Loading...

Haya hapa mambo matano yanayoigharimu Klabu ya Arsenal.

ARSENAL wamepokea kichapo cha pili mfululizo wakiwa ugenini na kuongeza tofauti ya pointi 9 baina yao na vinara wa ligi, Chelsea.

Awali walichezea kichapo cha bao 2-1 mbele ya Everton, kisha wakapata kipigo hicho hicho mbele ya Manchester City na kuibuka hofu kubwa kwa mashabiki wao.

Kama washika mitutu wa jiji la London wasipokuwa makini, huenda huu ndio ukawa mwanzo wa mwisho wa ndoto zao za ubingwa msimu huu, kwanini? Hizi hapa sababu 5 zinazowagharimu kwa sasa.

Hawajiamini


Wiki moja kabla ya vichapo hivyo viwili, Arsene Wenger alijitokeza hadharani na kukimwagia sifa kikosi chake kwa ushindi wa mabao 3-1 walioupata dhidi ya Stoke City.

Kwa haraka haraka huenda usione tatizo, lakini kimsingi hapa ndipo Wenger alipotengeneza balaa kwenye kikosi chake.

Mara kwa mara Arsenal wamekuwa na utamaduni wa kupongezana pindi wanapopata matokeo ya kushtua, hali inayowapa kujiamini sana.

Akili hii ya kujiamini ndiyo imewafanya waingie kwenye michezo miwili ya Goodison Park na Etihad bila umakini na matokeo yake kuambulia vichapo.

“Ni wiki mbaya sana kwetu,” alisema Wenger alipohojiwa na mtandao wa Sky Sports, lakini kabla alianza kushusha lawama kwa waamuzi na ratiba.

“Lakini pamoja na yote, tuko sawa kisaikolojia na tutarudi imara baada ya matokeo haya.”

Katika hali ya kawaida huu ulikuwa ujumbe wa kujenga kitu kilichoanza kubomoka na kwa namna moja au nyingine alionyesha wazi udhaifu wa Arsenal pindi wanapokuwa kwenye nyakati ngumu.

Hakika kuna jambo ambalo Wenger anatakiwa kulifanyia kazi kwa haraka kwa kujenga saikolojia ya wachezaji wake ikiwa wana nia ya kubeba taji msimu huu.

Matokeo mechi kubwa


Changanya uwezo wa Arsenal kupata matokeo wanapokuwa kwenye presha na matokeo yao dhidi ya timu kubwa, bila shaka utabaini tatizo kubwa linalowakabili.

Kwenye mechi tisa na timu za chini ya msimamo, Arsenal wameshinda saba na kupata sare mbili. Wamepata ushindi mnono kwa timu kama Hull City, Sunderland na West Ham, lakini dhidi ya timu kubwa za juu hali ni tofauti kidogo.

Wameshinda michezo mitatu kati ya nane ya timu za juu kwenye msimamo, wamefungwa na Liverpool, Everton na Manchester City kisha wakapata sare dhidi ya Tottenham na Manchester United.

Ushindi pekee wa Arsenal wanaoweza kujivunia nao msimu huu ni ule waliopata dhidi ya Chelsea.

Kwa sasa wanatakiwa kushinda michezo yao ijayo kabla ya safari ya Februari 4 pale Stamford Bridge watakaporudiana tena na Chelsea.

Uchovu


Baada ya kipigo cha Manchester City, Wenger alishusha lawama kwa refa na kuponda utayari wa mwili wa wachezaji wake kama sababu za wao kupoteza mchezo huo.

Huu ulikuwa mchezo wanne kwa Arsenal kucheza ugenini katika michezo yao mitano ya hivi karibuni hivyo Wenger anaamini kuwa wachezaji wake hupoteza nguvu kipindi cha pili.

“Nafikiri tulitoka mchezoni kipindi cha pili,” alisema Wenger. “Uliona tulivyokosa maamuzi ya haraka pindi tulipokuwa na mpira miguuni na hii ikawapa nafasi ya kutushambulia, hatukuwa vile kipindi cha kwanza.”

Huenda kweli Arsenal walikuwa na uchovu wa safari kutoka Liverpool mpaka Manchester, lakini ukweli ni kwamba ili uwe bingwa England ni lazima ujue namna ya kupita kwenye ratiba hizi.

Majeruhi


Ukiachana na uchovu, majeraha yameendelea kuwa chanzo kikubwa cha Arsenal kupata matokeo mabovu.

Ikumbukwe walipata sare dhidi ya Manchester United na PSG, beki wao wa kulia, Hector Bellerin akiwa nje.

Vichapo viwili vya hivi karibuni wamevipata baada ya kumkosa beki wao kisiki waliyemsajili kutoka Valencia, Shkordan Mustafi huku pengo la Cazorla likiendelea kuonekana mpaka leo hii.

Mpaka sasa Arsenal wana orodha ya wachezaji wanane ambao wako nje wakiuguza majeraha yao, ni Sunderland pekee waliowazidi kwa kuwa na majeruhi tisa.

Kupwaya kwa ukuta


Kwa mara ya kwanza tangu atue Premier League, Petr Cech ameruhusu nyavu zake kutikiswa kwenye michezo nane mfululizo.

Mpaka hapa utagundua udhaifu wa safu ya ulinzi unaoikabili klabu ya Arsenal kwa sasa.

Wamefungwa mabao machache kuliko Liverpool na Manchester City, lakini cha ajabu wawili hawa wako juu yake kwenye msimamo wa ligi.

“Kama unataka kufika juu unatakiwa kuhakikisha nyavu zako haziguswi kila siku,” alisema Wenger muda mfupi kabla ya mchezo dhidi ya City.

Huenda mabao ya City yalikuwa na utata lakini bado hili haliondoi udhaifu wa safu yao ya ulinzi kwenye mchezo huo.

Ni wakati sasa wa kuutumia mchezo wao wa Boxing day dhidi ya West Brom ili kuanza upya rekodi yao ya kutoruhusu mabao ili waweze kurejesha matumaini yao ya kubeba taji msimu huu.

Source: Dimba
ZeroDegree.
Haya hapa mambo matano yanayoigharimu Klabu ya Arsenal. Haya hapa mambo matano yanayoigharimu Klabu ya Arsenal. Reviewed by Zero Degree on 12/22/2016 11:48:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.