Loading...

Rais Magufuli avunja mwiko na kuweka historia mpya JWTZ.

RAIS John Magufuli ametunuku Kamisheni kwa maofisa wanafunzi 194 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kundi la 59/15 katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam.

Hii ni mara ya kwanza kwa maofisa wanafunzi wa JWTZ kutunukiwa Kamisheni nje ya Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli kilichopo mkoani Arusha, na ni mara ya kwanza kwa maofisa wanafunzi wa JWTZ kutunukiwa Kamisheni ndani ya Ikulu.

Maofisa hao ambao 168 ni wanaume na 26 ni wanawake, wametunukiwa Kamisheni katika cheo cha Luteni Usu na sasa wamekuwa maofisa wapya wa JWTZ.

Kabla ya kutunuku Kamisheni, Rais na Amiri Jeshi Mkuu alikagua gwaride rasmi lililoandaliwa na maofisa hao wanafunzi wa JWTZ na baadaye akashuhudia uhodari wa askari kutoka kikosi cha maadhimisho cha JWTZ waliofanya onesho la gwaride la kimyakimya.

Akizungumza baada ya chakula cha mchana katika ukumbi wa Ikulu, Rais Magufuli alimpongeza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange, Makamanda na askari wote wa JWTZ kwa jukumu kubwa wanalolitekeleza la kuhakikisha nchi ipo salama na alisema Serikali itahakikisha inaboresha zaidi maslahi na mazingira ya kazi kwa jeshi hilo na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.

Aidha, Rais Magufuli alisema ameamua tukio hili la kutunuku Kamisheni lifanyike Ikulu jijini Dar es Salaam kwa lengo la kutoa heshima kwa maofisa wa JWTZ kama ambavyo viongozi wengine serikalini wamekuwa wakipata heshima ya kuapishiwa Ikulu.

"Kwamba Mawaziri tunapotaka kuwaapisha tunawaapishia hapa, Wakuu wa Mikoa tunawaapishia hapahapa, Makatibu Wakuu tunawaapishia hapahapa, kwa nini hawa Maofisa wa Jeshi tusiwaapishie hapahapa kwenye nyumba yao? “Ninyi ndio mnalinda nchi, ninyi ndio mnasimamia usalama wa nchi hii, lakini nikiuliza hapa inawezekana wengine mpaka wamekuwa Mabrigedia Jenerali hawajawahi kukanyaga Ikulu, wakati hapa ni kwenu," alisema Rais Magufuli.

Sherehe za kutunuku Kamisheni kwa maofisa hao wanafunzi zilihudhuriwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dk Hussein Mwinyi na Wakuu wa Jeshi la Ulinzi wastaafu na Majenerali wastaafu wa JWTZ.

Kabla maofisa waliotunukiwa kamisheni waliwasili katika viwanja vya nje ya Ikulu pembezoni mwa bahari, saa 3:50 asubuhi kwa gwaride lililoongozwa na Jackson Kalambo.

Ilipotimu saa 4:35 asubuhi, Rais Magufuli aliwasili katika viwanja hivyo na kukagua gwaride la kumaliza mafunzo hayo kisha kutoa zawadi kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika mafunzo hayo.

Washindi katika mafunzo hayo, mshindi wa jumla katika fani zote ni Abel Kaka, aliyefanya vizuri darasani ni Simon Donald, aliyefanya vizuri katika mafunzo ya medani ni Rajab Harunana na aliyefanya vizuri kwa wanawake ni Anastazia Renatus.

Ilipofika saa 4:55, Rais Magufuli aliwatunuku maofisa hao kamisheni, kisha wakiwa katika mistari kila mmoja alimgeukia mwenzake na kuvua vyeo walivyokuwa navyo na kuvalishana vipya na baadaye kula kiapo cha utii.

Akizungumzia mafunzo hayo, Mkuu wa Chuo Mafunzo ya Kijeshi Monduli, Meja Jenerali Paul Masao alisema katika kundi hilo la 59, walianza mafunzo Novemba mwaka jana wakiwa 222, lakini 27 waliachishwa mafunzo kwa sababu mbalimbali.

Alisema watunukiwa hao 193 walisoma mwaka mzima nchini huku mmoja akisomea Uingereza na kwa mujibu wa sheria, anatakiwa kufika kutunukiwa kamisheni hiyo na Rais akiambatana na wenzake.

Alisema waliowasindikiza maofisa waliotunukiwa kamisheni ni kundi la 60 na wapo 166 na sasa wapo muhula wa tatu na wanatarajia kumaliza mwezi Februari mwakani huku chuoni wakiwepo kundi la 61 ambao ni 468.

ZeroDegree.
Rais Magufuli avunja mwiko na kuweka historia mpya JWTZ. Rais Magufuli avunja mwiko na kuweka historia mpya JWTZ. Reviewed by Zero Degree on 11/27/2016 11:30:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.