Loading...

Huyu hapa Jorge Sampoli, mkali aliyeziyeyusha ndoto za Kocha Zinedine Zidane

WAKATI Zinedine Zidane anapewa kibarua cha kuinoa Real Madrid, idadi kubwa ya wadau wa soka walidhani kuwa kazi hiyo ingekuwa kubwa kwake hasa kutokana na historia ya timu hiyo ya kutimua makocha kila kukicha.

Zidane ambaye si mgeni katika timu hiyo kutokana na kuichezea kwa mafanikio makubwa, alichukua kibarua hicho kutoka kwa kocha mkongwe wa zamani wa Liverpool, Rafael Benitez, aliyetimuliwa mchana kweupe kutokana na matokeo mabaya.

Wakati baadhi ya watu wakidhani kuwa kibarua hicho wangepewa makocha wakubwa na wazoefu, ghafla akatangazwa Zidane kuvaa viatu hivyo licha ya kwamba hajawahi kufundisha timu yoyote kubwa zaidi ya timu ya vijana ya kikosi hicho.

Zidane aliichukua timu katikati ya ligi ambapo wakati baadhi wakijiuliza kama anaweza kuiongoza klabu hiyo kubwa, ghafla mambo yakabadilika, soka likaanza kuchezwa la uhakika na matokeo yakapatikana.

Madrid walikuwa wameachwa mbali na Barcelona kutokana na matokeo waliyokuwa wakiyapata enzi za Benitez, lakini Zidane alipokamata usukani timu ikatishia nafasi ya wapinzani wao hao kileleni ambapo mpaka msimu unamalizika walipishana kwa pointi moja, Barcelona wakiwa kileleni na pointi 91 na kikosi cha Mfaransa huyo kikishika nafasi ya pili kikiwa na pointi 90.

Hali hiyo iliwafanya waliokuwa na wasiwasi na Zidane kuanza kutuliza mioyo yao, wakajua fika kwamba anastahili kuaminiwa na hicho ndicho ambacho ameendelea kukifanya msimu huu, kwani mpaka sasa ni mchezo mmoja tu kikosi hicho kimepoteza kati ya michezo 40 waliyocheza mpaka sasa.

Zidane alikuwa na malengo makubwa, msimu huu na bila shaka alikuwa anataka kuhakikisha anaumaliza bila kupoteza mchezo wowote lakini akakutana na mwanamume mwenzake, shoka la mpingo, Jorge Sampaoli, akamtuliza na kufuta kabisa kile kilichokuwa kichwani mwake.

Mfaransa huyo alikutana na kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Sevilla inayoongozwa na kocha huyo raia wa Argentina, mchezo wa ligi kuu nchini Hispania na kuwafanya Real Madrid, kupoteza mchezo mmoja kitu ambacho lazima kimemuumiza sana Zidane na wachezaji wake wakiongozwa na Cristiano Ronaldo.



Kitendo hicho kilichofanywa na Sevilla chini ya Sampaoli kwa Real Madrid, kinadhihirisha ukomavu wa kikosi hicho kwani hiyo si mara ya kwanza kufanya hivyo, waliwahi pia kuizima Barcelona katika harakati zao za kucheza michezo mingi bila kupoteza.

Katikati ya wiki iliyopita Sevilla walikuwa wenyeji wa Madrid mchezo wa Copa del Rey, timu hizo zikatoka sare ya kufungana mabao 3-3, huku Madrid wakisawazisha dakika za lala salama na walipokutana mchezo wa ligi mwishoni mwa wiki mambo yakawa magumu kwa Zidane na kikosi chake.

Kwa ujumla Sampaoli ni mgeni na Ligi Kuu nchini Hispania, kwani alijiunga na Sevilla Juni 27, 2016 yaani msimu uliopita lakini ndiye ambaye amekuwa kikwazo kwa Zidane anayeijua ligi hiyo kwa miaka mingi, kwani alianza akiwa kama mchezaji na sasa kama kocha Mkuu wa Real Madrid, hiyo ikimaanisha kuwa mpira hauna cha uzoefu, unaweza kuaibishwa muda wowote na sehemu yoyote.

Sampaoli ameipunguza nguvu ya Zidane na sasa Mfaransa huyo anatakiwa kuanza kujipanga upya, kwani akifanya vibaya michezo ijayo anaweza akajikuta anakutwa na wapinzani wao Barcelona kama si kuzidiwa kabisa na kupokonywa tonge mdomoni.

Kwa sasa ligi bado ni mbichi na kuhusu ubingwa hakuna mwenye uhakika wa moja kwa moja kwamba atautwaa, vinginevyo ni kusubiri kuangalia nini kitatokea na hapa la kujiuliza ni je, kipigo hicho kutoka kwa Sevilla ni mwanzo wa Zidane na kikosi chake kuanza kupotea au ndiyo kwanza watauwasha moto, n
goja tusubiri michezo inayokuja.

ZeroDegree.
Huyu hapa Jorge Sampoli, mkali aliyeziyeyusha ndoto za Kocha Zinedine Zidane Huyu hapa Jorge Sampoli, mkali aliyeziyeyusha ndoto za Kocha Zinedine Zidane Reviewed by Zero Degree on 1/18/2017 01:18:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.