Loading...

Waziri Mwigulu azuia mapinduzi ya benchi la ufundi Yanga, amrejesha Pluijm kikosini.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Lameck Nchemba, amezuia mabadiliko ya benchi la Ufundi katika klabu ya Yanga, baada ya kufanikiwa kuushawishi uongozi wa Yanga SC kumrejesha kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm.

Mholanzi huyo alijiuzulu mapema wiki hii baada ya kukerwa na uongozi wa klabu kuleta kocha mpya, Mzambia George Lwandamina
bila kumtaarifu, akisema huko ni kumvunjia heshima.

Kocha huyo akakataa hadi nafasi ya Ukurugenzi wa Ufundi ambayo inasemekana Yanga ilitaka kumpa baada ya kumleta Lwandamina kuwa kocha Mkuu.

Lakini baada ya kuwaaga wachezaji siku moja kabla ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya JKR Ruvu timu ikishinda 4-0, Waziri Nchemba aliingilia kati suala hilo.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jana ofisini kwake, makao makuu ya Wizara ya Mambo ya Ndani makutano ya mitaa ya Ohio na Ghana, Nchemba alisema kwamba aliamua kuingilia sakata hilo kwa sababu yeye ni mdau wa michezo na mwanachama hai wa Yanga.

Alisema alikutana na pande zote, kocha huyo na klabu na kuwauliza juu ya mfarakano wao kabla ya kuwakutanisha pamoja kuwasuluhisha hadi wakafikia makubaliano ya kuendelea kufanya kazi pamoja.

“Tangu Pluijm amekuja Yanga, timu imechukua ubingwa mara mbili mfululizo, imefika hatua ya makundi Kombe la Shirikisho na mwaka jana ilishinda mataji yote, Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na Kombe la TFF,” alisema

Alisema takwimu zinaonyesha kocha huyo bora wa Ligi Kuu msimu uliopita ni mzuri, kwani katika kipindi chote hicho amepoteza mechi mbili tu za Ligi Kuu, hivyo hata kama uongozi unataka kufanya mabadiliko, Pluijm anastahili heshima yake.

Mapema jana uongozi wa Yanga ulimuandikia barua Pluijm kumuomba rudi kazini, timu ikijiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu dhidi ya Mbao kesho.

Uongozi wa Yanga ulitaka kumuondoa Pluijm na Wasaidizi wake wote, Juma Mwambusi, kocha wa makipa Juma Pondamali na Meneja Hafidh Saleh wote wazalendo na kuwaleta Mzambia Lwandamina atakayekuwa Kocha Mkuu, akisaidiwa na wazalendo Charles Boniface Mkwasa, Manyika Peter kocha wa makipa na Meneja, Sekilojo Chambua.

Pluijm, aliyezaliwa Januari 3 mwaka 1949, alikuwa anafundisha Yanga katika awamu ya pili baada ya awali kufundisha kwa nusu msimu mwaka 2014, akimpokea Mholanzi mwenzake, Ernie Brandts.

Alikwenda Al Shoalah FC ya Saudi ya Arabia na nafasi yake ikachukuliwa na Mbrazil, Marcio Maximo ambaye naye alifanya kazi kwa nusu msimu kabla ya Pluijm kurejeshwa Januari mwaka jana.

Saudi Arabia ambako alikwenda na aliyekuwa Msaidizi wake, Yanga SC, Charles Boniface Mkwasa – Pluijm aliondoka baada ya kutofautiana na uongozi wa timu uliotaka kumsajilia wachezaji asiowataka.

Pluijm alitaka kuondoka Jangwani baada ya kuiongoza Yanga katika jumla ya mechi 124, akishinda 77, sare 25 na kufungwa 22.
Katika mechi 19 za nusu msimu mwaka 2014, alishinda 11, sare sita na kufungwa mbili, wakati katika mechi 106 za tangu mwaka jana, alisema 66, sare 19 na kufungwa 20.

ZeroDegree.
Waziri Mwigulu azuia mapinduzi ya benchi la ufundi Yanga, amrejesha Pluijm kikosini. Waziri Mwigulu azuia mapinduzi ya benchi la ufundi Yanga, amrejesha Pluijm kikosini. Reviewed by Zero Degree on 10/29/2016 11:46:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.