Loading...

Angban, Ndusha waachana na Simba kwa amani.

Kipa muivory Coast wa Simba, Vincent Angban.
KIPA Muivory Coast wa Simba, Vincent Angban anatarajiwa kuondoka nchini leo kurejea kwao, baada ya kumalizana na klabu ya Simba.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Angban alisema baada ya kumalizana na Simba ataondoka leo kurejea kwao.

“Natarajia kuondoka Jumapili [leo]baada ya kukutana na uongozi wa Simba na kukamilishiana malipo. Nawashukuru wapenzi wote wa Simba kwa sapoti yao kwangu kwa kipindi chote, maisha yanaendelea,”alisema.

Simba ilimuacha Angban na kiungo Mussa Ndusha kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika dirisha dogo Desemba mwaka jana ili kupata nafasi ya kumsajili Wathana, Kipa Daniel Agyei na kiungo James Kotei.

Lakini haikuwapa haki zao kwa wakati wachezaji hao hadi ilipofanya hivyo juzi – na sasa wote wanaondoka kurejea kwao kuendelea na maisha mengine.

Kipa huyo aliibukia katika klabu ya Vijana ya Rio Sport d'Anyama kabla ya kupandishwa kikosi cha kwanza mwaka 2005, ambako hata hivyo miaka miwili baadaye aliondoka na kwenda kujiunga na Sawe Sports msimu wa 2006/2007.

Mwaka 2007, Angban akajiunga na ASEC Mimosas ambako alikuwa kipa wa kwanza hadi mwanzoni mwa msimu wa 2009 alipoumia na nafasi yake kuchukuliwa na Daniel Yeboah.

Yeboah akawavutia zaidi makocha wa timu hiyo kwa ubora wake wa kuokoa michomo na akaendelea kudaka hata Angban alipopona.

Baada ya kumaliza mkataba wake ASEC, Angban akarejea Jeunesse na baadaye akaenda London kudakia U-21 ya Chelsea.

Amewahi kudakia timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya Ivory Coast katika michuano ya Afrika nchini Benin mwaka 2005 na aliiwakilisha pia nchi yake katika Michezo ya Olimpiki mwaka 2008.

Amedakia pia timu ya taifa ya wakubwa ya Ivory Coast ‘Tembo’ katika michuano ya CHAN ikiwamo ile ya mwaka 2009 na ndiye aliyesimama langoni katika mechi dhidi ya Tanzania, Taifa Stars ikishinda 1-0 bao pekee la Mrisho Ngassa.

Source: Nipashe
ZeroDegree.
Angban, Ndusha waachana na Simba kwa amani. Angban, Ndusha waachana na Simba kwa amani. Reviewed by Zero Degree on 1/01/2017 01:48:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.