Loading...

Baraza la vyama vya siasa latoa siku 21 zuio la maandamano na mikutano ya nje

MWENYEKITI wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, John Shibuda.
Shibuda amesema ndani ya siku 21 kuanzia jana, anatarajia kuweka hadharani visababishi na vichokonozi vilivyosababisha Rais John Magufuli kuzuia maandamano na mikutano ya nje ya vyama vya siasa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Shibuda alisema baada ya kufanya uchunguzi wa awali kuhusu zuio hilo, wamebaini zipo sababu ambazo zilichangia kuchukuliwa kwa hatua hiyo na kwamba tayari wameanza kuvifanyia kazi.

Alisema visababishi hivyo vya kuzuia mikutano ya vyama vya siasa vilitokana kukolezwa na vitendo hasi vya wadau wa siasa na makundi ya wanasiasa wenyewe ambao baada ya kuingia kwa serikali ya awamu ya tano walianza kuchokonoa na hivyo kusababisha Rais kufikia uamuzi huo.

“Viambishi vya awamu ya tano ni miito ya mageuzi kutoka katika mazoea chakavu ya fikra zilizosinyaa za kutokana na mawazo mnyauko, hivyo tukubali kitendawili cha zuio kilikolezwa na vitendo hasi vya sisi wadau wa siasa,” alisema.

“Mchakato unaendelea na nasema kwamba ndani ya siku 21 nitakuwa na ‘press conference’ (mikutano na waandishi wa habari) itakayopambanua dira timilifu ya safari ya kukunjua na kutanzua yale yaliyokuwa visababishi, hivi sasa niko katika unyumbulishaji, na katika siku hizo nitatoa nini maana ya amurisho ya dola,” alisema Shibuda.

Alisema siasa huru kwa sasa nchini zimeathiriwa na makundi ya siasa za wanasiasa wa maono na mitazamo tasa ya madaraja ya sifa tofauti za maana ya uhuru wa maoni.

“Haya makundi–siasa yalitumia dhana ya uhuru wa maoni na wa kuwa na ufahamu dhoofu wa umiliki welevu wa mitazamo hasi ya kuongozwa na maono ya maslahi binafsi, wakazua jambo na jambo likawa jambo.

Kundi hili ndilo lilichokonoa na kutia kitanzi uhuru wa uishi wa uhai huru wa haki mtambuka za vyama vya siasa, tukubali kwamba mficha maradhi huumbuliwa na kifo,” Shibuda alisema.

“Kwa hiyo, sasa kurejesha uthabiti wa uhuru wa kazi ya vyama vyote vya siasa ndani ya umma, linahitaji patendeke hali na sababu za kujenga mapinduzi ya kutoka katika mazoea potofu ya utamaduni wa mila na jadi ovu za kuotesha maamrisho gandamizi kwa vyama vyote vya siasa.”

Alisema ni vema ikakumbukwa kwamba wakati wanasiasa wanafikiria kuhusu zuio la mikutano kwa vyama hivyo, pia wanapaswa kufahamu wao ndio walisababisha kufikiwa kwa uamuzi wa kuzuia mikutano hiyo.

“Ifahamike kwamba watu wastaarabu hawachokozeki, lakini ukiwachokoza hawakubali kuchokonoleka, kwa hiyo tunapojifikirisha kuhusu kitendawili cha kutokomeza mkazo wa zuio, tukumbuke kwamba palizuka kauli za utaalamu hasi wa kuichokonoa serikali, na serikali nayo ikajibu kwa somo maalum kwamba ‘ukichokonoa mzinga wa nyuki lazima nyuki wakung`ate kwa hiyo tujifunze kwamba mlina asali haendi na shari kwenye mzinga wa nyuki,” alisema zaidi Shibuda.

Mwanasiasa huyo mzoefu aliendelea kueleza kuwa katika uongozi wake anaamini kwamba pale mtu anapofanya vizuri ni vema akapongezwa na anaamini hata vyama vya siasa hususani vya upinzani vitafanya hivyo kwa kuipongeza serikali pale inapofanya vizuri.

Shibuda pia alimpongeza Rais Magufuli kwa kurejesha uwajibikaji kwa watumishi akida kuwa kwa sasa wafanyakazi wa kila sekta wanafanya kazi kwa uadilifu na kujitahidi kutoa huduma bora kwa wananchi tofauti na ilivyokuwa awali.

Source: Nipashe
ZeroDegree.
Baraza la vyama vya siasa latoa siku 21 zuio la maandamano na mikutano ya nje Baraza la vyama vya siasa latoa siku 21 zuio la maandamano na mikutano ya nje Reviewed by Zero Degree on 1/30/2017 11:13:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.