Loading...

Kardinali Pengo atoa ya Moyoni.

ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amewashangaa watu wanaolalamika maisha ni magumu wakati serikali ya awamu ya tano imejitahidi kuboresha miundombinu yenye kuleta unafuu wa maisha.

Katika salamu zake za Krismasi kwa Watanzania, Askofu Pengo alisema hali ya maisha kwa sasa imeboreka zaidi kwani barabara nyingi zimetengenezwa kurahisishia usafirishaji wa biashara kati ya nchi na nchi jirani na kati ya mkoa na mkoa.

Pia alisema kitendo cha Serikali kununua ndege kadhaa kwa ajili ya Kampuni ya Ndege (ATCL) kumerahisisha maisha ya Mtanzania kwani kunawezesha watu kusafiri kwa haraka kwa gharama ndogo.

"Kwa mfano Arusha kwa ndege tulikuwa tunaenda kwa Sh 800,000, lakini sasa hivi unaweza kwenda kwa gharama kati ya Sh 360,000 na Sh 400,000 kwa kutumia ndege za Serikali, napata shida kusema hali ya maisha ni ngumu," alisema Askofu Pengo.

Kuhusu amani Pengo alisema katika awamu hii ya tano, kuna amani kubwa na akatoa mfano wa kisiwani Zanzibar kuwa siku za nyuma watu waliishi kwa wasiwasi mkubwa kutokana na watu kumwagiwa tindikali na viongozi wa dini ya Kikristo kupigwa risasi, lakini sasa hivi kuna amani kuliko wakati uliopita.

"Kule Zanzibar, hali ilikuwa ya kutia mashaka, sisi hatukujua tukimbilie wapi kutokana na mashambulizi yale yaliyolenga watu wa dini moja, lakini kwa sasa amani ni kubwa zaidi kuliko awamu iliyopita," alisema Askofu Mkuu Pengo.

Aliwakumbusha Watanzania kwamba kila mtu akisimama na kutambua wajibu wake wa kudai amani, hali itakuwa nzuri zaidi. Pia alitoa mwito Watanzania wasifarakane kwa sababu ya dini na akawataka waamini wa Kikatoliki wawe wa kwanza kutetea amani na mapatano dhidi ya watu wa dini nyingine.

Pia alisema pamoja na tofauti za dini na itikadi za kisiasa, Wakatoliki wanatakiwa kuwa na msimamo wa kutetea umoja na amani.

Asema amani italetwa na masikini, si matajiri

Akizungumza kwenye mkesha wa Krismasi katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph, Dar es Salaam, Pengo alisema watu maskini ndio wenye kuleta amani katika nchi kutokana na kukesha kulinda amani na usalama wa nchi huku matajiri wakiwa wamelala.

"Matajiri wao huwa wanakesha kwenye nyumba za starehe, wakiwa wanakunywa na kufanya anasa za kila aina, wanakesha huko hadi asubuhi baada ya hapo wanakuwa hawana uwezo wa kufanya kitu chochote," alisema Pengo.

Aliongeza kuwa, lakini maskini wao hawakeshi kwenye ulevi na kwenye ulafi kama ilivyo kwa matajiri, bali wakati wowote wako tayari kutekeleza majukumu yao na ndio maana Mungu alifunua fumbo la wokovu wa dunia hii kupitia kwa wachungaji baada ya Yesu Kristo kuzaliwa kwenye zizi la ng'ombe.

"Kwa kipimo cha ubinadamu hatuwezi kuelewa, kwa nini Mwenyezi Mungu muumba wa mali zote duniani, aruhusu mwana wake azaliwe kwenye pango na katika ufukara mkubwa. Lakini ukweli wa fumbo hili ni kwamba Yesu Kristo alizaliwa katika ufukara ili wokovu uanzie kwa watu maskini," alisema askofu Pengo.

Aliwakumbusha Wakristo kuwa maadhimisho ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo ni kudumisha amani. Alisema binadamu wanaamini kuwa anayeweza kuleta amani duniani ni matajiri na watawala ambao wanaishi kwenye majumba mazuri, jambo ambalo sio kweli.

"Historia inaonesha wenye maisha mazuri, matajiri na watawala wanatumia muda mwingi kwenye starehe na kuwasahau watu wengine na hivyo amani kushindwa kupatikana kupitia kwa matajiri hao.

"Tunapotafuta amani ya dunia, tusitegemee italetwa na matajiri ambao muda mwingi wanautumia kwenye ulevi au wale wenye mamlaka ya kutawala ulimwengu huu, bali italetwa na maskini watu ambao ni wa kawaida kama ilivyokuwa kwa Kristo na kama wale wachungaji walivyoupokea ujumbe wa amani kutoka kwa malaika," alisema Pengo.

Askofu huyo aliwataka watu ambao ni maskini wasije wakajiaminisha kuwa kwa kuwa wao ni maskini hawawezi kuleta amani.

"Usiseme mimi maskini sina uwezo wa kutawala, hivyo siwezi kuwa chimbuko la amani, mimi ni mtu maskini, jioni ya leo nakwambia kwamba unaweza kuleta amani kwa umaskini wako huo huo."

Kiongozi huyo wa dini alisema wapo maskini wengi katika dunia wanakuwa chimbuko la ukosefu wa amani kwa sababu wana hamu ya kuwa na utajiri kwa njia yoyote ile.

"Tunajua kwamba maskini ambaye anatamani kuwa tajiri ni hatari zaidi kuliko mwenye utajiri wa kuzaliwa nao."

Alitoa mwito kuwa ili kudumisha amani ya nchi, kila mmoja atekeleze wajibu wake kwa zamu, na inapokuwa zamu yako fanya kazi, mtu afanye kazi kama ilivyokuwa kwa wachungaji waliofanya kazi kwa kupokezana.

"Tumwombe Mwenyezi Mungu ambaye aliwatuma malaika wakapeleka habari njema kwa wale wachungaji, afikishe ujumbe huo kwetu kwetu pia, asiwepo mmoja kati yetu ambaye atasema mimi maskini siwezi kuwa chimbuko la amani.

"Kila mtu atekeleze wajibu wake kwa ukamilifu, anaweza kuwa chimbuko la amani katika eneo lake. Tunapoiombea dunia na taifa letu amani, sisi wenyewe tuwe wa kwanza kutekeleza wajibu wetu ili tuwe kielelezo cha chimbuko la amani," alisema Pengo.

Akitoa salamu za sikukuu ya Krismasi baada ya kumalizika misa ya Krismasi aliyoingoza katika Kanisa la Mtakatifu Maurusi lilipo Kurasini wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, Askofu Pengo mbali na kuwatakia siku kuu njema Watanzania wote, aliwaasa pia kuitunza amani ya Tanzania.

“Nawatakia kila mmoja baraka na neema katika siku hii ya kuzaliwa bwana wetu Yesu Kristo, lakini pia sote tulinde amani hii tuliyonayo hadi siku ya kuja kwake bwana wetu Yesu,” alisema Askofu Pengo.

Aidha aliwataka pia Wakristo wote kuishi maisha ambayo yanampendeza Mungu na pia kutokujiombea wao wenyewe pekee badala yake kuwaombea pia watu wengine.

ZeroDegree.
Kardinali Pengo atoa ya Moyoni. Kardinali Pengo atoa ya Moyoni. Reviewed by Zero Degree on 12/26/2016 02:36:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.