Loading...

Bidhaa feki zenye thamani ya milioni 500/= zateketezwa na Tume ya Ushindani Nchini [FCC]

Tingatinga likiteketeza kwa kukanyaga bidhaa mbalimbali kama vile vifaa vya kuunganisha umeme njia kubwa, betri za kompyuta mpakato, viatu, miswaki, redio, vifaa vya muziki na wino wa printa ambavyo vilikamatwa na Tume ya Ushindani (FCC) vyenye thamani ya sh milioni 517 kwenye maeneo mbalimbali kwa kipindi cha miaka miwili.
KATIKA kuwalinda walaji na bidhaa bandia, Tume ya Ushindani nchini (FCC) imeteketeza bidhaa mbalimbali zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 500, ikiwemo vifaa vya umeme kwa ajili ya transfoma.

Bidhaa hizo zikiwemo vifaa 1850 vya umeme kwa ajili ya kufungwa kwenye transfoma na njia za umeme vyenye thamani ya Sh milioni 231.2, vimekamatwa katika maeneo mbalimbali nchini kufuatia misako iliyofanyika ya kutokomeza bidhaa bandia sokoni.

Akizungumza wakati wa kuteketeza bidhaa hizo, Ofisa Mwandamizi Mawasiliano na Mahusiano wa Tume hiyo, Frank Mdimi alisema bidhaa hizo zimekamatwa katika msako uliofanywa katika mikoa ya Mbeya, Mwanza, Kilimanjaro, Arusha, Dar es Salaam na maeneo mengine ikiwemo bandari zote.

“Hizi ni bidhaa bandia ambazo zilikamtawa katika miaka miwili au mitatu iliyopita katika misako mbalimbali nchini hadi bandarini kitengo cha kontena pamoja na bandari kavu zote zinazohifadhi makontena yanayotoka bandarini,” alisema Mdimi.

Alizitaja bidhaa zilizokamatwa na thamani yake kwenye mabano ni miswaki katoni 200 (Sh milioni 96), mafuta ya karafuu chupa 100 (Sh 300,000), nyembe za Gillette katoni 13 zenye paketi 1728 (Sh milioni 2.6), viatu aina ya Timberland na Caterpillar jozi 500 (Sh milioni 30).

Bidhaa zingine ni wino wa printa aina ya HP, kisha 704 (Sh milioni 126.7), betri za kompyuta mpakato 363 (Sh milioni 54.4), chaji za kompyuta mpakato 88 (Sh milioni 4) na vitabu vya kuandikia (Sh milioni 2) ambavyo jumla yake ni Sh 517,272,000.

“Bidhaa hizi zinakamatwa kwa sababu zinaigiza miliki bunifu ya mtu mwingine, zinakiuka sheria ya alama za bidhaa kwa kuigiza miliki bunifu ya mtu mwingine na kumdanganya mlaji,” alisema Mdimi.

Alisema mara nyingi walaji ndio wamekuwa wakidanganyika na wakati mwingine huko mahali pa kulalamika na kupata sehemu ya kutatua migogoro iwapo bidhaa itaharibika, kwa kuwa hatakuwa na mtu wa kumdai kwasababu bidhaa hizo zi za mwenye miliki bunifu husika.

Alifafanua kuwa hatari ni kubwa zaidi katika vifaa vya umeme, ambavyo kama vinakosa sifa na vikaleta athari, vinaweza kusababisha hatari kubwa ya moto na hata kupoteza maisha ya watu na pia hakuna atakayelipa fidia kwa kuwa aliyeviuza hafahamiki.

Mdimi aliwataka wafanyabiashara kuhakikisha wanapouza bidhaa hizo, wanazitafuta kutoka katika vyanzo halisi na pia kampuni za kimataifa ambazo hazina viwanda vyao nchini, zinatakiwa kuhakikisha kuwa na wataalamu wao ili kulinda soko la bidhaa zao.

Aidha, aliwataka wananchi kuhakikisha wananunua bidhaa katika maeneo yanayofahamika, badala ya kununua katika maduka ambayo hayana sifa na kuhakikisha wanapewa risiti ili kuweza kudai haki yao, inapotokea bidhaa waliyonunua ina tatizo.

Source: Habari Leo
ZeroDegree.
Bidhaa feki zenye thamani ya milioni 500/= zateketezwa na Tume ya Ushindani Nchini [FCC] Bidhaa feki zenye thamani ya milioni 500/= zateketezwa na Tume ya Ushindani Nchini [FCC] Reviewed by Zero Degree on 1/01/2017 01:21:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.