Loading...

CCM yarudisha kivingine staili ya uvuaji magamba.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema matajiri wenye mikono michafu inayohusika na rushwa na dhuluma, wakae kando na chama hicho kwa kuwa kimeanza safari ya mageuzi ili kusimamia misingi ya uadilifu, haki, uaminifu na uwajibikaji.

Katibu wa Halmashauri Kuu Taifa (NEC), Itikadi na Uenezi, Humprey Polepole, aliyasema hayo juzi wakati akihojiwa na kituo kimoja cha runinga kuhusu mambo mbalimbali yanayoendelea ndani ya CCM likiwamo suala la mabadiliko yaliyofanywa hivi karibuni na vikao vya juu vya chama hicho.

“Kuwa tajiri si dhambi na si kwamba CCM inafukuza matajiri, hapana. Tatizo letu kama CCM katika mwelekeo mpya, mtizamo mpya na mageuzi yanayofanyika, hatuhitaji kuwa na aina ya matajiri wanaojipatia utajiri wao kwa hila, kwa rushwa na kwa dhuluma.

Polepole alisema tajiri aliyepata utajiri kwa hila, halipi kodi.

"CCM inajiweka kando naye tunaielekeza serikali kuwashughulikia watu wa aina hiyo na wanapokosea, wawajibishe kwa mujibu wa Katiba, sheria na taratibu za nchi," alisema Polepole.

“Ukijiona wewe ni tajiri na mikono yako ni michafu kwa maana ya kuwa na makando kando ya kukosa uaminifu, hulipi kodi, ukae mbali na CCM,” alisema.

Alisema CCM haiwachukii wafanyabiashara, bali inawachukia watu wasio waadilifu na wenye mikono michafu inayohusika na rushwa na dhuluma na kwamba ni wakati sasa kwa viongozi ndani ya CCM waishi kwenye mwenendo bora.

Aliongeza kuwa CCM ijayo itafika mahali ambapo kama mtu ana mambo mengi kwenye biashara yake kiasi kwamba hana muda wa kuhudumia chama na wanachama, ni bora akachagua moja.

Alisema CCM imeanza safari ya mageuzi makubwa ambayo faida yake itakuwa ni kwa wanachama na wananchi kwa ujumla kwa kusimamia misingi ya uadilifu, haki uaminifu, uwajibikaji.

Polepole alisema katika kuhakikisha chama kinajiimarisha kiuchumi na kuondokana na utegemezi, mwishoni mwa mwezi huu, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, atafanya ziara ya kufanya tathmini ya mali zote za chama.

“CCM ina mali nyingi, lakini kumekuwa na changamoto katika kuzisimamia kuhakikisha zinasaidia chama kijiendeshe chenyewe,” alisema.

Alisisitiza kuwa wapo watu wanaoweza kukejeli misimamo hiyo mipya ya CCM wakidhani haiwezi, lakini ikumbukwe baada ya uchaguzi mkuu, Rais John Magufuli aliahidi mambo mengi kwa wananchi ikiwamo kupambana na rushwa ambalo limeanza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa na taasisi za serikali kukusanya mapato kihalali.

Alisema hivi sasa nidhamu kwenye utumishi wa umma imekuwa ya hali ya juu ukilinganisha na miaka iliyopita, kwani watumishi wamejiweka kwenye fikra za jinsi mkuu wa nchi anavyotaka na ambaye ndiye mtumishi namba moja.

Aliongeza kuwa mabadiliko yaliyofanywa na vikao vya juu kupunguza wajumbe wa NEC na idadi ya vikao kufanyika, inalenga kupunguza matumizi ya fedha kwenye chama.

“Haiwezekani ikafanyika nidhamu ya matumizi ya fedha kwenye serikali halafu chama kikawa kinafanya mikutano kama vile hatuoni nini kinafanyika serikalini,” alisema.

Polepole alisema kuwapo kwa vikao vingi ndani ya chama, ilikuwa haitoi fursa kwa chama kujitathmini mambo yaliyofanyika na kwamba baada ya kupunguza idadi ya vikao kitajitathmini vizuri.

Alisema katika mabadiliko ya utendaji kazi, NEC imekubaliana kwamba ifike wakati asipenye mla rushwa kwenye CCM kuupata uongozi, tumefanikiwa mwaka jana na tunataka tufanikiwe zaidi kipindi hiki cha kuelekea uchanguzi ndani ya chama utakaofanyika mwakani. “Tunataka watu waaminifu, waadilifu, wawajibikaji na wanaokipenda chama kweli katika imani yao. Tunataka CCM iwe kimbilio la wanyonge wanaojua kutatua kero za wananchi,” alisema Polepole.

Source: Nipashe
ZeroDegree.
CCM yarudisha kivingine staili ya uvuaji magamba. CCM yarudisha kivingine staili ya uvuaji magamba. Reviewed by Zero Degree on 12/20/2016 10:30:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.