Loading...

Serikali yaokoa zaidi ya bilioni moja katika ununuzi wa magari.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa GPSA, Jacob Kibona.
SERIKALI kupitia Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA), imeokoa Sh bilioni 1.3 baada ya wakala huyo kununua kwa pamoja magari 392 katika mpango wa serikali wa manunuzi ya pamoja.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa GPSA, Jacob Kibona alisema jana kuwa, fedha hizo zimeokolewa na serikali baada ya kununua magari 392 kwa pamoja kwa Sh bilioni 56.1 badala ya Sh bilioni 58.1 iwapo kila taasisi ingenunua magari yake.

“Kwa kweli huu mpango wa manunuzi ya pamoja ni mpango mzuri sana ambao unaiwezesha serikali kuokoa fedha nyingi,” alisema Kibona na kuongeza kuwa fedha zilizookolewa zitaiwezesha serikali kufanya shughuli nyingine za maendeleo ya umma na kama vile kuboresha miundombinu ya barabara, huduma za afya na elimu.

Aliongeza kuwa, taasisi yake pia katika kipindi cha Julai hadi Oktoba mwaka huu, imezikabidhi taasisi za serikali magari ya aina mbalimbali yapatayo 136.

Aidha, alisema katika kuhakikisha wanapunguza gharama katika manunuzi, wamekuwa wakinunua bidhaa kutoka kwa wazalishaji moja kwa moja ila inaposhindikana kutokana na sera za kampuni kubwa kuwa na mawakala wa usambazaji wamekuwa wakinunua kwa mawakala hao kwa makubaliano maalumu ya kupunguza bei.

Alisema kazi nyingine muhimu ya taasisi yake ni kugomboa mizigo kupitia bandarini, viwanja vya ndege na mipakani kwa niaba ya serikali ambapo kwa mwaka wa fedha uliopita waligomboa mizigo yenye thamani ya Sh bilioni 62.7 ikiwamo ya Mkongo wa Taifa, vifaa vya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wizara ya Maliasili na Utalii.

Aliongeza kuwa kwa kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka huu, pia walikomboa vifaa mbalimbali vya serikali zikiwamo ndege mbili zilizonunuliwa na serikali kutoka Canada aina ya Bombardier, vyote vikiwa na thamani ya Sh bilioni 100.97.

Alisema GPSA ina majukumu mengi, ikiwa ni pamoja kuhifadhi vifaa kwa ajili ya taasisi za serikali, kutoa huduma ya mafuta kwa magari ya serikali na kadhalika.


ZeroDegree.
Serikali yaokoa zaidi ya bilioni moja katika ununuzi wa magari. Serikali yaokoa zaidi ya bilioni moja katika ununuzi wa magari. Reviewed by Zero Degree on 11/30/2016 02:48:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.