Loading...

Waziri mkuu, Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi mweka hazina Bahi.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi aliyekuwa Mweka Hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Issai Mbilu ambaye kwa sasa amehamishiwa Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma.

Ameagiza arudishwe haraka, kujibu tuhuma za ubadhilifu Sh milioni 642.4 za miradi zinazomkabili.

“Tunaendelea kudhibiti na kuweka nidhamu ndani ya serikali. Ukiharibu Longido usitegemee kuhamishiwa wilaya nyingine, tunamalizana hapa hapa. Hatuwezi kuhamisha ugonjwa hapa na kuupeleka wilaya nyingine, hivyo Mwekahazina huyu arudishwe haraka Longido,” alisisitiza.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo, akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Arusha.

Pia alimwagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega kumuandikia barua Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), akimuomba amrudishe Mwekahazina huyo katika kituo chake cha kazi cha zamani ili aweze kujibu tuhuma zinazomkabili.

Alisema Serikali haitamvumilia mtumishi wa idara yoyote atakayeharibu jambo, halafu kuhamishwa sehemu nyingine.

“Hivyo naagiza kuanzia sasa nimemsimamisha kazi Mwekahazina huyu na arudi hapa kujibu kwanini ameleta hasara ya hizi fedha. Na nyie watumishi wengine hili liwe funzo kwenu,” alisema.

Alisema miradi mingi ya maendeleo, inakwama kwa sababu ya baadhi ya watumishi kuweka mbele maslahi binafsi, badala ya kuzingatia maadili ya utumishi. Hivyo, aliwaagiza wakuu wa idara, wafuatilie kwa makini miradi inayotekelezwa katika maeneo yao, kama inalingana na thamani halisi ya fedha zilizotolewa.

Akizungumzia kuhusu kushamiri kwa biashara haramu ya dawa za kulevya wilayani Longido, Waziri Mkuu aliwaagiza wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya, kufanya msako wa nyumba hadi nyumba na kuwakamata wote watakaokutwa wanafanya biashara hiyo.

“Wilaya hii ina sifa mbaya ya kuwa kitovu cha kusafirisha dawa ya kulevya zikiwemo bangi na mirungi. Hivyo nawaagiza wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama waendeshe msako kwa kila nyumba na atakayekamatwa achukuliwe hatua. Dawa za kulevya zinadhohofisha nguvu kazi ya Taifa. “Ukivuta bangi unapishana na kauli mbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’ kwani unakwenda kulala jambo ambalo hatuwezi kulikubali. Watakaokutwa wanauza au kununua mirungi na bangi wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa pamoja na kutaifisha magari yanayotumika kubeba bidhaa hiyo haramu,” alisema.

Awali, Mkuu wa Wilaya hiyo, Daniel Chongolo akisoma taarifa ya wilaya, alisema Longido inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo kutumika kama njia kuu ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi na mirungi kwenda nchi jirani ya Kenya, ambako biashara hiyo imehalalishwa.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema Serikali ipo mbioni kujenga kiwanda cha kuchakata madini ya magadi soda ili yawe na ubora na thamani kubwa. Alitoa kauli hiyo, aliposimamishwa na wananchi katika kijiji cha Loonolwo kilichopo Kata ya Gelai Merugoi Wilayani Longido akitokea wilayani Ngorongoro.

Alisema lengo la kujenga kiwanda hicho ni kuwawezesha wananchi wa wilaya hiyo hasa akinamama wanaoishi karibu na Ziwa Natron, linalotoa magadi hayo, waweze kunufaika na uwepo wa ziwa hilo.

Waziri Mkuu alisema ujenzi wa kiwanda hicho, utawezesha vijana na akinamama hao wanaouza magadi maeneo ya pembezoni mwa barabara katika Ziwa Natron, kupata ajira kwa kuwa kitazalisha ajira zaidi ya 500 katika wilaya hizo mbili za Longido na Ngorongoro.

Pia alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kushirikiana na wataalam wake, kufanya tathimini ya uhaba wa chakula katika Wilaya za Longido na Ngorongoro ili serikali ijue Mkoa wa Arusha una ukosefu wa chakula kwa kiasi gani.

Awali, wananchi hao waliokuwa na mabango mbalimbali, walilalamikia kero ya mipaka ya ardhi kati ya vijiji vya wilaya za Longido na Ngorongoro, ambapo Waziri Mkuu alimuagiza Ofisa Ardhi Mkoa wa Arusha, Hamdoun Mansour kwenda katika vijiji hivyo vya mpakani na kukutana na viongozi wa kimila ili kumaliza mgogoro huo.

ZeroDegree.
Waziri mkuu, Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi mweka hazina Bahi. Waziri mkuu, Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi mweka hazina Bahi. Reviewed by Zero Degree on 12/17/2016 09:43:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.