Loading...

Serikali yasitisha mwongozo wa mihuri kwa wenyeviti wa mitaa na vijiji

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene
SERIKALI imesitisha mwongozo ilioutoa wa matumizi ya mihuri kwa wenyeviti wa mitaa na vijiji mpaka hapo utaratibu mwingine utakapoandaliwa.

Mwongozo huo ambao ulitolewa Novemba mwaka jana, ulikuwa ukiwataka wenyeviti wa Serikali za Mitaa na Vijiji kurudisha mhuri ambao ulitakiwa kubaki wa mtendaji.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene alisema hatua hiyo imefikiwa ili kuondoa mgongano ambao tayari umeshaanza kujitokeza sasa.

Tangu kutangazwa kwa mwongozo huo, wenyeviti wa mitaa walitishia kujiuzulu nyadhifa zao na kususa shughuli za serikali, ikiwa ni hatua ya kupinga kuwanyang’anya mihuri ya kufanyia kazi. Pia wenyeviti hao waliahidi kulipeleka suala hilo mahakamani kwa lengo la kwenda kutafuta tafsiri ya kisheria.

“Serikali hizi mbili (Serikali Kuu na Serikali za Mitaa) zimekuwa zikifanya kazi vizuri kwa muda, sioni sababu ya kuingia kwenye mgogoro, nimefuta mwongozo tulioutoa kwa sababu hatukusudii kuingia kwenye ugomvi. “Kwa sababu wenzetu (wenyeviti) mnafanya kazi ngumu katika mazingira magumu ya kuwahudumia wananchi hili jambo lisituletee shida, nasitisha mwongozo nilioutoa juu ya matumizi ya mihuri, mpaka pale tutakaposhirikishana na kuona namna bora ya kuendesha masuala ya kuwahudumia wananachi,” alisema Simbachawene.

Alisema hatua ya kutoa mwongozo wa matumizi ya mihuri kwa wenyeviti hao haikuwa na ajenda yoyote, zaidi ya kuondoa matatizo yaliyotokana na matumizi ya mihuri likiwemo tatizo la migogoro ya ardhi.

“Hatukuwa na ajenda yoyote ile, mwongozo ulitolewa ikiwa ni katika kuweka utaratibu mzuri ndio maana tuliona tutoe maelekeza hayo ambayo nia yake ni kushughulika na baadhi walioleta madhara makubwa,” aliongeza waziri huyo.

Simbachawene alisema haamini kama mihuri kuwa kwa watendaji ambao wanaweza kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria za ajira wakikosea, unawaondolea mamlaka na heshima na kusisitiza kuwa mamlaka ziko pale pale.

“Siamini wenyeviti kutokuwa na mihuri basi kunawapunguzia mamlaka na heshima. Mamlaka yao ipo pale pale…tulijiuliza je mamlaka ya mwenyekiti ipo kwenye muhuri? Uwepo wake na nguvu inatokana na uwepo wa mhuri, kama ndivyo basi rais angekuwa na mhuri. Nguvu ya mwenyekiti haijengwi kwenye mhuri bali maamuzi,” alisema.

Alisema katika kuhakikisha serikali inaondoa migongano ya matumizi ya ardhi, baada ya kufanya tafiti walibaini kuwapo na mwingiliano wa mamlaka na hususani mihuri iliyokuwa ikigongwa. “Baadhi ya wenyeviti wamekuwa hutumia mihuri ndivyo sivyo na hatukuwa na nia ya kuwapunguzia nguvu na heshima zao,”alisema Simbachawene.

Alisema migogoro mingi imetokana na saini na mihuri ya wenyeviti iliyokuwa ikigongwa kwenye hati na kutambuliwa kisheria kama ilivyo hati zinazotolewa na wizara.

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mwongozo, Kata ya Makuburi Wilaya ya Ubungo, James Ngoitamile alisema hatua itarahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Mwenyekiti wa Mtaa au Kijiji ndiye anayekaa eneo husika na anawafahamu wananchi wake, lakini mtendaji si lazima awe wa eneo hilo, na wananchi wanahitaji huduma nyingi,” alisema.

Source: Habari Leo
ZeroDegree.
Serikali yasitisha mwongozo wa mihuri kwa wenyeviti wa mitaa na vijiji Serikali yasitisha mwongozo wa mihuri kwa wenyeviti wa mitaa na vijiji Reviewed by Zero Degree on 1/18/2017 01:30:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.