Loading...

Maofisa katika wizara ya Mambo ya Nje wapunguzwa.

WIZARA ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imesema imeanza kupunguza maofisa walioko katika balozi na kuweka wapya ili kupanua wigo wa uwakilishi na kubana matumizi.

Aidha, imesema kuwa baadhi ya maofisa wameshaanza kurudi na wengine wamesharipoti wizarani hapo kuendelea na majukumu mengine.

Hayo yalibainishwa juzi na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk Aziz Mlima wakati akizungumzia mambo mbalimbali yanayofanywa na wizara hiyo kwenye kipindi cha Tunatekeleza kinachorushwa na TBC 1.

Dk Mlima alisema kuwa ili kupanua wigo wa balozi katika kutangaza utalii nchini, waliamua kuwaondoa maofisa walioko kwenye balozi 35 na ofisi mbili za uwakilishi zilizopo nchi mbalimbali ili kupeleka watu wenye uwezo wa kutumia nafasi hiyo vyema.

“Tumeamua kubana matumizi hususani kupunguza mahitaji yasiyo ya lazima, ikiwemo watumishi. Tunaangalia mchango wa maofisa waliokuwepo kwenye balozi zetu kama anahitajika mmoja au la,’’ alisema Dk Mlima.

Alisema pia wanaangalia maofisa wenye weledi na uwezo kwa ofisa mmoja mwenye uwezo wa kufanya kazi za watu watatu au ni lazima wawepo wote watatu.

“Miongoni mwa majukumu ya balozi zetu ni pamoja na kutangaza fursa za utalii na vivutio vilivyopo nchini kwetu ili kuongeza watalii kutoka nje kuja hapa. Kwa hivyo, tumeona ni vyema kuwabadilisha waliokuwepo na kuweka watu wapya ambao watakuwa wachache wenye uwezo wa kufanya kazi hii kikamilifu,’’ aliongeza.

Aliongeza kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuongeza uwakilishi mzuri katika balozi hizo na kuboresha mazingira ya maofisa wao walioko nje kwa kutumia rasilimali chache zilizopo.

Kwa mujibu wa Dk Mlima, hivi sasa maofisa hawatapata uhamisho kwenda ubalozi fulani ilimradi kukidhi mahitaji bali watapewa wale wenye uwezo na ubora wa kuiwakilisha nchi katika masuala mbalimbali.

Alisisitiza kuwa azma hiyo ya kubana matumizi itasaidia kukarabati nyumba zaidi ya 100 zilizopo kwenye balozi hizo na kukamilisha mradi uliokuwepo Maputo Msumbiji. Dk Mlima alisema watapeleka watu wenye ushawishi wa kuleta watalii kwa wingi nchini kwani kwa kuwatumia maofisa hao wenye weledi.

Akitoa mfano alisema katika nchi zingine huwa na utaratibu na mikakati mbalimbali ya kutangaza utalii wao kwa kuanisha vivutio vya kitalii na makumbusho mbalimbali ambapo watalii wanavutiwa navyo. Vile vile, alieleza kuwa serikali ikiboresha sehemu hizo za utalii na kuzitangaza, idadi ya watalii itaongezeka kutoka milioni mbili kwa mwaka.

Alitoa mfano, katika awamu hii Rais John Magufuli ameweza kuleta ndege mbili na nyingine nne ambazo zimetajwa kuja baadaye, jambo ambalo litachangia ongezeko la utalii kwa kuwa watakuwa na uhakika wa usafiri.

‘’Tanzania ina vivutio vingi vya utalii lakini idadi ya watalii kwa mwaka ni milioni mbili tu. Tunaamini kwamba tutakapoboresha vivutio hivyo ikiwemo ujio wa ndege hizo utasaidia ukuaji wa utalii,’’ alifafanua.

Akizungumzia namna wanavyotafuta fursa nje ya nchi, Dk Mlima alisema wamekuwa wakitafuta wawekezaji na kuwaeleza fursa za uwekezaji zilizopo nchini na baada ya makubaliano, wamekuwa wakisaini mikataba hiyo yenye maslahi kwa taifa.

Alisema kuna baadhi ya mikataba inayokuja nchini yenye masharti magumu, hivyo Serikali huikataa na kukubali ile yenye maslahi mapana kwa wananchi wote ambapo watekelezaji wake wakuu ni sekta husika ikiwemo halmashauri.

“’Masuala yote ya kifedha ikiwemo mikopo kutoka Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB), Umoja wa Mataifa (UN) na mashirika mengine, sisi ndio tunashughulikia na baada ya kusaini mikataba tukakabidhi wizara husika kwa ajili ya utekelezaji wake,’’ alisema Katibu Mkuu huyo.

Hata hivyo, alisema mikataba mingi iliyoletwa wameiacha kwa kuwa inaweza kuleta matatizo kwa Taifa kutokana na masharti yake na kwamba hukaguliwa kwanza kuona kama haina mgongano.

Alisema, wanao wajibu wa kutoa taarifa sahihi kwa mwekezaji kuhusu mazingira halisi ya uwekezaji yaliyopo kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na wadau wengine.

ZeroDegree.
Maofisa katika wizara ya Mambo ya Nje wapunguzwa. Maofisa katika wizara ya Mambo ya Nje wapunguzwa. Reviewed by Zero Degree on 12/10/2016 12:24:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.