Loading...

UNYAMAA: Mwanafunzi auawa na watu wasiojulikana na kisha kuchunwa ngozi.

MAUAJI ya watu kwa kuchunwa ngozi yaliyovuma Wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe miaka ya 2000, sasa yameanza kujitokeza wilayani Karatu, baada ya mwanafunzi wa Shule ya Msingi Sumawe, kuuawa kwa staili hiyo kisha mwili wake kutupwa shambani kwa baba yake.

Wazazi wa mtoto huyo, Andrea Paulo na Paulina Petro, walisema mtoto wao, Witness Andrea (9), alipotea katika mazingira ya kutatanisha Desemba 5, mwaka huu, wakati akichunga ng'ombe porini. 

Paulo alisema tangu alipopotea walimtafuta maeneo mbalimbali bila mafanikio hadi walipokuta maiti yake juzi majira ya 10 jioni.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kiwandani, kilichoko kijiji cha Tloma, Alexander Lulu, alisema mtoto alipatikana Jumatano wiki hii akiwa amefariki dunia huku mwili wake ukiwa umechunwa kuanzia kifuani sehemu za mbele na kukatwa mkono wake wa kushoto.

Alisema mwili wa mtoto huyo ulikutwa umetupwa katika shamba moja jirani na nyumbani kwao.

Alisema polisi baada ya kupata taarifa, walikwenda kuuchukua mwili na kuupeleka katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Karatu kwa uchunguzi. 

Mtoto huyo alipotea katika mazingira ya kutatanisha alipokuwa akichunga ng’ombe. Baada ya kuuawa, kuchunwa ngozi na kukatwa mkono, mwili wake ulitupwa shambani kwa baba yake.

Baba mazazi alishangazwa kuonekana kwa mwili wa mwanawe katika shamba lake huku awali wakiwa wamepita hapo wakati wakimtafuta lakini hawakumkuta. Alisema huenda mwanawe aliuawa eneo lingine na mwili wake kutupwa shambani mwake.

Tukio hilo la aina yake limetokea umbali wa mwendo wa nusu saa kwa miguu kutoka katikati ya mji wa Karatu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Theresia Mahongo, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Karatu, alisema alikuwa anafuatilia suala hilo.

Hata hivyo, Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) ya Karatu, John Hadu, alisema amepata taarifa hizo na kwamba mwili wa marehemu ulipelekwa hospitalini kwa uchunguzi zaidi.

Alisema uchunguzi wa mauaji hayo ya kwanza ya aina yake wilayani hapa unaendelea.

ZeroDegree.
UNYAMAA: Mwanafunzi auawa na watu wasiojulikana na kisha kuchunwa ngozi. UNYAMAA: Mwanafunzi auawa na watu wasiojulikana na kisha kuchunwa ngozi. Reviewed by Zero Degree on 12/09/2016 11:00:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.