Loading...

Wajumbe wamuidhinisha Donald Trump kuwa mshindi wa kiti cha urais nchini Marekani.

Donald Trump sasa amehakikishiwa kuwa Rais wa 45 wa Marekani.
Wajumbe wa Jopo la Kuamua Mshindi wa Urais nchini Marekani wamemuidhinisha Donald Trump kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika Novemba.

Hii ni licha ya juhudi za dakika za mwisho za kutaka kumzuia kuingia ikulu ya White House mwezi Januari.

Wiki sita baada ya uchaguzi mkuu kufanyika tarehe 8 Novemba, mwanachama huyo wa Republican amepata zaidi ya kura 270 za wajumbe ambazo alikuwa anahitaji kufanya rasmi ushindi wake.

Baada ya ushindi huo, Bw Trump ameahidi "kufanya kazi kuunganisha nchi ya marekani na kuwa rais wa Wamarekani wote".

Wajumbe walikuwa wametumia ujumbe mwingi kupitia barua pepe na pia kupigiwa simu wakihimizwa kutomuunga mkono bilionea huyo kabla yao kukutana kupiga kura.

Shughuli yao ya kupiga kura kwa kawaida huwa kama shughuli ya kutimiza wajibu tu, ambapo huwa wanamuidhinisha mshindi, lakini mwaka huu uchaguzi umegubikwa na tuhuma za kuingiliwa na wadukuzi kutoka Urusi.

Jimbo la Texas hatimaye lilimuwezesha kufikisha idadi ya kura 270 za wajumbe alizohitaji,, licha ya wajumbe wawili wake kugeuka na kupiga kura kumpinga.

Gazeti la New York Times pia linaripoti kwamba kuna wajumbe wanne wa chama cha Democratic, chake Hillary Clinton, ambao walimpigia kura mgombea mwingine lakini Bi Clinton.

Matokeo ya kura hiyo yatatangazwa rasmi tarehe 6 Januari kwneye kikao maalum cha pamoja cha bunge la Congress.

"Nawashukuru Wamarekani kwa kunipigia kura kwa wingi kuwa rais wa Marekani," Bw Trump alisema kupitia taarifa baada ya matokeo kutangazwa.

"Kwa hatua hii ya kihistoria, tunaweza sasa kutazama mbele na kutarajia maisha ya kufana siku za usoni. Nitafanya kazi kwa bidii kuunganisha nchi yetu na kuwa rais wa Wamarekani wote," alisema.

Donald Trump alitumia ukurasa wake wa Twitter kuwashukuru wafuasi wake.
Makamu wa rais mteule Mike Pence alimpongeza mkubwa wake kwa ushindi kupitia Twitter, na kuandika: "Hongera kwa @realDonaldTrump; ameteuliwa rasmi kuwa Rais wa Marekani leo na Jopo la Kuamua Mshindi wa Urais."
Aliongeza kwamba ni heshima kubwa kwake kuchaguliwa kama makamu wa rais wa Marekani.

Ujumbe wake kwenye Twitter ulipendwa sana na kusambazwa mara nyingi mtandaoni.

'Hatutaki uhaini, hatutaki Trump!'

Waliokuwa wanafanya juhudi za kumzuia Bw Trump walikuwa wamepigana vikali kuwashawishi wajumbe wa chama cha Republican kutomuunga mkono mgombea wa chama chao.

Mamilioni ya Wamarekani walitia saini ombi mtandaoni kuwahimiza wajumbe hao kutomuunga mkono Bw Trump.

Siku ya kufanyika kwa uchaguzi, maelfu ya watu wanaompinga Trump walikusanyika na kuandamana katika miji mikuu ya majimbo kote nchini humo.

Waandamani Augusta, Maine wakimpinga Trump.
Katika jimbo la Pennsylvania, zaidi ya waandamanaji 200 walivumilia baridi kali na kuandamana wakiimba, "Hatutaki Trump, hatutaki KKK, hatutaki Wafashisti Marekani!" na "Hatutaki uhaini, hatutaki Trump".

Jimbo la Maine, waandamanaji walipiga ngoma na kubeba mabango yaliyosema, "Msiache Putin Aamue Rais Wetu," - wakirejelea tuhuma kwamba wadukuzi walioungwa mkono na serikali ya Urusi walijaribu kuvuruga uchaguzi kumfaa Bw Trummp.

Kimsingi, waliokuwa wanampinga Bw Trump hawakuwa na nafasi ya kuzuia ushindi wake.

Ndipo waweze kumzuia kuingia ikulu, wangehitaji kuwashawishi wajumbe 38 wa chama cha Republican kubadili msimamo wao.

Na hilo huenda labda lingechelewesha tu ushindi wake.

Iwapo kungetokea iwe kwamba hakuna mgombea aliyefikisha kura 270 za wajumbe, Bunge la Wawakilishi ndilo lingekuwa na jukumu la kuamua nani angekuwa rais.

Ikizingatiwa kwamba bunge hilo linadhibitiwa na chama cha Republican, bila shaka wangemchagua Bw Trump.

Mwandamanaji mjini Los Angeles akiwahimiza wajumbe.

ZeroDegree.
Wajumbe wamuidhinisha Donald Trump kuwa mshindi wa kiti cha urais nchini Marekani. Wajumbe wamuidhinisha Donald Trump kuwa mshindi wa kiti cha urais nchini Marekani. Reviewed by Zero Degree on 12/20/2016 10:37:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.