiki, kwani wengine wanautaka na wengine hawautaki.

Katika mkutano wa dharura wa klabu hiyo uliofanyika Agosti 6 mwaka huu, Manji aliwasilisha wazo la kuikodi klabu hiyo kwa miaka 10, jambo lililoridhiwa na wanachama walioliacha suala hilo kwa bodi ya wadhamini na siku chache zilizopita kulitolewa taarifa kwamba bosi huyo ameingia mkataba na kampuni ya Yanga Yetu kuikodi klabu kwa miaka 10, jambo lililozua mtafaruku na kuweka makundi mawili moja likikubali, lingine likikataa na kutaka ufuatwe utaratibu, kwa madai mchakato wa kwenda kwenye mkataba huo haukuwekwa wazi.

“Wote tunajua kwamba kulikuwa na mvutano wa Yanga asili na Yanga kampuni, baadaye tukakubaliana twende na Yanga Kampuni utaratibu kuwe na hisa, Yanga SC kuwe na hisa 51 na wanachama wawe na asilimia 49, na tulizunguka mikoa mingi ili kufuta mgogoro uliokuwepo na kuomba ridhaa ya wanachama wa klabu kukubali hisa na Manji akiwa ndio msimamizi mkuu wa muafaka huo, sasa leo inakuwaje yale hatujafika tulipotaka tena anaanzisha suala la kukodishwa klabu,” alisema Akilimali.

Pia Akilimali alisema hawataki kurudi katika mgogoro wa miaka saba, ambapo mwaka 2003 ndiyo walipata suluhisho na kukubaliana kuwa litumike jina ambalo lilikubaliwa na waasisi ambapo walikubaliana kuwe na Yanga SC na Yanga Corporation.

Akilimali alisema wakati Lloyd Nchunga anaingia madarakani timu ilikuwa na Sh milioni 200, lakini yeye alijiuzulu baada ya miaka miwili, akachaguliwa Manji akaongoza kwa miaka miwili kwa sababu ya upenzi wakaikanyaga katiba wakamwongezea muda ili wajipange na yeye ajipange watafute kiongozi na baadaye wakafikia muafaka kwamba wamchague yeye kama mwenyekiti wao kutoka kwenye kuwa mdhamini.

“Kabla haijafika hata miezi minane imeibuka suala la deni la Sh bilioni 11 na laki sita, jambo ambalo limetushtusha sana Wanayanga, limekuja tamko la mwenyekiti kuleta hoja kuwa akodishwe Yanga na lebo yake kwa muda wa miaka 10, kwasisi wote tunasema Yanga ni kubwa sana, Yanga haiwezi kukodishwa kama masufuria ya kwenda shughulini. Kupitia mimi na wazee wa kamati tumesema hatukubaliani na hilo,” alisema Akilimali.

Naye aliyekuwa Mwenyekiti wa Matawi ya Yanga, Mohammed Msumi alisema kutokana na Manji kuwa na mahitaji makubwa na klabu ni vyema akakaa pembeni na kuanzisha timu yake mwenyewe na kuacha Yanga iendeshwe na mfumo ambao umezoeleka.

ZeroDegree.
Wazee Yanga wazidi kumtilia ngumu Manji. Wazee Yanga wazidi kumtilia ngumu Manji. Reviewed by Zero Degree on 10/20/2016 09:29:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.