Loading...

Vipodozi vyenye sumu vyanaswa mkoani Ruvuma.

IDARA ya Afya katika Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma imekamata vyakula vibovu na vipodozi vya sumu vyenye thamani ya Sh. 500,000.

Ofisa Habari wa Manispaa hiyo, Albano Midello, alisema juzi kuwa katika kuhakikisha udhibiti wa vyakula na dawa unakuwa endelevu, Idara ya Afya wiki hii imekamata vyakula vyenye thamani ya Sh.300, 000 baada ya kubainika vimekwisha muda wake na kuharibika.

“Idara pia imekamata chumvi isiyokuwa na madini joto yenye thamani ya Sh. 80,000 na vipodozi vyenye viambata vya sumu vyenye thamani ya Sh. 120,000,” alisema.

Kutokana na kukamatwa kwa vitu hivyo, alisema wahusika wametozwa faini ya Sh. 100,000 na gharama ya uteketezaji ya sh. 122,500.

Alitoa wito kwa wafanyabiashara wa vyakula na vipodozi kuacha kuuza bidhaa ambazo muda wa matumizi umekwisha au kuharibika ili kulinda afya za walaji na watumiaji.

Katika hatua nyingine, Midelo alisema bado kuna mlipuko wa ugonjwa wa kichaa cha mbwa katika Manispaa ya Songea na kwamba wataalam wa afya na mifugo wanaendelea kutoa chanjo na elimu ya kukabiliana na ugonjwa huo kwa jamii na watu waliong’atwa na mbwa.

Kwa mujibu wa Midello, kuanzia Novemba Mosi hadi 20, mwaka huu, watu 15 wameng’atwa na mbwa wanaodhaniwa kuwa na kichaa wakiwamo 13 kutoka Mtaa wa Osterbay, Kata ya Msamala.

Hata hivyo, alisema watu hao wamepatiwa chanjo ili kuzuia uwezekano wa kupata ugonjwa huo.

Midello alitoa wito kwa wafuga mbwa kuhakikisha mbwa wao wanapatiwa chanjo na kufangia kwenye vibanda vyao mchana ili kutoleta madhara kwa binadamu.

ZeroDegree.
Vipodozi vyenye sumu vyanaswa mkoani Ruvuma. Vipodozi vyenye sumu vyanaswa mkoani Ruvuma. Reviewed by Zero Degree on 11/27/2016 11:28:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.