Loading...

Sikukuu ya Krismasi kitaifa mwaka huu 2016 kufanyikia Bukoba.

IBADA ya sikukuu ya Krismasi kitaifa mwaka huu, inafanyika wilayani Bukoba mkoani Kagera. Inafanyika huko ikiwa ni njia ya kuwafariji wananchi wa mkoa huo, kutokana na maafa ya tetemeko yaliyowakumba na kusababisha vifo vya watu zaidi ya watu 18 na uharibifu wa mali na mazingira.

Akizungumza kwa njia ya simu Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Mchungaji John Kamoyo, alisema pamoja na kusherehekea sikukuu ya Kuzaliwa kwa Mwana wa Mungu, Yesu Kristo, ibada hiyo pia itakuwa ni daraja kwa wakazi wa mkoa huo kutokana na matatizo yaliyowapata.

“Unajua wenzetu hawa hivi karibuni walikumbwa na tukio kubwa lililowasababishia maafa la tetemeko, sasa tumeona twende Bukoba tusherehekee nao katika ibada hii na kuwafariji,” amesisitiza Mchungaji Kamoyo.

Alisema kwa mujibu wa ratiba ya ibada hiyo ya Krismasi, mkesha wa kuamkia siku ya Krismasi yaani Desemba 24 kuamkia Desemba 25 mwaka huu, itafanywa na Kanisa Katoliki Tanzania (TEC).

Alisema ibada hiyo ya mkesha wa Krismasi ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo miaka zaidi ya 2000 iliyopita, itafanyikia katika Kanisa Kuu la Bikira Maria. Alifafanua kuwa ibada ya siku ya Krismasi itafanywa na CCT katika Kanisa Kuu la Mwokozi (KKKT Bukoba) maarufu kengele tatu.

Akitoa salamu za sikukuu hiyo, Mchungaji Kamoyo alisema siku hiyo inaposherehekewa ili kukumbuka kuzaliwa kwa mwokozi Yesu Kristo, aliyewatendea upendo na mambo mema watu duniani kote.

“Watanzania naomba tuikumbuke siku hii kwa kudumisha upendo, tuitumie siku ya Krismasi kuunganisha watu na kujenga umoja. Lakini kubwa zaidi tuwasaidie wale wenye mahitaji na tuwatembelee wagonjwa hospitalini na kuwafariji,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Method Kilaini, alisema wananchi wa Bukoba wamefarijika kutokana na uamuzi wa kuifanyia ibada ya Krismasi kitaifa mkoani humo. Alisema tayari maandalizi ya kufanyika kwa ibada hiyo yanaendelea vizuri.

“Ibada inakuja Bukoba, ni kweli wananchi hawa walihitaji kufarijiwa na kuzaliwa upya kutokana na kilichowapata. Tetemeko lile liliwaumiza na kuwajengea simanzi sasa wanahitaji furaha,” alisema.

Kuhusu kauli yake kwa watanzania katika kusherehea sikukuu hiyo, Askofu Kilaini, alisema siku hiyo Kristo anazaliwa, hivyo watanzania wanahitaji kuwa watu wapya kwa kubadili matendo yao na kuwa tayari kushikamana na kuwa kitu kimoja.

Septemba 10, mwaka huu mkoani Kagera kulitokea tetemeko lenye ukubwa wa Ritcher 5.7 na kusababisha vifo vya watu 18 ikiwemo majeruhi 252, ambapo nyumba za makazi zilizoanguka ni 840 na nyumba zilizopata nyufa 1,264.

ZeroDegree.
Sikukuu ya Krismasi kitaifa mwaka huu 2016 kufanyikia Bukoba. Sikukuu ya Krismasi kitaifa mwaka huu 2016 kufanyikia Bukoba. Reviewed by Zero Degree on 12/21/2016 01:00:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.