Loading...

TANZIA: Aliyekuwa Mbunge wa Rufiji, Profesa Idris Mtulia afariki dunia.

ALIYEWAHI kuwa Mbunge wa Rufiji mkoani Pwani na Katibu Mkuu wa wizara kadhaa nchini, Profesa Idris Mtulia (73) amefariki dunia.

Profesa Mtulia ameaga dunia jana asubuhi nyumbani kwake Upanga jijini Dar es Salaam akiwa usingizini.

Kwa mujibu wa shemeji wa marehemu, Selemani Marijani, Profesa Mtulia alifariki dunia saa tano kasorobo asubuhi baada ya kujipumzisha kwa muda baada ya kuswali swala ya alfajiri na kisha kusoma magazeti na kuangalia taarifa ya habari kwenye televisheni.

Marijani alieleza kuwa mbunge huyo wa Rufiji kuanzia mwaka 2005 hadi 2010, hakuwa na tatizo lolote la afya na mwishoni mwa wiki, alishiriki katika sherehe za binti yake, Salma kuhitimu katika Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya Muhimbili (MUHAS) na baadaye kumfanyia tafrija ndogo.

“Mzee hakuwa na matatizo ya afya na usiku wa Jumamosi alishiriki katika tafrija ya binti yake wa mwisho kutokana na kuhitimu masomo katika chuo cha udaktari cha Muhimbili. Leo (jana) pia aliamka vizuri, akaswali, akaangalia taarifa ya habari na kusoma magazeti kama kawaida yake na kisha kupumzika, ndio hakuamka tena,” alieleza shemeji yake huyo.

Alisema Profesa Mtulia ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa wizara za Afya na Maji, pamoja na kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Bohari Kuu ya Dawa (MSD) atazikwa leo saa saba mchana kwenye makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam na maiti yake itaswaliwa kwenye msikiti wa Shandhily jijini humo.

Kwa mujibu wa shemeji huyo, Profesa Mtulia ameacha mjane, Rehema Abdallah na watoto sita, Khadija, Dk Ali, Nuru, Yussuf, Abdallah na Dk Salma.

Mbunge wa zamani wa Rufiji na aliyewahi kuwa Waziri wa Afya na Maendeleo ya Jamii, Dk Seif Rashid alisema amepokea kwa masikitiko kifo cha Profesa Mtulia kwa kuwa kwake alikuwa mwalimu, kiongozi na mlezi.

“Ni mshituko mkubwa maana ni kifo cha ghafla, ni mzee wetu, mwalimu wetu, amefundisha pake UDSM (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam) amekuwa Muhimbili (Hospitali ya Taifa) Idara ya Moyo, amekuwa Mbunge wa Rufiji. Nilipokea ubunge kutoka kwake na pia Mwenyekiti wa Bodi ya MSD (Bohari ya Dawa), kweli ni huzuni mno," alisema.

Alisema amefanya naye kazi katika serikali na kwenye siasa na kwamba alipopokea tasrifa za kifo chake saa tisa alasiri jana, alishtuka.

Profesa Mtulia pia alikuwa akifanya kazi katika Hospitali ya Tumaini ya jijini Dar es Salaam na jana alikuwa na miadi ya kuwatibu baadhi ya wagonjwa hospitalini hapo. Profesa Mtulia alikuwa pia daktari wa Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi.

Alikuwa Mbunge wa Rufiji tangu mwaka 2005 hadi 2010. Pia aliwahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kuanzia mwaka 2002 hadi 2007.

ZeroDegree.
TANZIA: Aliyekuwa Mbunge wa Rufiji, Profesa Idris Mtulia afariki dunia. TANZIA: Aliyekuwa Mbunge wa Rufiji, Profesa Idris Mtulia afariki dunia. Reviewed by Zero Degree on 12/06/2016 10:04:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.