Loading...

Wanachama Simba waridhia mabadiliko ya Katiba.

Ni wazi mabadiliko ndani ya klabu ya Simba hayana tena mjadala. Jana, wanachama wa klabu hiyo kwa kauli moja waliyabariki kwa mfumo wa kubadili vipengele vya katiba ya klabu hiyo.


Wanachama hao waliridhia mabadiliko ya ibara ya 49 ya katiba ambayo awali haikuonyesha mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo bali ilielezea kuvunja ama kufutwa kwa klabu hiyo.

Wanachama 642 waliohudhuria mkutano huo wa dharura uliofanyika kwenye Ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi, Oysterbay jijini Dar es Salaam, asilimia 98 walipiga kura ya kupitisha marekebisho ya Ibara hiyo na vipengele vyake vitatu. Hata hivyo, wanachama hao walishauri marekebisho hayo yaandaliwe kitaalamu na kamati ya utendaji, yarudishwe kwao ili yajadiliwe kwenye mkutano mkuu ujao mwakani.

Katibu mkuu wa zamani wa klabu hiyo, ambaye ndiye mwanasheria wao, Evodius Mtalawa alifafanua kipengele kimoja baada ya kingine ili wanachama wayaelewe mabadiliko hayo ya mfumo wa uendeshaji na baadaye waliyapigia kura.

Rais wa klabu hiyo, Evans Aveva aliyefungua mkutano huo saa 6:00 mchana aliwaeleza wanachama kuwa hiyo ni hatua ya kwanza kuelekea kwenye mabadiliko hayo na ili yakamilike ni lazima zifuatwe taratibu zote.

“Waambieni walioshindwa kufika hapa kwani naamini mtakuwa mmeelewa nini tunakusudia, hii ni hatua ya kwanza, tukienda kukutana na kamati ya utendaji tutakavyoandaa itabidi tuwarudishie kama mlivyopendekeza, baadaye tupeleke TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) wapitie na kisha msajili wa michezo ili iwe katiba halali.

Ibara 49 (i) ilisomeka; Uamuzi wowote wa kuvunja au kufutwa kwa klabu ya Simba unahitaji theluthi mbili ya wanachama (wote wa Simba) waliopataikana katika mkutano mkuu ulioitishwa maalumu kwa madhumuni hayo.

Baada ya mabadiliko hayo, kifungu hicho kinasomeka; Uamuzi wowote wa kubadilisha mfumo, kuvunja au kufutwa kwa klabu ya Simba unahitaji theluthi mbili za wanachama waliopatikana kwenye mkutano.

Kipengele kingine kilichofanyiwa marekebisho ni (iii); awali kilisomeka; kuwapo na sababu za kuvunja au kufutwa kwa klabu kama vile kuwa na madeni makubwa yasiyolipika, kupoteza hadhi ya kutoaminika na kukopesheka pia kimefanyiwa marekebisho.

Kwa sasa kifungu hicho kitakuwa; kuwapo kwa sababu za kubadilisha mfumo, kuvunja ama kufutwa kwa klabu ya Simba kama vile kuwa na madeni makubwa, kupoteza hadhi ya kutoaminika au kuendana na matakwa ya mfumo wa nyakati, iwe kibiashara ama kimichezo.

Marekebisho hayo yameongeza kipengele cha (iv) (a), kinachoeleza; mkutano mkuu wa wanachama unaweza kuitishwa kwa mujibu wa Ibara ya 22 na kufanya mabadiliko ya mfumo wa umiliki au uendeshaji wa Simba.

(b) Mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji au umiliki wa Simba hayataathiri hadhi ya wanachama wote halali, isipokuwa hadhi hiyo itabadilika kuendana na mfumo stahiki wa mabadiliko yaliyofanyika.

Uwiano wa thamani ya umiliki wa kila mwanachama katika mfumo mpya utajadiliwa na kamati ya utendaji na kuwasilishwa katika mkutano mkuu kwa ajili ya kupitishwa. (c) Mfumo mpya wa mabadiliko ya uendeshaji au umiliki wa Simba utarithi hali na mali zote pamoja na madeni kwa wajibu wowote uliokuwa chini ya Simba pamoja mabadiliko hayo yatamaanisha kuacha kutumia katiba ya sasa na kutengenezwa mpya kwa utaratibu wa haki ya kupiga kura za mfumo huo mpya.

ZeroDegree.
Wanachama Simba waridhia mabadiliko ya Katiba. Wanachama Simba waridhia mabadiliko ya Katiba. Reviewed by Zero Degree on 12/12/2016 02:08:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.