Loading...

Gwaride lamwisho jijini Dar, ...Sherehe za uhuru kufanyikia Dodoma kuanzia mwakani.

SHEREHE za maadhimisho ya Uhuru wa Tanzania Bara, hazitafanyika tena Dar es Salaam na badala yake zitakuwa zinafanyika Dodoma kuanzia mwakani, ikiwa ni dhamira ya Serikali kuhamia rasmi katika mji huo.

Pia gwaride hilo la jana, litakuwa la mwisho kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange, anayetarajiwa kustaafu Desemba 31, mwaka huu.


Kustaafu huko kwa Mwamunyange, kunatokana na kumalizika kwa mwaka mmoja wa kutumikia nafasi hiyo alioongezewa na Rais John Magufuli, Januari 30, mwaka huu.

Mwisho wa Enzi Dar

Akihutubia jana kwenye halaiki iliyohudhuria maadhimisho ya miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Uhuru, Rais Magufuli alisema maadhimisho ya mwaka huu yatakuwa ya mwisho kufanyika Dar es Salaam kwa kuwa yanayofuata yatakuwa yakifanyika Dodoma, ambako ni makao makuu ya nchi.

“Hizi ni sherehe za mwisho kufanyika hapa Dar es Salaam. Mwakani zitafanyika Dodoma, wapenda gwaride wajiandae kusafiri kuelekeza Dodoma. Sherehe za Uhuru ni za umuhimu na tutaendelea kuziadhimisha, lakini kwa wakazi wa Dar es Salaam sherehe hizi za leo zitakuwa za mwisho kwao,” alisema.


Rais Magufuli alisema maadhimisho ya Uhuru kwa mwaka jana hayakufanyika kutokana na gharama kubwa iliyokuwa itumike kuyaandaa.

Alitaja sababu nyingine ni kutokana na yeye kuwa na muda mfupi ofisini kwa wakati huo, akiwa hajateua hata baraza la mawaziri.

“Nilipoambiwa gharama za sherehe hizo kwa mwaka jana kuwa ni Sh. bilioni nne, nikawauliza kuna mambo yapi ambayo yatafanyika. Wakanijibu itakuwa kualika wageni, watakula chakula, kutakuwa na posho nikauliza hizo posho na chakula watakula Watanzania wote? Wakasema ni wale wachache watakaokuwa wamealikwa ndiyo maana nikaamua hizo bilioni nne ziende kupanua barabara ya Ally Hassan Mwinyi ambayo inapitiwa na Watanzania wote,” alisema. 



Aliongezea kuwa: “Inawezekana niliwakosea Watanzania naomba mnisamehe, lakini ule uamuzi ulikuwa wa msingi wa kupunguza msongamano na Watanzania wengi wataitumia katika maisha yao yote.”

Aidha, Rais Magufuli alisema katika maadhimisho ya sherehe za miaka 55, ameamua zifanyike kwa sababu gharama zake ni ndogo na hakutakuwa na dhifa ya taifa.

Sherehe hizo zilizoongozwa na kaulimbiu ya ‘‘Tuunge Mkono Jitihada za Kupiga Vita Rushwa na Ufisadi na Tuimarishe Uchumi wa Viwanda kwa Maendeleo yetu’, zilihudhuriwa na viongozi wa ndani, huku kukiwa hakuna marais wa nchi au wawakilishi wao kama ilivyozoeleka.


Badala yake, waliwakilishwa na mabalozi wao walioko nchini.

Rais alisema katika kipindi cha miaka 55 ya Uhuru, kuna mafanikio mengi yaliyopatikana, lakini kuna watu wanayabeza na kusema ukweli ni kwamba Tanzania ya leo ni tofauti na ile ya mwaka 1961.

“Kwanza tumelinda uhuru wa nchi yetu, tumelinda mipaka yetu, mipaka yote iko salama. Tunafanya mambo yetu sisi wenyewe bila kuingiliwa, wapo waliojaribu kutishia uhuru wetu lakini wameshindwa.

Tuko imara tumedumisha Amani, umoja na mshikamamo wa nchi yetu, tangu tumepata uhuru nchi imeendelea kuwa na amani na wananchi wamebaki kuwa wamoja. Hakuna ubaguzi, tumeudumisha Muungano wetu,” alisema Magufuli.

MAFANIKIO YA MIAKA 55

Rais Magufuli alisema katika miaka 55, serikali imejenga miundombino ya kiuchumi ikiwamo barabara, madaraja, vivuko, meli, reli, viwanja vya ndege , miradi ya umeme na maji.

Alisema huduma za afya na elimu zimeboreshwa na kusogezwa karibu na wananchi wakati zamani iliwalazimu watu kutembea umbali mrefu kufuata huduma za shule au hospitali.

Pia alisema nchi imeng’aa kimataifa kutokana na mchango ilioutoa katika ukombozi wa bara la Afrika katika kutafuta amani na kupinga uonevu duniani.

“Napenda kuwapongeza viongozi wa awamu mbalimbali za uongozi wa nchi yetu kwa kazi kubwa walizofanya na kuwezesha kupatikana kwa mafanikio haya.

Wa kwanza ni Marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, mzee wetu (Abeid Amani) Karume, Mzee wetu Ali Hassan Mwinyi, Benjamini Mkapa na Jakaya Kikwete na pia nawapongeza viongozi wa Zanzibar walioshiriki kutufikishia maendeleo haya,” alisema.

CHANGAMOTO

Rais Magufuli alisema licha ya mafaniko hayo, bado kuna changamoto na matatizo ya umaskini ambayo serikali inapambana kuyatatua, yakiwamo ukosefu wa ajira, huduma za jamii na rushwa. Alisema suala la ufisadi na rushwa kwa baadhi ya watendaji wa serikali bado ni tatizo.

Alisema wakati serikali ikijitahidi kuwaapunguzia wafanyakazi kodi zinazotokana na mishahara (PAYE) kutoka asilimia 11 hadi tisa wamejikuta hadi sasa wana wafanyakazi hewa 19,000.

Rais Magufuli alisema serikali imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) kwa kaya zilizo maskini, lakini imegundua hadi sasa kuna kaya maskini hewa zipatazo 55,000.

“Wakati tunajitahidi kuboresha wanafunzi kwa kusoma bure, tumekuta hadi sasa tuna wanafunzi hewa 65,000 na mambo mengine mengi.

Kwa hiyo napenda kuwathibitisha Watanzania katika juhudi ambazo tunazichukua katika serikali ya awamu ya tano ni kwa lengo la kuboresha maslahi ya Watanzania wote na si kuboresha maslahi ya watu wachache kama walivyokuwa wamezoea kula jasho la watu wengine,” alisema.

Alisema serikali itaendelea kuchukua hatua kali ikiwa ni pamoja na kuwatumbua wale ambao wamekuwa wakitumbua mali zaa Watanzania hadharani.

“Wale wanaohusika kupata malipo yao kutokana na kutufikisha hapa tulipo waweze kushughuikiwa kikamilifu na serikali yangu imejipanga kuondoa uonevu kwa wananchi tutaendelea kushirikiana na kutatua changamoto ili waananchi wanyonge wanufaike na Tanzania yao,” alisema Rais.

Alisema serikali ya awamu ya tano inawahakikishia wananchi kuwa itaendelea kutatua changamoto hizo na tayari wameanza kuzishughulikia.

Rais Maagufuli alisema kuna wazee 17 ambao walijitoa muhanga kupigania uhuru wa nchi ambao walikuwa waanzilishi wa Chama cha Tanu wakiongozwa na Mwalimu Nyerere, hivyo wanapaswa kukumbukwa.

“Kama isingekuwa ujasiri wao, huenda hadi leo tungekuwa bado tunatawaliwa kwa hiyo tunawashukuru sana kwa sababu walijitoa kwa hiari yao kutafuta uhuru wa Watanzania ili tuwe huru,” alisema.

MIKAKATI YA SERIKALI

Rais Magufuli akiwahutubia maelfu ya Watanzania waliojitokeza katika uwanja huo alisema serikali ya awamu ya tano iliingia madarakani Novemba 5, mwaka jana, baada ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu katika kampeni na walinadi ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo ilisheheni mambo mengi na wananchi wakawakubali na kuwapa kura.

Alisema waliahidi kujenga misingi imara ya kufanya nchi kuwa ya uchumi wa kati kwa kuongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025.

“Kulingana na dira yetu ya taifa ya maendeleo, tuliahidi kupambana na uzembe na ubadhilifu serikalini pamoja na kuboresha huduma za jamii kama vile afya, elimu na maji,” alisema Magufuli.

Alisema suala hilo wameanza kulishughulikia na katika bajeti ya mwaka huu, Sh. bilioni 29.5 sawa na aslimia 40 ya fedha zote, zimeelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.

Rais alisema katika miradi hiyo ya maendeleo, serikali imeanza kuziwekea mikakati ili kuhakikisha nchi inajengeka kiuchumi kwa kuanzisha miradi ya umeme kama ule wa Kinyerezi.

Pia alisema katika miundombinu, serikali imetenga zaidi ya Sh. trillion 5.6 huku Sh.trilioni moja zkitengwa kwa ajili ya reli.

Kwa upande wa usaafiri wa anga, alisema serikali imenunua ndege sita na tatu ni aina ya Q400 Bombardier zenye uwezo wa kubeba abiria 76, mbili aina ya CS300 zitaanzaa kutumika kwa mara ya kwanza Afrika na zitabeba abiria kati ya 137 na 150 ambazo zitaletwa mwaka 2018 .

Alisema ndege nyingine ambayo ni kubwa zaidi, ambayo serikali imeshamaliziwa kulipa fedha ni aina ya Boeing 787 yenye uwezo wa abiria 262. Alisema lengo la kufanya hivyo ni kujenga uchumi wa nchi na utalii.

Alisema hiyo ni mikakati ambayo wanaendelea nayo na katika sekta ya afya bajeti imeongezeka fedha za zilizoteangwa za kununua dawa zimeongezeka kutoka Sh. bilioni 31 hadi Sh. bilioni 250.

Aidha, alisema katika sekta ya elimu, serikali imeongeza bajeti ya fedha na kuanza kutoa elimu bure kwa kutenga Sh. billion 18.77 kila mwezi.

“Katika elimu ya vyuo vikuu tumeongeza bajeti kutoka Sh. bilioni 340 zilizotengwa mwaka jana hadi Sh. bilioni 483, hivyo kuongeza idadi ya wanafunzi watakaojiunga na chuo kikuu,” alisema.

VIONGOZI WALIOHUDHURIA

Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kiserikali akiwamo Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein; Makamu wa Rais , Samia Suluhu Hassan; Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa; Jaji Mkuu Othman Chande; Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.

Wengine ni Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi; Makamu Mwenyekiti CCM Bara, Philip Mangula; Spika wa zamani wa Zanzibar, Pandu Ameir Kificho; mabalozi na wakuu wa taasisi mbalimbali.

VIONGOZI AMBAO HAWAKUWAPO

Hata hivyo, katika hali isiyo ya kawaida kwa Sherehe za Uhuru baadhi ya viongozi wastaafu wa ngazi ya juu ya Serikali hawakuonekana katika sherehe hizo, hata wale wa kutoka nchi za jirani.

Viongozi wa ndani wa ambao hawakuonekana ni pamoja na Spika wa Bunge, Job Ndugai; Naibu Spika Dk. Tulia Ackson, Rais mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa, Rais mstaafu awamu ya nne, Jakaya Kikwete na mawaziri wakuu wastaafu wote.

MATUKIO YALIYOVUTIA

Sherehe hizo pia zilipambwa na matukio mbalimbali ikiwamo kwata ya kimya kimya na vikundi mbalimbali vya majeshi ya ulinzi na usalama.

Pia makomandoo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWT) walikuwa kivutio kwa wageni waalikwa kwa uhodari wao wa kuonyesha mbinu za kumwadhibu adui. Sherehe hizo pia zilipambwa na ngoma ya Msihaya na Mkera.

Mbali na matukio hayo pia gwaride lililojumuisha vikundi vya majeshi ya ulinzi na usalama ya Tanzania lilikuwa kivutio baada ya kupita kwa mwendo wa ukakamavu mbele ya Rais Magufuli.

Credits: Nipashe
ZeroDegree.
Gwaride lamwisho jijini Dar, ...Sherehe za uhuru kufanyikia Dodoma kuanzia mwakani. Gwaride lamwisho jijini Dar, ...Sherehe za uhuru kufanyikia Dodoma kuanzia mwakani. Reviewed by Zero Degree on 12/10/2016 09:37:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.