Loading...

Tambwe awashtua viongozi wa Klabu ya Yanga.

MSHAMBULIAJI wa Yanga raia wa Burundi, Amisi Tambwe, amewashtua viongozi wa klabu hiyo ambao wanaonekana hawana mpya wa kumwongezea mkataba wa kuendelea kukipiga katika kikosi hicho.

Tambwe alitemwa na Simba katika msimu wa usajili wa dirisha dogo la 2014 la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na kujiunga na Yanga, sasa amebakisha miezi minne kuitumikia klabu hiyo.

Pamoja na kubakisha muda huo, viongozi wa Yanga hawajaonyesha nia ya kumwongezea mkataba mwingine mshambuliaji huyo aliyetokea klabu ya Vital’ ya Burundi kabla ya kutua Simba na baadaye Jangwani.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Tambwe alisema mpaka sasa hajafanya mazungumzo na viongozi wake kuhusu kumwongezea mkataba mwingine ili aweze kuitumikia klabu hiyo.

Tambwe alisema kwa sasa amebakisha miezi minne kumaliza mkataba wa kuichezea Yanga na anaweza kufanya mazungumzo na klabu yoyote itakayohitaji huduma yake.

“Bado sijafanya mazungumzo na viongozi wa kamati ya usajili, mkataba wangu unaisha Aprili mwakani,” alisema Tambwe.

Katika hatua nyingine, Tambwe alisema wanaendelea kujipanga kufanya vizuri zaidi msimu huu kutokana na vitu adimu anavyopewa na kocha mpya wa timu hiyo, Mzambia Goerge Lwandamina, katika mazoezi yanayoendelea kwenye Uwanja wa Gymkhana jijini Dar es Salaam, kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara.

Tambwe amekuwa akipata mbinu mpya ya kucheza soka baada ya kocha Hans van der Pluijm kupewa majukumu ya ukurugenzi ndani ya klabu hiyo.

Mshambuliaji huyo amekuwa mfungaji bora katika misimu miwili tofauti Ligi Kuu Bara, alifunga mabao 19 katika msimu wake wa kwanza akiwa na Simba na msimu uliopita alifunga mabao 21 Yanga.

Source: Bingwa
ZeroDegree.
Tambwe awashtua viongozi wa Klabu ya Yanga. Tambwe awashtua viongozi wa Klabu ya Yanga. Reviewed by Zero Degree on 12/05/2016 06:00:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.