Loading...

Walichosimulia waliofukiwa na kifusi mgodini kwa muda wa siku 3

MMOJA wa wachimbaji 15 ambao jana waliokolewa wakiwa hai kutoka katika mgodi wa dhahabu wa Kampuni ya RZ Union Mining Ltd uliopo Kata ya Nyarugusu wilayani Geita Mkoa wa Geita, amesimulia walivyoishi ndani ya mgodi huo kwa siku tatu, wakitegemea zaidi kunywa maji yaliyokuwa yakitiririka kutoka kwenye miamba.

Wachimbaji hao 15, mmoja akiwa raia wa China, waliokolewa wakiwa salama jana asubuhi na kukimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Geita ambako wanapatiwa matibabu, baada ya kufukiwa usiku wa kuamkia Januari 26, mwaka huu.

Aidha, imefahamika kuwa pamoja na kuwa na vifaa vya uokoaji vya kutosha ilichukua siku tatu kuwatoa kutokana na tahadhari kubwa waliyochukua waokoaji.

Mmoja ya wachimbaji hao 15 waliookolewa, Dickson Morris akisimulia alisema waliishi siku zote wakinywa maji yaliyokuwa yakitiririka kutoka kwenye miamba.

Alisema walitulia kwenye shimo hilo, na siku ya pili waliamua kupanda juu kuangalia kama kuna uwezekano wa kutoka, wakasikia mlio wa kitu kutoka juu wakaamini kuna watu wanatafuta njia ya kuwapa msaada. “Tuliposikia mlio huo tukakubaliana turudi chini isije kutuua.

Jumamosi tukaona bomba limeleta maji na ujumbe kutuuliza tuko salama, na sisi tukajibu tuko salama tukashukuru Mungu tutaokolewa,” alieleza mchimbaji huyo akizungumza na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1).

Kijana huyo alisema baadaye waliendelea kuletewa maji, biskuti na uji, jambo ambalo liliwapa faraja kwamba watapata msaada wa kuokolewa, na hilo likatimia jana asubuhi.

Akizungumza kwa njia ya simu jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo akielezea uokoaji ulivyofanyika, alisema ilibidi kuwa na umakini mkubwa ili kuhakikisha wanawatoa watu wote waliokuwa wamefukiwa mgodini yaani Watanzania 14 na Mchina mmoja, wakiwa salama.

Kamanda Mwabulambo alisema hata hivyo walifanya uokoaji kwa tahadhari kubwa kuhakikisha kwamba hakuna ambaye ataumizwa na vifaa ambavyo vilikuwa vikifukua na pia kusababisha hatari yoyote.

“Uokoaji ulifanyika kwa tahadhari kubwa kuhakikisha hatusababishi hatari yoyote kule ndani, lakini pia hatutafanya waumie, na kweli tulifanikiwa na kuwafikia wakiwa salama kabisa,” alieleza Kamanda Mwabulambo.

Mbali na Jeshi la Polisi, kazi ya uokoaji ilifanyika kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji, Mgodi wa Dhahabu wa Geita Gold Mine (GGM), Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, Busolwa Gold Mine pamoja na Kampuni ya RZ Union Mining Ltd ambayo inamilikiwa na Wachina.

Kamanda Mwabulambo alisema changamoto kubwa ilikuwa hawakuwa na ramani ambayo inaonesha kwa uhakika eneo ambalo watu hao walipokuwa, hivyo pamoja na kuwa na vifaa vya kutosha, lakini walipata shida kuwafikia.

Alisema juzi saa mbili usiku walipata mwanga kwamba watawapata wakiwa hai kwani walifanikiwa kufika eneo ambalo walikuwa wachimbaji hao ambapo walituma ujumbe nao wakajibu kwa kuandika kikaratasi kilichoeleza kuwa wako salama, lakini wanahitaji chakula, vinywaji na sigara.

Ujumbe huo ulikuwa ukisomeka, “tuko salama kumi na tano chakula ndio shida shusha soda, uji, bisikuti, watu wana njaa sana kuna mmoja amechomwa na msumari. Cha kufanya chakula, sigara, kiberiti, redio haikamati.”

Waliorodhesha pia majina yao kuwa ni Sabato Frimotojo, Mr Mo, Cheku Togwa, Ezekiel Bujiku, Rashid Shiringap, Rafael Nzumbi, Musa Mtanga Cosmas, Hassan Iddy, Agustin Robart, Mgarura Kayanda, Aman Sylvester, Dotto Juma, Yona Kachungwa, Dickson Morris na Aniset Masanja.

“Tulifanikiwa kuwadondoshea vyakula laini na vinywaji kwa kutumia mitambo ile na hiyo ndiyo iliyowasaidia hata leo (jana) walipotoka walikuwa katika hali nzuri na nguvu ya kutosha,” alisema Kamanda Mwabulambo.

Watu hao 15 walipotoka, walionekana kujaa matope mwili mzima, ikimaanisha mvua zilizonyesha ziliwaathiri. Walivuliwa nguo na vitu vingine vikiwamo kofia ngumu, ambazo walikuwa wamevaa wakati wakitumbukia katika mashimo hayo ya mgodi huo, Alhamisi iliyopita. Kamanda Mwabulambo alieleza kuwa hata hivyo ilikuwa ni kukisia tu, hawakuwa na uhakika kwamba ni eneo fulani, ndiko waliko watu ambao wanawatafuta. Alisema baada ya kutolewa, walipata huduma ya kwanza kabla ya kupelekwa hospitali kwa huduma zaidi ingawa hali zao zilikuwa nzuri.

Kamanda Mwabulambo alisema baada ya watu hao kuingia mgodini, ni watu waliokuwa juu ya mgodi, ndio waliona tukio la mlango huo wa kuingilia mgodini kujifunga. Hakika ilikuwa ni furaha ya aina yake walipokuwa wakitolewa wachimbaji hao kuanzia wa kwanza mpaka wa 15 tukio lililotokea kati ya saa 5.00 hadi saa 5.20 asubuhi.

Hali ya furaha ilitawala nje ya mgodi saa 5.20 baada wachimbaji wote 15 akiwemo Mchina, kuokolewa kutoka chini ya mgodi walikokaa kwa siku tatu. Familia za watu hao hazikuwa na amani katika siku zote hizo tatu wakihofia maisha ya ndugu zao.

“Kama unavyoelewa mtu unapoona ndugu yako, jamaa yako yuko katika hatari kubwa, hawa ndugu tulikuwa nao siku zote hawakuwa na amani kabisa wakihofia uhai wa ndugu zao,” alisema Kamanda Mwabulambo, akielezea hali ilivyokuwa baada ya wachimbaji hao kuokolewa.

Taarifa iliyokuwa ikitolewa awali ilibainisha kuwa watu waliofukiwa walikuwa 14 tofauti na waliotolewa jana. Watu hao walifukiwa chini ya mgodi baada ya mlango mmoja wa kuingilia kwenye shimo la mgodi huo kumeguka udongo na kujiziba.

Kati ya watu ambao walishuhudia wakati wachimbaji hao wakitolewa ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Jenerali mstaafu Ezekiel Kyunga. Mkuu wa Mkoa wa Geita alisema matukio ya wachimbaji wa madini ni ya kawaida katika maeneo ya uchimbaji, hata hivyo inategemea na mazingira katika uokoaji.

“Haya matukio huku sio jambo geni kabisa, unaweza kukuta tukio jingine kulingana na mazingira yake watu wakapoteza maisha na tukio jingine mkafanikiwa kuwaokoa lakini sio jambo geni,” alisema Kyunga.

Alisema pamoja na kwamba walikuwa na vifaa vya kutosha, lakini uokoaji ulichukua siku tatu kutokana na tahadhari kubwa waliyokuwa nayo kuhakikisha wanawatoa watu wakiwa salama.

“Ilibidi baada ya kutumia vifaa juu kutoa mchanga, tulipofika kwenye miamba kutumia chepe na kwenda polepole sana,” alisema Kyunga.

Awali ilielezwa kwamba kwa mujibu wa kitabu cha orodha ya watu wanaojiandikisha kuingia mgodini, kuna majina ya Watanzania 12 na Mchina pamoja na mtu mmoja ambaye alionekana kuingia, lakini hakuwa ameandika jina lake kwenye kitabu hicho.

Kyunga alisema wakati huo huo Januari 26, mwaka huu waokoaji walitoboa eneo jingine na kupitisha mabomba ya hewa ya oksijeni ili kuwafanya watu hao wasikose hewa.

Naye Dk Kalemani ametoa siku tano kwa Kamishna wa Madini kufanya ukaguzi katika mgodi huo na kusimamisha kazi mpaka utakapokaguliwa na kufanyiwa tathmini. Alimtaka pia kuchukua hatua kwa mhandisi anayesimamia mgodi huo baada ya tathmini, na pia kuunda timu ya watu saba kukagua migodi yote.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amemtumia salamu za pole na pongezi Mkuu wa Mkoa wa Geita, Kyunga kwa kazi nzuri na kubwa waliyoifanya ya kuwaokoa wachimbaji wadogo 15 waliofukiwa na maporomoko ya udongo kwenye Mgodi wa Dhahabu wa RZU uliopo katika Kijiji cha Nyarugusu, wakiwa hai.

Makamu wa Rais alisema amepokea kwa furaha taarifa za kuokolewa kwa wachimbaji hao wadogo na alisifu na kupongeza jitihada za kuwaokoa wachimbaji hao, zilizofanywa na Serikali ya Mkoa wa Geita, Jumuiya ya Wachimbaji Wadogo wa Mkoa wa Geita, wamiliki wa migodi ya dhahabu na wananchi kwa ujumla kwa kutoa vifaa mbalimbali vya uokoaji jitihada ambazo zimepelekea kuokolewa kwa wachimbaji hao wakiwa hai.

Makamu wa Rais aliwataka wamiliki wa migodi kote nchini, kuhakikisha wanafanya kazi zao za uchimbaji wa madini kwa kuzingatia kanuni, taratibu na sheria kama hatua ya kuepuka madhara yanayoweza kutokea wakiwa wanafanya shughuli zao za uchimbaji wa madini.

“Kupitia kwako Mkuu wa Mkoa wa Geita napenda kutuma salamu za pole kwa ndugu, jamaa na marafiki kufuatia kutokea kwa tukio hilo na nawaombea kwa Mwenyezi Mungu wachimbaji hao ambao kwa sasa wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Serikali ya Mkoa wa Geita matibabu mema ili waweze kupona haraka na kurejea kwenye kazi zao za kujitafutia riziki,” alieleza Makamu wa Rais.

ZeroDegree.
Walichosimulia waliofukiwa na kifusi mgodini kwa muda wa siku 3 Walichosimulia waliofukiwa na kifusi mgodini kwa muda wa siku 3 Reviewed by Zero Degree on 1/30/2017 11:30:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.