Loading...

Mkurugenzi Taasisi ya utafiti wa magonjwa ya binadamu atumbuliwa, ..Serikali yakanusha uwepo wa virusi vya ZIKA nchini.

Mkurugenzi wa Taasisi ya utafiti wa magonjwa ya binadamu nchini Tanzania (NIMR), Dkt Mwele Malecela, ambaye alitangaza kugunduliwa kwa virusi vya Zika nchini Tanzania, amefutwa kazi.

Taarifa kutoka kwa mkurugenzi wa mawasiliano ya ikulu Gerson Msigwa inasema Rais wa John Magufuli ametengua uteuzi wa mkurugenzi huyo mkuu.

Taarifa hiyo hata hivyo haijaeleza sababu ya kufutwa kazi kwa Dkt Malecela, siku moja tu baada yake kutangaza kwamba kuna virusi hiyo.

Hata hivyo, kulikuwa kumetokea habari za kukinzana kutoka kwake na wizara ya afya kuhusu kuwepo kwa virusi vya Zika nchini Tanzania.

Alitangaza kuwepo kwa virusi hivyo nchini Tanzania siku ya Alhamisi lakini Ijumaa, baada ya habari hizo kuenea kwenye vyombo vya habari, waziri wa afya Ummy Mwalimu akatoa taarifa kukanusha habari hizo.

"Uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa NIMR atakayejaza nafasi iliyoachwa na Dkt Mwele Malecela utatangazwa baadaye," taarifa hiyo inasema.

Dkt Mwele Malecela alikuwa ametangaza kwamba virusi hivyo vimepatikana mkoani Morogoro, Mashariki mwa Tanzania na Mkoani Geita, kaskazini magharibi mwa Tanzania.

Kwa mujibu wake, virusi hivyo viligunduliwa wakati wa utafiti uliofanyika kutokana na uhalisia kuwa kuna mazingira yanayowezesha kuzaliana kwa mbu wanaoeneza virusi hivyo.

Kati ya watu 533 waliopimwa wakati wa utafiti huo, asilimia 15.6 waligunduliwa kuwa na virusi vya Zika.

Hata hivyo wizara afya nchini humo, ilitoa taarifa ambapo inakanusha kuwepo kwa virusi hivyo.

"Kama nilivyoeleza mnamo Februari 2016, ugonjwa huu bado haujaingia nchini, na leo pia napenda kuwatoa hofu wananchi kuwa kwa sasa Tanzania haujathibitishwa kuwepo na ugonjwa wa Zika," taarifa ya wizara ya afya imesema.

Wizara hiyo inasema uchunguzi uliofanywa na NIMR ulikuwa wa kuchunguza ubora wa kipimo kipya cha kupima magonjwa ya Zika na Chikungunya.

"Matokeo haya bado yanahitaji kuchunguzwa kwa kina zaidi kupitia vipimo vilivyothibitishwa na Shirika la Afya Duniani," wizara ilisema.
Asili ya Zika

Jina la virusi hivyo linatokana na msitu wa Zika, Uganda ambapo virusi hivyo vilitambuliwa kwa mara ya kwanza 1947.

Wengi wa walioambukizwa aina ya awali ya virusi walikuwa wakipatwa na homa ambayo si kali sana, mwasho na maumivu katika maungio.

Lakini kwa aina ya sasa, ambayo mlipuko wake ulianza mwishoni mwa mwaka 2015 nchini Brazil, dalili zake zimekuwa kali na virusi hivyo vinaaminika kusababisha kudumaa kwa ubongo na kasoro nyingine mwilini.

Historia ya kuenea kwa virusi vya Zika

  • 1947: Wanasayansi wanaotafiti kuhusu homa ya manjano msitu wa Zika, Uganda wagundua virusi hivyo kwenye tumbili.
  • 1948: Virusi hivyo vyapatikana kutoka kwenye mbu aina ya Aedes africanus msitu wa Zika
  • 1952: Visa vya kwanza vya binadamu kuambukizwa virusi vya Zika vyaripotiwa Uganda na Tanzania
  • 1960-80: Virusi vya Zika vyapatikana kwenye mbu na tumbili maeneo ya kati Afrika
  • 1960-80: Virusi vya Zika vyapatikana maeneo yenye misitu na mvua nyingi Asia, ikiwemo India, Indonesia, Malaysia na Pakistan
  • 2007: Virusi vya Zika vyaenea nje ya Afrika na Asia, kwanza katika visiwa vya Yap kwenye bahari ya pasifiki
  • 2012: Watafiti wagundua aina mbili tofauti za virusi vya Zika, virusi vyenye asili Afrika na vingine vyenye asili Asia
  • Machi 2, 2015: Brazil yaripoti visa vya watu kuugua kutokana na maambukizi ya virusi vya Zika
  • Julai 17: Brazil yaripoti visa vya watoto kuzaliwa na ubongo uliodumaa na vichwa vidogo
  • Okt. 30: Visa vya watoto kuzaliwa an vichwa vidogo Brazil vyaongezeka
  • Novemba 2015-Januari 2016: Visa vya Zika vyaripotiwa Suriname, Panama, El Salvador,
  • Mexico, Guatemala, Paraguay, Venezuela, French Guiana, Martinique, Puerto Rico,
  • Guyana, Ecuador, Barbados, Bolivia, Jamhuri ya Dominika, Nicaragua, Curacao,
  • Na Jamaica
  • Feb. 2, 2016: Kisa cha kwanza cha Zika kuenezwa Marekani charipotiwa, kikidaiwa kutokana sana na ngono badala ya kuumbwa na mbu.
  • Mei 20: WHO yatangaza kupatikana kwa virusi vya Zika kwa mara ya kwanza Afrika kipindi cha sasa cha mlipuko, katika visiwa vya Cape Verde. Virusi hivyo ni vya aina sawa na virusi vilivyosababisha watoto kuzaliwa na vichwa vidogo Brazil.
  • Agosti 3, 2016: Wataalamu Marekani watangaza kuanza kwa majaribio ya chanjo dhidi ya Zika.
Credits: BBC Swahili
ZeroDegree.
Mkurugenzi Taasisi ya utafiti wa magonjwa ya binadamu atumbuliwa, ..Serikali yakanusha uwepo wa virusi vya ZIKA nchini. Mkurugenzi Taasisi ya utafiti wa magonjwa ya binadamu atumbuliwa, ..Serikali yakanusha uwepo wa virusi vya ZIKA nchini. Reviewed by Zero Degree on 12/17/2016 09:57:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.