Loading...

Msajili afunguka kuhusu milioni 400/= za ruzuku za CUF

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi.
MSAJILI wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, amefunguka kuhusu sakata la kutolewa kwa ruzuku kwa Chama cha Wananchi (CUF).

Akizungumza katika mahojiano na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Jaji Mutungi alisema ruzuku kwa CUF ya hivi karibuni imetolewa kihalali kwa uongozi wa chama unaotambuliwa na ofisi yake.

Alisema haijaibwa kama inavyoelezwa na baadhi ya watu.

CUF, ambayo ipo katika mgogoro wa kiuongozi ambao umepelekea chama hicho kumshtaki Msajili, miongoni mwa walalamikiwa watatu, katika Mahakama Kuu.

Ruzuku hiyo ya Sh. milioni 369 ilitolewa kwa CUF kupitia akaunti ya wilaya ya Temeke, badala ya taifa na kupelekea upande mmoja katika mvutano huo kudai kuibwa kwa fedha hizo.

“Ni kauli potofu kueleza kwamba ruzuku wamepewa upande wa CUF Bara kwa kuwa ofisi yangu inaamini kuwa ndani ya chama hicho hakuna mgogoro," alisema Jaji Mutungi.

"Na ruzuku hiyo imetolewa kwa uongozi wa chama unaotambuliwa na si vinginevyo, hivyo watu hawawezi kuzungumza kuwa ruzuku ya CUF imeibwa.”

Jaji Mutungi alisema pamoja na kuwepo kwa shutuma za wizi, katika hali ya kushangaza ofisi yake haijapokea malalamiko yoyote rasmi kutoka kwa viongozi halali wa CUF kuhusiana na yeye kukipatia ruzuku chama hicho.

Alisema viongozi na wanachama wa CUF ni lazima watambue kuwa njia sahihi ya kumaliza sintofahamu iliyopo ndani ya chama hicho ni vikao halali vya chama na kuheshimu uamuzi wa vikao hivyo na siyo kulalamika barabarani.

“Wapo baadhi ya watu wanaojiita viongozi wa CUF wanalalamika tu barabarani wakati ofisi yangu haiwatambui, wafuate taratibu," alisema.

"Kwanza nilikuwa sitaki kuzungumza suala hilo kwa kuwa linakuzwa mno na vyombo vya habari.

"Mgogoro wa chama hicho ulimalizwa tangu mwaka jana nilipotoa muongozo wa kikatiba wa CUF kuhusu kurejea kwa Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahimu Lipumba katika nafasi yake.”

Jaji Mutungi alisema kinachoendelea hivi sasa ni manung’uniko ya upande mmoja, kutokuridhika na uamuzi wake, jambo ambalo lingetokea hata kama upande wa Lipumba ungepata matokeo yasiyowapendeza.

Upande wa Lipumba unakinzana na kambi ya Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad ambao umeegemea zaidi Zanzibar.

Habari za kutolewa kwa ruzuku hiyo kwa upande wa Lipumba zilifichuliwa jijini Dar es Saalam wiki moja iliyopita na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi, Julius Mtatiro.

“Fedha hizo zilitoroshwa kutoka Hazina ya Serikali Januari 5 mwaka huu na kuingizwa kwenye Akaunti ya NMB tawi la Temeke yenye jina la The Civic United Front ikiwa na akaunti namba 2072300456,” alisema Mtatiro.

Septemba 26, mwaka jana wajumbe 43 wa Baraza Kuu la CUF katika kikao kilichoongozwa na Mbunge wa Tandahimba, Katani Katani walimfukuza uanachama Lipumba.

Uamuzi huo hatahivyo, hautambuliwi na Ofisi ya Msajili hivyo kupelekea upande wa Maalim Seif kumfungulia kesi Mahakama Kuu.
Kesi hiyo iliyofunguliwa na Bodi ya Wadhamini ya CUF ni dhidi ya Msajili, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Profesa Ibrahim

Lipumba na wanachama wengine 11 wa chama hicho. Inasikilizwa na Jaji Sekiet Kihiyo wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam.

Kesi hiyo ilifunguliwa chini ya hati ya dharura na CUF inawakilishwa na jopo la mawakili watatu - Juma Nassoro, Twaha Taslima na Hashim Mzirai.

Katika madai ya msingi, Bodi hiyo kwa niaba ya CUF inaiomba Mahakama Kuu mambo matatu ikiwamo kutengua barua ya Jaji Mutungi ya Septemba 23, mwaka huu, iliyotengua uamuzi halali wa kikao cha chama hicho.

Aidha, CUF inaomba mahakama kumzuia msajili huyo asiendelee kufuatilia suala la kufutwa kwa uanachama wa Prof. Lipumba.
Pia CUF inaomba Msajili azuiliwe kuingilia masuala yanayohusu chama hicho na abaki kusimamia na kuangalia usajili wa vyama vya siasa.

Oktoba 10 mahakama hiyo ilitoa kibali kwa bodi hiyo kufungua kesi ya madai dhidi ya walalamikiwa.

Source: Nipashe
ZeroDegree.
Msajili afunguka kuhusu milioni 400/= za ruzuku za CUF Msajili afunguka kuhusu milioni 400/= za ruzuku za CUF Reviewed by Zero Degree on 1/18/2017 11:24:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.