Loading...

Simba yavutwa mkia Morogoro

Mshambuliaji wa Simba, Juma Luizio (kushoto) akijaribu kumtoka beki wa Mtibwa, Henry Joseph Shindika wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro jana, ambapo timu hizo zilitoka suluhu. 
TIMU ya soka ya Simba imeshindwa kunyakua pointi tatu muhimu baada ya kutoka sare ya bila kufungana na timu ya soka ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini hapa.

Timu hizo katika kipindi cha kwanza zilicheza zaidi mpira kati kati na kufanya mashambulizi ya kushitukiza na kwa zamu, lakini Simba ikiwa imepata nafasi nyingi zaidi ya tatu katika kipindi hicho dhidi ya moja ya Mtibwa Sugar.

Mchezaji wa Mtibwa Sugar, Vicent Barnabas alikosa bao katika dakika ya 35 ya mchezo huo baada ya kupokea pasi ya Henry Joseph, lakini shuti lake lilipanguliwa na kipa wa Simba na mpira kuokolewa na beki Abdul Banda.

Simba ilifanya mashambulizi kupitia mchezaji wake Laurent Mavugo katika dakika ya 21, ambapo shuti lake lilipanguliwa na kipa wa Mtibwa Sugar, Said Mohamed na kuokolewa na mabeki wa timu hiyo.

Mavugo alikosa tena bao la wazi katika dakika ya 40, baada ya kupasiwa mpira na Mwinyi Kazimoto, ambapo shuti lake lilitoka sentimita chache juu ya lango la Mtibwa Sugar.

Katika kipindi hicho cha kwanza mpira ulichezwa zaidi kati kati ya uwanja, huku kila timu ikifanya mashambulizi ya kushitukiza na hadi mapumziko timu hiyo zilitoka uwanjani zikiwa suluhu.

Kipindi cha pili Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog katika dakika ya 58 alimtoa mshambuliaji Mavugo na kumwingiza Ibrahim Ajib ambaye aliongeza uhai katika safu ya ushambuliaji akishirikiana na Kichuya na Juma Liuzio na kusukuma mashambulizi ya mara kwa mara na kusababisha kona nyingi upande wa Mtibwa Sugar, ambazo hata hivyo hazikuzaa matunda.

Kocha Omog pia alimtoa Mwinyi Kazimoto na kumwingiza Pastori Atanas na pia kumtoa Kichuya na kumwingiza Mzamili Yassin ikiwa ni hatua ya kusaka mabao.

Lakini ukuta wa timu ya Mtibwa Sugar ikiongozwa Salim Mbonde, Shaaban Nditi na Issa Rashid wakikaa imara kuzuia mashambulizi ya wachezaji wa Simba.

Zikiwa zimesalia dakika 15, wachezaji wa Simba waliongeza juhudi za kutafuta mabao ya ushindi wa kuweza kuondoka na pointi tatu muhimu, ambapo katika dakika ya 75 na 80, mchezaji Ajib alikosa bao la wazi baada ya shuti lake kupanguliwa na kipa wa Mtibwa Sugar.

ZeroDegree.
Simba yavutwa mkia Morogoro Simba yavutwa mkia Morogoro Reviewed by Zero Degree on 1/19/2017 11:11:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.