Loading...

CCM yaishutumu Chadema kuvuruga uchaguzi mdogo Singida

Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Singida kimesikitishwa na kitendo cha CHADEMA kutumia vijana kuvuruga uchaguzi mdogo wa nafasi ya udiwani kata ya Kinapundu wilaya ya Mkalama kuwatishia wapiga kura wasitoke kupiga kura.

CCM imesema siku moja kabla ya kufanyika uchaguzi baadhi ya vijana wa CHADEMA walikuwa wakitembea na daftari la wapiga kura na kuwaendea wapiga kura.

Wapiga kura hasa wale wenye umri mkubwa walikuwa wanaonyeshwa picha zao na kutishiwa wasiende kupiga kura wakithubutu kupiga kura,watakiona cha mtema kuni.

Hayo yamesemwa na katibu CCM mkoa wa Singida, Mary Maziku wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake. Maziku alikuwa akitoa taarifa juu ya uchaguzi mdogo nafasi ya udiwani kata ya Kinapundu wilaya ya Mkalama.

“Naomba nitumie nafasi hii kuiomba serikali ifanye uchuguzi wa kina kujua vijana hao wamepata wapi daftari za wapiga kura. Kama watakuwa wamepata daftari hizo kinyume na sheria, wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vinavyohusika sheria iweze kuchukua mkondo wake,” alisema Maziku.

Pia alisema kuwa vijana wengine walipewa jukumu la kuiba kura kwa wapiga kura ambao wana mwelekeo hasi kwa wagombe wa UKUTA.

Katika hatua nyingine, Katibu Maziku alisema chama kinasikitishwa na kitendo cha mtumishi wa umma Katibu wa Chama cha Walimu (CWT) Tanzania wilaya ya Mlakama,kujihusisha na kampeni za kisiasa jambo ambalo ni kinyume na taratibu, kanuni na sheria za mikataba ya ajira.

“Huyu katibu wa CWT ambaye alionyesha wazi kuwa ni CHADEMA, alichofanya kwenye kampeni za uchaguzi Kinapundu ni kuiponda serikali wazi wazi huku akijua ndiyo iliyomwajiri,” alisema.

Katibu Maziku alisema uchaguzi mdogo umeisha na kilicho mbele ya CCM na wanachama wake ni kujipanga vizuri kwa ajili ya kushinda chaguzi zote zijazo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Singida, Shabani Limu, alisema wao wamefanya kampeni za kistaarabu tofauti na CCM ambao walitoa fedha na vifaa vya miradi ya ujenzi wa majengo ya shule katika kata hiyo wakati wa kampeni.

“Hata kama miradi hiyo ilikuwa na bajeti wakati diwani Helana Msengi Kitila hajafariki dunia ni kwanini wasiendelee kutekeleza muda wote huu wakati kampeni hazijaanza, wanasubiri katikati ya kampeni, ndio walete mabati mbao kwa ajili ya nyumba ya mwalimu na wajenge daraja katikati ya kampeni,” alisema.

Mwenyekiti huyo amesema tuhuma zilizotolewa na CCM, zote hazina mashiko.

Katika uchaguzi huo, Selvestar Yambi wa CCM alipata kura 1,409, Patrick Wazaeli wa CHADEMA 804 na Eriki Ali Hamisi wa CUF,41 na kura 69 ziliharibika. Uchaguzi huo umefanyika kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Helena Msengi Kitila wa CCM ambaye alifariki.

Source: DewjiBlog
ZeroDegree.
CCM yaishutumu Chadema kuvuruga uchaguzi mdogo Singida CCM yaishutumu Chadema kuvuruga uchaguzi mdogo Singida Reviewed by Zero Degree on 1/24/2017 09:50:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.