Loading...

Mzee wa baraza ahukumiwa kwenda jela miaka 3 kwa kupokea rushwa.

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Pwani iliyoko Kibaha, imemhukumu kifungo cha miaka mitatu jela mzee wa baraza, Francis Isaya (64).

Mzee huyo wa baraza alihukumiwa kifungo hicho baada ya kupatikana na hatia ya kupokea rushwa ya Sh. 100,000 kutoka kwa mume wa mshtakiwa, ili kumsaidia katika kesi.

Mshtakiwa huyo alitakiwa ama kulipa faini ya Sh. 500,000 au kwenda jela kutumikia kifungo hicho lakini alishindwa kulipa hivyo kwenda kuanza maisha mapya gerezani.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Hariet Mwailolo alisema mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa walalamikaji na kumwona mshtakiwa kuwa na hatia.

Hakimu Mwailolo alisema kutokana na mahakama kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka pamoja na mlalamikaji, mahakama inampa mshtakiwa adhabu ya kulipa faini au kwenda jela ili iwe fundisho kwake au kwa watu wengine waliozoea kuomba rushwa.

Awali, mwendesha mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Pwani, Sabrina Weston, alidai mahakamani kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Novemba, mwaka huu.

Alidai kuwa Isaya alimshawishi Omary Hiza ampe kiasi hicho cha fedha ili amsaidie mkewe Mariam Hussein ambaye alikuwa akikabiliwa na kesi ya jinai ya shambulio la kudhuru mwili.

Weston alidai kuwa baada ya mshtakiwa kuomba rushwa hiyo, ndipo walipoweka mitego na kufanikiwa kumkamata akichukua fedha hizo.

Kabla mahakama haijampa mshtakiwa adhabu hiyo, alitakiwa kujitetea pamoja na kuishawishi mahakama kumpunguzia adhabu lakini hakusema chochote.

ZeroDegree.
Mzee wa baraza ahukumiwa kwenda jela miaka 3 kwa kupokea rushwa. Mzee wa baraza ahukumiwa kwenda jela miaka 3 kwa kupokea rushwa. Reviewed by Zero Degree on 12/17/2016 10:22:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.