Loading...

Upinzani wamtaka Mkapa ang'oke katika mazungumzo ya kusaka amani nchini Burundi.

ULore Makundi ya upinzani nchini Burundi yamemtaka mpatanishi wa kimataifa katika mgogoro wa nchi hiyo, Benjamin Mkapa ajiuzulu ikiwa ni siku kadhaa zimepita tangu awasili nchini humo.

Wito huo umezusha hali ya wasiwasi wa kufanikiwa juhudi zinazosuasua za kutatua mgogoro wa kisiasa unaoendelea kwa miezi kadhaa sasa katika nchi hiyo.

Mkapa aliwasili nchini Burundi Ijumaa iliyopita akiongoza ujumbe wa upatanishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambapo akiwa katika Uwanja wa Ndege wa Bujumbura alitoa matamshi ambayo makundi yanayoipinga Serikali yanasema yanaashiria kuipa uhalali wa kisheria Serikali ya Rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza, suala ambalo ni kiini cha mgogoro uliopo.

Muungano wa upinzani wa CNARED umemwandikia barua rais huyo mstaafu wa Tanzania kumtaka aondoke.

Sehemu moja ya barua hiyo imeeleza kuwa: “CNARED haikutambui tena wewe kama mpatanishi katika mgogoro wa ndani wa Burundi”.

Alipozungumza na waandishi wa habari katika uwanja wa ndege wa Bujumbura, Mkapa alisema kipaumbele chake ni kuhakikisha uchaguzi ujao wa rais wa mwaka 2020 unakuwa huru na wa haki.

“Ni watu wa Burundi ndio waliompa uhalali wa kisheria rais wa Burundi... wale wanaodhani mimi ndiye ninayetoa uhalali wa kisheria hawajifahamu hata kidogo,” alisema mpatanishi huyo wa EAC.

Burundi imekumbwa na mgogoro wa kisiasa na machafuko ya umwagaji damu kwa muda wa takriban miaka miwili sasa uliochochewa na uamuzi wa Rais Nkurunziza kugombea urais kwa muhula wa tatu na kuibuka mshindi katika uchaguzi uliofanyika Julai, 2015, hatua ambayo ilizidisha mgogoro huo.

Mgogoro huo umesababisha mamia ya raia kukimbilia nchi za jirani huku wengi wao wakiripotiwa kuingia nchini Tanzania na Rwanda.

Hali ya usalama nchini humo imekuwa ya kutilia mashaka kutokana na kuendelea kuzuka kwa matukio ya kihalifu.

Hivi karibuni mmoja wa wasaidizi wa Rais Nkurunziza alinusurika katika jaribio la mauwaji. Serikali ilisema itaendesha msako nchini kote kwa ajili ya kuwasaka wale iliowaita wasaliti wa taifa.

Credits: Mwananchi 
ZeroDegree.
Upinzani wamtaka Mkapa ang'oke katika mazungumzo ya kusaka amani nchini Burundi. Upinzani wamtaka Mkapa ang'oke katika mazungumzo ya kusaka amani nchini Burundi. Reviewed by Zero Degree on 12/15/2016 06:44:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.